Yapo makosa watu wanayafanya kwenye maisha yao pasipo kukusudia kabisa.

Wapo wanafanya kutokana na kushindwa kuzuia hasira zao.

Wapo madereva wanaua watu barabarani sio kwa sababu walikusudia kufanya hayo. Wala sio kwa sababu ya uzembe.

Wanajikuta wameua kutokana na mazingira yenyewe waliyokutana nayo.

Watu kama hao wanaofanya mambo mabaya pasipo kukusudia, na maisha yao yanakuwa hatarani kwa jamii inayomzunguka.

Wanahitaji hifadhi kunusuru maisha yao, sio hilo tu unawasaidia kutuliza akili zao wasije wakaharibikiwa zaidi.

Maana wapo watu wakipatwa na mambo mazito, tena yale ambayo hawakuyakusudia. Huwa wanapaniki sana na wasipopata watu wa kuwasikiliza na kuwashauri, na kuwatuliza mahali.

Watu hao wanaweza kupata madhara makubwa kuliko yale waliyoyafanya.

Kwanini mahali pa makimbilio ni muhimu? Hii ni kwa ajili ya wale wanaofanya mambo mabaya wasiyoyakusudia.

Wanapokimbilia mahali wanapoona panawafaa wao, inawasaidia kujihifadhi hadi pale hali itakapokuwa shwari.

Hili tunajifunza kupitia maandiko ya Biblia, yanatuonyesha vile wana wa Israel waliagizwa kutenga mahali pa makimbilio.

Rejea: Nena wewe na wana wa Israeli, uwaambie, Haya, toeni hiyo miji ya makimbilio, ambayo niliwaambia habari zake kwa mkono wa Musa; ili kwamba mwenye kuua mtu, aliyemwua mtu awaye yote pasipo kukusudia, na pasipo kujua, apate kukimbilia kuko; nayo itakuwa ni mahali pa kukimbilia kwenu, kumkimbia huyo ajilipizaye kisasi cha damu. YOS. 20:2‭-‬3 SUV.

Haya yalikuwa maalumu kwa wale watu ambao watafanya makosa pasipo kukusudia, na ikathibitika hivyo.

Hili halipaswi kuwa kama historia za zamani, hili tunapaswa kulielewa na kuliweka kwenye matendo.

Atakuja mtoto wa ndugu yako au wajirani yako, au wa kijijini kwenu, anataka umhifadhi kwako na umtunze ndani kwako. Kwa usalama wa maisha yake.

Kama hutokuwa na maarifa haya hutoweza kufanya hivyo kwa kuogopa kwako.

Wakati ungeweza kukaa na familia yako, au wazee, au uongozi wa mtaa, au kijiji au kata, ukawaeleza shida iliyompata huyo mtu. Na nia yako njema ya kumhifadhi ili asije akauawa.

Atakuja mtumishi mwenzako mwenye kuhitaji hifadhi ya muda kutokana na yale yaliyomtokea huko alikokimbia.

Pasipo kuwa na maarifa haya hutoweza kumsaidia mtumishi mwenzako, hutoweza kabisa nakwambia.

Nakusihi sana uwe sehemu ya kuwasaidia wale wenye mambo magumu, ambayo wamekueleza na ukaelewa kweli hawakukusudia kufanya hayo.

Mungu akubariki sana
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255 759 80 80 81.