“Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu”, Mal 3:8 SUV.

Waisraeli walikuwa wanamwimbia Mungu sana kwa kushindwa kuleta zaka zao (sehemu ya kumi ya mapato yao).

Katika sheria ya Musa watu au Waisraeli walitakiwa kutoa zaka walizoamriwa kutoa kutokana na maelekezo waliyopewa.

“Tena zaka yote ya nchi, kama ni mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi, ni ya BWANA; ni takatifu kwa BWANA”, Law 27:30 SUV.

Mungu alitishia kuwalaani wale ambao kwa uchoyo tu hawakutaka kutoa (Mal. 3:8-9) na kuwabariki wale “waliotegemeza kazi yake” (Mal. 3:10-12)

Waamini wa Agano Jipya ambao ni mimi na wewe tunapaswa kuelewa halikuwa jambo la Waisraeli tu, tunatakiwa kutoa kutokana na vipato vyetu ili kuitegemeza kazi ya Bwana.

Tunapotoa sehemu ya mapato yetu, tunaitegemeza nyumba ya Bwana, yapo matumizi mbalimbali hemani mwa Bwana.

Tunapotoa tunasaidia injili ya Bwana kwenda mbele, watumishi wa Mungu wanafanya kazi ya Bwana kwa urahisi bila kupata shida ya uchumi.

“Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao; wakituomba sana pamoja na kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu. Tena walitenda hivi si kama tulivyotumaini tu, bali kwanza walijitoa nafsi zao kwa Bwana; na kwetu pia, kwa mapenzi ya Mungu”, 2 Kor 8:3‭-‬5 SUV.

Shetani anajua hili, ndio maana hili eneo lina vita sana, yapo mafundisho yanayozuia watu wasitoe, na wapo wakristo wameacha kutoa.

Shetani anajua watu wanapotoa kuna baraka za Kimungu zinaachiliwa kwao, na watu bila kujua wameacha kutoa, wanapoacha hawajui kuna watu wengine wanatolea miungu yao sadaka.

Sisi hatupaswi kuwa hivyo, tunapaswa kumtolea Mungu zaka/sadaka zetu, kufanya hivyo tutakuwa tumefanya jambo linalompendeza Mungu wetu, kwa sababu yeye ndiye hatupaye.

Kila mmoja afanye kutokana na uwezo wake kutokana na kipato chake, fanya kwa moyo wa kupenda na Mungu atakubariki sana.

Usiache kuungana nasi kwa njia ya wasap kwa ajili ya kusoma na kutafakari neno la Mungu kila siku. Hii itakufanya ukomae kiroho na kuacha kuyumbishwa kiimani.

Mungu akubariki sana
Soma neno ukue kiroho
Samson Ernest
+255759808081