“Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum”, Mt 10:28 SUV.

Zipo dhana nyingi juu ya hili, wapo wanakataa kuwa hakuna jehanum, wapo wanakubali kuwa ipo, wapo wanaamini ukishakufa basi, na wengine wanaamini Mungu hawezi kumwangamiza mwanadamu kutokana na upendo wake.

Wapo wengine wakachanganyikiwa zaidi na kuamua kusema “bora kuishi maisha matakatifu ukafika mbinguni ukamkosa Mungu kuliko kuishi maisha machafu ukafika mbinguni ukakutana naye”.

Hizi ni kauli za watu ambao imani yao imepigwa na mafundisho yasiyo sahihi, wanaona wanachanganyikiwa, lakini bado mwanga wa tumaini upo kwa mbali, wanaamua kujiendea tu huku wakijiambia kuishi maisha yanayompendeza Mungu.

Hapa tutaenda kujifunza zaidi kuhusu jehanamu, sio somo la kutia moyo sana na kuhamasisha ila ukweli ni muhimu kwa mwanadamu, awe ana lengo la kwenda mbinguni au kuishi maisha ya umilele au hana lengo hilo.

Kwanza tunaposema au tunapozungumzia neno “jehanamu” tunazungumzia mahali pa mateso ya milele kwa wasiomcha Mungu, ama unaweza kusema wasiomkiri Kristo na wasio na matendo mema.

“Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika; [ ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki”, Mk 9:43, 48 SUV.

Moja ya siku kuu ya jehanamu ni hii, funza wasiokufa na moto wake hauzimiki, unaweza kuona ni kama stori fulani za watu ambao hawawapendi wenzao ila ukweli huu umethibitishwa na maandiko matakatifu.

Biblia inatufundisha na kutuweka wazi kuwa uhai wa mtu hauishii pale anapokufa bali unaendelea milele, itagemeana na matendo ya mtu mwenyewe, ama awe kwenye uwepo wa Mungu au sehemu ya adhabu.

Mambo 4 ya kufahamu kuhusu hali ya waliopotea au wanaotenda mambo yasiyompendeza Mungu au wasiookoka;

  1. Yesu alifundisha kwamba kuna sehemu ya adhabu ya milele kwa watakaohukumiwa mbele za Mungu (Mt 5:22, Lk 10:15).

Ni ukweli usiopingika hata kama wengine hawataki kuukubali, kuna adhabu isiyo na kikomo, sehemu ambapo moto wake hauzimiki milele (Mk 9:43), sehemu ya moto wa milele alioandaliwa Ibilisi na malaika zake (Mt 25:41).

Sehemu ambayo kutakuwa na kulia na kusaga meno (Mt 13:42), mateso ya kutisha sana, sio hilo tu kutakuwa na kutengwa kabisa na mbingu (Lk 16:23), wakati huo hakuna nafasi nyingine ya kutengeneza mambo yako.

  1. Mafundisho ya nyaraka mbalimbali katika Biblia hayatofautiani, mitume wanazungumzia hukumu ijayo ya Mungu ili kuwapatiliza wote wasiotii Injili ya kweli (2The 1:5-9), vilevile kutengwa kutoka kwenye uwepo na ukuu wa Bwana na maangamizo ya maadui wa Mungu (Flp 3:18-19).
  1. Biblia inatuweka wazi na kutufundisha ya kwamba hukumu juu ya watenda maovu wote ni hakika na sio habari ya kusadikika. Wazo kubwa ni kutupwa katika adhabu ya milele, kuteseka milele, kutengwa na Mungu milele yaani muda usio na mwisho au ukomo.

Wakristo wengi hasa kizazi cha sasa wanaweza kuona mafundisho haya sio mazuri kwao, au ni magumu kueleweka. Pamoja na kuona hivyo inatubidi kuelewa na kujitenga na maovu yote na kulitii na kulinyenyekea neno la Mungu.

  1. Tunapaswa kukumbuka kila mara ya kuwa Mungu alimtuma Mwanawe wa pekee aje afe ili mtu yeyote asipotee bali awe na uzima wa milele (Yn 3:16).

Lengo la Mungu si kupeleka watu jehanamu, kumbuka hilo! angekuwa na lengo hilo asingeleta njia ya kumwendea yeye baada ya Adamu na Hawa kukosea pale bustani ya Edeni.

Wale watakaoingia jehanamu sio kwa sababu Mungu hakuwapenda, ni kwa sababu walikataa au walipinga wokovu uliotolewa na Mungu bure kwa mwanadamu (Rum 1:16, 2:10)

Ukweli huu na uhalisia huu wa jehanamu, unapaswa kuwafanya watu wote wa Mungu wachukie kutenda dhambi kwa kila hali, waendelee kuwahubiri wengine habari njema za wokovu kwa wasioamini na kuwarejesha wale waliopotea. Na kuendelea kuwaonya na kuwakumbusha watu kuhusu hukumu ijayo ya Mungu (Ufu 20:14).

Tukielewa na kutii haya, tutakula mema ya nchi, tutafurahi pamoja na Bwana Yesu baada ya maisha haya ya dunia hii, sio jambo la kukosa kabisa kwa kila mmoja, tumwamini Kristo na kuishi maisha matakatifu.

Mwisho, nikualike kwenye kundi la wasap la kusoma na kutafakari neno la Mungu kila siku, kundi hili lina mkusanyiko mkubwa wa watu wanaopenda kujifunza, ukiingia utaambukizwa tabia ya kusoma biblia. Wasiliana nasi kwa wasap namba +255759808081 utaunganishwa.

Soma neno ukue kiroho

Mungu akubariki sana

Samson Ernest