Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye, jina lipitalo majina yote, jina lenye nguvu, jina lenye kuogofya nguvu zote za giza, kila litamkwapo, wagonjwa wanapokea uzima.

Sio kila kitu tutaweza kukumbuka kumuuliza Mungu, ila yapo mambo lazima useme na Mungu kwanza ndipo akupe kibali cha kukabiliana nayo.

Jambo hilo linaweza lisiwe la hatari ila unapaswa kumwambia Mungu, ili yeye akutangulie usije ukakwama njiani.

Kumtanguliza Mungu inakupa nafasi wewe, Mungu kuhusika na jambo lako kila hatua utakazopiga.

Usione jambo dogo, kuwa na tabia ya kumwomba Mungu akutangulie kwa jambo hilo, utaona nguvu za Mungu na uwepo wake katika kufanikisha jambo lako.

Haya tunajifunza kwa mfalme Daudi, aliyemuuliza Mungu kuhusu maadui zake wafilisti waliokuja kumvamia.

Kabla hajaenda kupigana nao, aliomba kwanza kibali cha Mungu anasemaje kuhusu vita ile.

Tunaona Mungu akimpa kibali Daudi na akamruhusu kwenda kupigana na wafilisti.

Rejea; Daudi akamwuliza Mungu, kusema, Je! Nipande juu ya Wafilisti! Utawatia mikononi mwangu? Naye Bwana akamwambia, Panda; kwa kuwa nitawatia mikononi mwako. 1 Nya 14 :10.

Usijitangulize tu mwenyewe, mtangulize Mungu kwanza, haijalishi hilo jambo ni ngumu kiasi gani, mtangulize Mungu.

Kumwomba Mungu kabla ya kuchukua hatua, inamfanya Mungu aone nidhamu/utii wako kwake, na inamruhusu Mungu akufunike na nguvu zake, ili usije ukapata madhara kwa jambo/vita iliyopo mbele yako.

Huenda katika huduma, mtangulize Mungu kwanza kabla hujaanza kwenda.

Huenda ni shule/chuo, mtangulize Mungu akutangulie kwenye masomo/mafunzo yako ili uweze kuibuka mshindi.

Huenda katika kutafuta mke/mume, mtangulize Mungu akahusike na jambo lako ili unapokutana na mke/mume wako usiwe na mashaka naye.

Huenda katika kukamilisha ndoa yenu na mchumba wako, mtangulize Mungu kwa maombi, usitumie tu akili zako, zitumie ila hakikisha zimetiwa kibali na Mungu.

Familia yako inamwitaji sana MUNGU, haijalishi upo mwaka wa kumi kwenye ndoa, bado unamwitaji Mungu ahusike na ndoa yako.

Haijalishi upo kwenye huduma mwaka wa 20 sasa, bado unamwitaji sana MUNGU akutangulie katika huduma yako.

Tamani kumwona Mungu akiwa ameambatana na wewe katika jambo unalofanya/unalotaka kufanya, usiwe peke yako, mshirikishe Mungu kwanza.

Mungu akubariki sana.

Samson Ernest.
+255759808081.