Ndugu yangu katika Kristo, nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, habari za muda huu, bila shaka siku umeimaliza kwa ushindi mkubwa. Maana kufikia mpaka muda huu, ni neema tu ya Mungu imekufikisha, pamoja na changamoto mbalimbali za maisha unazokutana nazo, Mungu bado anaendelea kukupa pumzi yake.

Kama hujawahi kujua thamani uliyonayo mbele za Mungu baada ya kuokoka, naomba ufahamu leo kuwa wewe ni wa viwango vya juu sana. Miongoni mwa watu ambao wamechagua fungu lililo jema ni pamoja na wewe uliyeokoka, na kuachana na ya dunia.

Unaweza usielewe sana hili, kutokana na changamoto mbalimbali za maisha, lakini wakati unaendelea kusoma ujumbe huu naamini kuna kitu unaenda kuondoka nacho. Ambacho kitakuwa na msaada kwako, kuepuka kutishwa tishwa na adui shetani popote pale utakapokuwa.

Kuna wakati tunaonekana wanyonge kutokana na mazingira tunapokuwa, unajikuta upo eneo ambalo labda wewe ndio peke yako unamjua Kristo. Kutokana na upeke yako ule, unaanza kukosa ujasiri wa kujitambulisha kuwa wewe umeokoka.

Labda tuseme umeenda sehemu ukakutana na marafiki ambao wote hawajamjua Kristo, japo wanaenda kanisani lakini unaona matendo yao yanamkataa Kristo kabisa. Kwa kuwa unaongopa kutengana nao, unaanza kuwafuatisha yale mabaya wanayotenda.

Bila shaka utakuwa hujui thamani ya wokovu wako, kijana makini anayejitambua yeye ni nani mbele za Mungu, hawezi kuzuiliwa na mazingira ya aina yeyote ile kujibadili tabia yake.

Unakutana na mtu anakwambia, unajua bwana sio vizuri kumtaja YESU au Sio vizuri kujulikana umeokoka kuna mambo mazuri utayakosa. Unakuta mambo yenyewe mazuri labda kutembea na wadada/wakaka, kwa uasherati.

Fahamu hili na uliweke ndani ya moyo wako, walio na Yesu wana amani nyingi, wana heri nyingi, wana ushindi wa maisha yao kiroho na kimwili, hawana hofu yeyote ya maisha. Hawatishwi sana na nyakati, hata kama kibinadamu yanayonekana mazingira ni magumu na hayawezekani. Kwao wanaona yanawezekana, wanaona upo ushidi kwao.

Tuliye naye ni mkuu sana, vyote vinavyoonekana na visivyoonekana, yeye ameviumba, miliki zote ni zake. Hakuna linaloshindikana kwake, hakuna jambo kubwa linaweza kukutokea katika maisha yako, litapate nafasi ya kukumaliza.

Utasema haya umeyatoa wapi wewe, ina maana niwe jasiri wakati naona naenda kumalizwa, labda umemsahau Daudi aliyemwona Goliati mfu lakini Sauli na jeshi lake walimwona ni jitu la kutisha. Labda umemsahau Daniel waliyemwona kitoweo cha simba, akatupiwa ndani ya tundu la simba. Lakini akatoka akiwa mzima wa afya.

Haya pia tunayaona kwa taifa la Yuda, lililoonekana lenye watu wachache ambao wanawekana kupigwa mara moja wakasambaratika. Lakini walijua Mungu waliyenaye ni mkuu sana, na walijua maadui zao walishamwasi Mungu wa kweli, na waligeukia miungu mingine. Ambapo walijua ni chukizo kwa Bwana kuabudu mingine, na walijua nguvu ya Mungu ni kubwa kuliko ya miungu yao.

SOMA: Lakini sisi, BWANA ndiye Mungu wetu, wala sisi hatukumwacha; tena tunao makuhani wanaomtumikia BWANA, wana wa Haruni, na Walawi, kwa kazi yao; nao humtolea BWANA kila asubuhi, na kila jioni, sadaka za kuteketezwa na fukizo la manukato; mikate ya wonyesho pia huiweka kwa taratibu yake juu ya meza takatifu, na kinara cha dhahabu chenye taa zake, kuwaka kila jioni; kwa maana sisi twayalinda malinzi ya BWANA, Mungu wetu; bali ninyi mmemwacha. 2 NYA. 13:10‭-‬11 SUV.

Ukiwa unamwabudu Mungu katika roho na kweli, unapata wapi hofu ya wachawi, unapata wapi hofu ya kulogwa, unapata wapi hofu ya kutupiwa nguvu za giza. Wewe ni mali ya Bwana, hakuna chochote kinachoweza kukuzuru kwa namna yeyote ile.

Hajalishi waliokuwa upande wa Yeroboamu walikuwa jeshi la askari 800,000, na Abiya mfalme wa Yuda alikuwa na jeshi la askari 400,000. Lakini Abiya alishinda kwa kuwa Mungu alikuwa upande wao.

Haijalishi adui atakuja kukutishia kwa kuwa unaonekana u dhaifu katika eneo fulani, kama una uhakika una uhusiano mzuri na Mungu wako. Usiwe na wasiwasi wa kushindwa bali uwe na ujasiri wa kumweleza adui yako aache kukusumbua. Maana mkono wa MUNGU u upande wako, haijalishi yeye anakuonaje.

SOMA: Na tazama, Mungu yu pamoja nasi atutangulie, na makuhani wake wenye mapanda, ili wapige sauti ya kugutusha juu yenu. Enyi wana wa Israeli, msipigane na BWANA, Mungu wa baba zenu; kwani hamtafanikiwa. 2 NYA. 13:12 SUV.

Watasema una ringa sana una nini, waambie unaye Yesu Kristo aliye shinda kifo na mauti kwa ajili yake na yako wewe. Mchawi akikugusa atakufa yeye na kukuacha wewe, bora achague moja kuokoka au kukutana na ghadhabu ya Mungu.

Pamoja na mfalme Yeroboamu kuelezwa kwa kina mfalme Abiya, Yeroboamu hakusikia na kuwazunguka Yuda kwa nyuma ili awapinge. Lakini Yuda walimlilia Mkuu wao, Mungu wa miungu, Mfalme wa wafalme, akashuka akawapia jeshi la Yeroboamu yapata watu 500,000.

SOMA: Lakini Yeroboamu aliwazungushia waviziao kwa nyuma; basi wao wakawa mbele ya Yuda, na wale waviziao nyuma yao. Na Yuda walipotazama nyuma, angalia, vita vikawa mbele na nyuma; wakamlilia BWANA, na makuhani wakapiga mapanda. Ndipo wakapiga kelele watu wa Yuda; ikawa, watu na Yuda walipopiga kelele, Mungu akampiga Yeroboamu na Israeli wote mbele ya Abiya na Yuda. Wana wa Israeli wakakimbia mbele ya Yuda; naye Mungu akawaua mikononi mwao. Abiya na watu wake wakawapiga mapigo makuu; hata wakaanguka wameuawa wa Israeli mia tano elfu, watu wateule. Ndivyo walivyotiishwa wana wa Israeli wakati ule, wakashinda wana wa Yuda, kwa kuwa walimtegemea BWANA, Mungu wa baba zao. 2 NYA. 13:13‭-‬18 SUV.

Nimejaribu kukupa maandiko mengi zaidi ili uelewe vizuri nafasi uliyonayo mbele za MUNGU, usiishi ndani ya wokovu kama mtu aliye kifungoni. Mtu aliyefungwa hana uhuru wa kufanya mambo yake, lakini wewe haujafungwa ndugu yangu, unayo mamlaka na kibali mbele za Mungu wako.

Naamini kuna kitu umejifunza katika ujumbe huu, fanyia kazi ile imani iliyojenga ndani yako.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
+255759808081.