Haleluya,

Tunapenda kuona tukiwa Nyakati za furaha tu, hatupendi kuona tukiwa kwenye nyakati za majonzi, hatupendi kuona tukiwa kwenye nyakati za kuugua miili yetu, hatupendi kuona tukiwa kwenye nyakati za kudhulumiwa mali zetu, na hatupendi kuona tukipoteza vitu vyetu vya thamani.

Hatupendi kuona tukipishana kauli na ndugu zetu, marafiki zetu, wafanyakazi wenzetu, wapenzi wetu, na watoto wetu. Tunapenda kuona tukiwa na amani siku zote za maisha yetu.

Hata unapoingia kwenye ndoa unaambiwa hatutegemei kuwaona mkikogombana, wazazi na watumishi wa Mungu wanategemea kuwaona mkiwa wenye furaha na amani. Hayo yote mazuri hakuna asiyependa kuyaona katika maisha yake, na mtu wa Mungu lazima apende amani.

Lakini pamoja na hayo yote, hakuna nyakati zinazodumu, najua hupendi kusikia hili. Ila fahamu kwamba hakuna kizuri kinachodumu, wala hakuna kibaya kinachodumu katika maisha ya mwanadamu.

Ukijiona una furaha nyingi sana, uwe a uhakika huzuni I karibu sana kukujia, ukijiona una huzuni sana ujue furaha I karibu sana kukujia.

Ukijiona unasumbuliwa sana na upweke, ujue hilo jambo halina muda mrefu sana litakuondoka. Na utasahau kabisa hiyo hali kama umewahi kuwa nayo.

Ukiona familia yako imejaa sana amani na furaha, yaja siku ya kuondoa hiyo furaha. Yaweza kuwa katikati yenu kifo kitawatenganisha naye, yaweza kuwa katikati yenu ugonjwa utamfanya asiwe karibu nanyi, yaweza kuwa katikati yenu ajali mbaya itawatenganisha naye.

Ukisikia hivyo unajisikia vibaya sio, wala usijikie vibaya sana ukashindwa kunielewa. Hii ni ili uwe tayari kukabiliana na hali hizi zitakapokujia katika maisha yako. Maana kila unachokiona kizuri kitafika wakati kitakuletea huzuni, kinaweza kisiwe cha kuangamiza maisha yako. Ila jua kuwa kuna siku hutoweza kuwa na furaha yako.

Unaona biashara zako zinaenda vizuri sana, fahamu ipo siku zitaenda vibaya, tena vibaya haswa. Unapaswa kujipanga kifikra ili ikitokea usiwe na wasiwasi ambao utakufanya upoteze mwelekeo wako.

Unaona leo una kazi nzuri, cheo kizuri, kila mtu ofisini anakuita boss, yaani hakuna kinachopita ofisini pasipo wewe kutia saini. Fahamu ipo siku hutokuwa na hicho cheo kazini kwako, weka akilini mwako kabisa ipo siku hutokuwa na hayo mamlaka uliyonayo sasa.

Chochote unachokiona leo ni kizuri sana katika maisha yako, ipo siku kitageuka huzuni kwako, ipo siku kitakuwa kichungu sana kwako. Pamoja na kugeuka kote huko, hizo hali hazitadumu milele, nazo zitageuka na kuwa nyakati zenye furaha kuu.

Haijalishi unapitia katika hali gani sasa, iwe nzuri au iwe mbaya sana. Fahamu haitadumu siku zote za maisha yako, ni kipindi cha muda fulani tu.

Hebu turejee maandiko matakatifu kwa ufupi, tuone yanatuhusia nini kuhusu haya ninayokueleza hapa;

Rejea: Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kungoa yaliyopandwa; Wakati wa kuua, na wakati wa kupoza; Wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga; Wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; Wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza; Wakati wa kutupa mawe, na wakati wa kukusanya mawe; Wakati wa kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia; Wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza; Wakati wa kuweka, na wakati wa kutupa; Wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; Wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena; Wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; Wakati wa vita, na wakati wa amani. MHU. 3:1‭-‬8 SUV

Upo pia wakati wa vita, na upo pia wakati wa amani, unaweza kuona amani imejaa sana nyumbani kwako. Ufahamu kwamba utakuja wakati ambao hutokuwa na amani kabisa, vivyo hivyo kwenye nchi yako unapoishi.

Kwa kuwa hatuna maarifa sahihi ya Neno la Mungu, tupatwapo na hali hizi, huanza kufikiri tumepatwa na mikosi na balaa. Huanza kufikiri tumepoteza uhusiano wetu na Mungu.

Rejea: Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho. MHU. 3:11 SUV

Daka haya na uyaweka akilini mwako, kama leo unapendwa sana, fahamu upo wakati watu watakuchukia sana. Ukielewa haya hutopata shida siku yamekukuta hayo.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.