Upo kwenye wakati mgumu sasa, ,hiyo inaeleweka, je unaona nini mbele yako? Je! Unaona kufanikiwa au unaona kushindwa?

Je! Unaona nini kwenye huduma yako? Je! Unaona kufanikiwa au unaona kushindwa? Je unaona kupanda viwango vya kihuduma au unaona kusinyaa kihuduma?

Je! Unaona nini kwenye mahusiano yako ya uchumba? Je unaona kuna kuolewa/kuoa? Au unaona hakuna cha ndoa ila umeamua kung’ang’ana na hayo mahusiano yasiyo na matunda.

Je! Unaona nini kwenye ndoa yako? Ndoa yako ina amani au imegeuka uwanja wa vita, na kama imegeuka uwanja wa vita. Je! Unaona kuna tumaini la kurudi kwenye hali yake nzuri au unaona kusambaratika?

Je! Unaona nini kwenye kazi yako miaka 10 ijayo? Je Unajiona utakuwa pale pale ulipo au unajiona utakuwa umesogea hatua nyingine kubwa?

Je! Unaona nini kwenye biashara yako miaka 5 ijayo? Je! Unajiona mfanyabiashara mkubwa mwenye mafanikio makubwa au unajiona utakuwa mtu wa chini kama unavyojiona sasa?

Je! Unaona nini kwenye maisha yako ya kiroho miaka ijayo? Je! Unajiona kukua zaidi kiroho au unajiona utakuwa umeshuka zaidi kiroho?

Majibu ya maswali haya yote unaweza ukawa nayo kutokana na unavyoiishi leo yako. Vile unajiweka leo, vile unaweka bidii zako leo kwa unachofanya, vile unatoa maisha yako kwa mambo ya Mungu. Ni majibu tosha ya kesho yako.

Mungu anamuuliza nabii Yeremia, unaona nini? Na wewe leo unaulizwa unaona nini katika maisha yako. Je! Unaona matatizo yako uliyonayo leo au unaona kesho yako iliyo njema?

Unaona kutokuolewa kwako au unajiona mama aliye na nyumba yake nzuri, mama mwenye familia safi inayomcha Mungu. Vile unaishi leo ndio inaweza kuleta matokeo chanya.

Rejea: Ndipo BWANA akaniambia, Unaona nini Yeremia? Nikasema, Naona tini; tini nzuri zilizo nzuri sana; na tini mbovu zilizo mbovu sana, zisizoweza kuliwa, kwa kuwa ni mbovu sana. YER. 24:3 SUV.

Leo unaweza ukawa na mahusiano mazuri ya uchumba yenye furaha, lakini ukitazama kesho yako unaona ni ndoa iliyojaa mafarakano makubwa. Ukiona hivyo rudi haraka mbele za Mungu usahishe mambo kabla haijawa jioni.

Leo unaweza ukawa na hali duni ya kimaisha, ila ukawa unaiona kesho yako yenye mafanikio makubwa. Ukiona hivyo endelea kumtegemea na kumtumaini Mungu wako siku zote, bila kuchoka.

Tazama kile unachokiona mbele yako, usitazame madhaifu uliyonayo leo, hayo ni ya muda tu, inakuja siku utayaacha hayo yote. Utakuwa na maisha mengine mapya kabisa ila lazima uvumilie hali uliyonayo sasa.

Mungu akupe ufahamu uweze kuelewa haya.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.