Linaweza likawa ni swali ambalo hujawahi kukaa chini ukajiuliza, wala hujawahi kukaa chini ukatengeneza tafakari inayohusiana na hili swali.

Ama huenda umewahi kukaa chini ukajiuliza hili swali moyoni mwako, na ukatengeneza tafakari nzito ndani ya moyo wako.

Hayo yote mojawapo huenda limekutokea katika maisha yako, na huenda pamoja na kukutokea hukuwahi kukaa chini ukaona ni jambo ambalo linahitaji utulivu. Ili ulione ni la muhimu na linahitaji kuwekwa katika matendo.

Leo tunaweza kujifunza hili kwa upana zaidi ukaondoka na somo la kukusaidia katika maisha yako ya kiroho na kimwili.

Tunapoishi na watu, tunahitaji kuwaachia alama kwenye mioyo yao, kule kutimiza kusudi la Mungu katika maisha yetu. Tukifanya katika Mungu, lazima tuweke alama njema, na tuache alama njema tunapoondoka maeneo tulikuwepo, na tusipokuwepo duniani.

Vizuri zaidi tukaona hili tukiwepo hai, ulikuwa umeajiriwa ofisi fulani, je unapohamishwa wale uliokuwa unafanya nao kazi wanaona pengo lako? Kama ni ndio unaona ishara kweli au ndio muda wao wa kufurahia kuondoka kwako?

Ikatokea viongozi wako wakakuletea fitina za kukuhamisha/kukuondoa kwa hila. Je wale uliokuwa unawaongoza wapo tayari kusimama na wewe kutokana na mchango wako mkubwa uliouonyesha kwao?

Unaishi nyumbani kwa wazazi/walezi wako, siku unaaga kuondoka hapo nyumbani, kutokana na mchango wako mkubwa hapo nyumbani. Utaona hawataki kusikia kuaga kwako, bali wanatamani kukuona ukiwasaidia.

Haya sio maneno ya hewani, haya yapo kibiblia, wapo watu waliokatazwa kuondoka kutokana na mchango wao uliokuwepo.

Rejea: Kisha Musa akamwambia Hobabu, mwana wa Reueli Mmidiani, mkwewe Musa, Sisi twasafiri kwenenda mahali ambapo BWANA amenena habari zake hivi, Nitawapa ninyi mahali hapo; uje pamoja nasi, nasi tutakufanyia mema; kwa kuwa BWANA ametamka mema juu ya Israeli. HES. 10:29 SUV.

Huyu ni Musa anamweleza shemeji yake Hobabu, anamweleza mahali ambapo Mungu amewaambia waende.

Baada ya kumweleza sasa hiyo habari, Hobabu alimwambia yeye haendi wanapotaka kwenda. Badala yake atarudi kwao.

Rejea: Naye akamwambia, Siendi mimi; ila nitairudia nchi yangu mwenyewe, na kwa jamaa zangu mwenyewe. HES. 10:30 SUV.

Sasa tunakuja kwa yale niliyoanza kukueleza mwanzo kwenye somo hili, Musa alimzuia na kumsihi waende naye wanapoenda.

Nini kilimsukuma Musa kumzuia shemeji yake Hobabu asirudi kwao, ule mchango wake aliokuwa nao wakati wapo naye.

Rejea: Naye akamwambia, Usituache, tafadhali; kwa kuwa wewe wajua jinsi tutakavyopanga nyikani, nawe utakuwa kwetu badala ya macho. HES. 10:31 SUV.

Tupo pamoja hadi hapo, tena akamwahidi kuwa kile BWANA atawatendea ndivyo na wao watamtendea na yeye Hobabu.

Rejea: Itakuwa, ukienda pamoja nasi, naam, itakuwa mema yo yote BWANA atakayotutendea sisi, tutakutendea wewe vivyo. HES. 10:32 SUV.

Sawa na leo unaambiwa usiondoke tutakuongezea kiasi cha mshahara unaotaka wewe uongezwe, usiondoke tutakufanyia yale ambayo ulituoomba tukufanyie.

Haya hayaji tu, yanakuja kutokana na utendaji wako wa kazi, kutokana na kujituma kwako, kutokana na kujitoa kwako katika kumtumikia Mungu, kutokana mema yako uliyowatendea wengine.

Hata wewe leo unaweza kuacha alama njema, unaweza ukawafanya watu wakalia kwa kukukosa kwenye nafasi fulani uliyokuwepo.

Jitume sasa kwa moyo wako wote, kwa nguvu zako zote, kwa akili zako zote, ipo siku utaona na kuvuna matunda ya kutumika na kujitoa kwako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081