Haleluya, ninamshukuru Mungu kwa nafasi hii adimu aliyonipa niweze kukushirikisha yale aliyonijilia kujifunza siku ya leo kupitia Neno lake.

Hebu chukua dakika chache, ukiwa na muda wa kutosha unaweza kutumia dakika 30 au Lisaa limoja. Muda huo utumie kutafakari maisha yako kwa ujumla, fikiri mienendo na mahusiano yako na watu wanaokuzunguka.

Baada ya kukaa chini ukafakari, jiulize ni jinsi gani umeweka akiba yako ndani ya mioyo ya watu, ambao watakuwa na uwezo wa kukumbuka kwa mema uliyowatendea. Hata kama binadamu huwa ni wagumu kumkubali mwenzake, basi matendo yako mema yazungumze.

Utaona upo kiasi gani ndani ya mioyo yao, ni rahisi tu kujua kwa kujipima mwenyewe, kwa kujihoji haya maswali; unatoa nini kwao mpaka wakuone wewe ni mhimu kwao, na umewahi kutenda nini ambayo mioyo ya watu hawatakusahau mpaka unakufa/wanakufa.

Kabla hujafa wewe unaona nini ndani ya moyo wako ukikushuhudia kwa matendo mema kwa wengine? Bila kuingiza unafiki wa aina yeyote, utajua una mapungufu sehemu fulani unapaswa kurekebisha au utajipongeza kwa uliyofanya nyuma yakawa alama nzuri kwa wale uliowatendea.

Labda nikutolee mfano wa mama mmoja, ambaye ni member wa Chapeo Ya wokovu, ambaye anaitwa mama Ukende Shalla. Huyu mama alipatwa na musiba wa kufiwa na mama yake mzazi, ambaye kwangu ni mjukuu wake kabisa kutokana na umri wake. Maana alikuwa na umri wa miaka 100 mpaka kifo kinamkuta.

Wakati tupo kanisani kuaga mwili wa marehemu, muda wa salamu za rambirambi ulipofika, kila kikundi kilichoinuka kutoa salamu za rambirambi. Nilikuwa nasikia mama Ukende Shalla alikuwa mwenzetu, mama Ukende Shalla ameshirikishi nasi mambo mengi, tumeona vyema kufika Kwenye msiba wa mama yake.

Nasi tulipofika zamu yetu kama wana familia ya Chapeo Ya Wokovu, tukasema mama Ukende Shalla ni mama yetu tumekuja kujumuika naye katika majonzi. Bila shaka wale ambao wanamfahamu huyu mama watakubali ninayosema, ni mama mwenye umri mkubwa ila yupo mstari wa mbele na vijana kufanya mambo ya kiMungu.

Unaweza kujiuliza mama Ukende Shalla ndio alikuwa hana ndugu wengine mpaka watu wote wawe wanamtaja yeye tu. Unaweza kuona ni kitu ambacho hakiwezekani kutokuwa na ndugu wengine.

Mama huyu ameanza kuona matunda ya kujitoa kwake hata Kabla hajaondoka duniani, ameanza kuona ule ushirika mzuri na watu wengine. Hata siku amekaa peke yake anaona kweli nilifanya, Kabla ya kuambiwa na mtu mwingine atajisemea yeye moyoni.

Je mimi na wewe tunashiriki vipi matukio ya wenzetu wanapopatwa na shida, je tunashiriki vipi kuwasaidia wahitaji wa pesa, je tunashiriki vipi misiba ya wenzetu kifedha na kujitoa wenyewe pasipo fedha, je tunajitoa vipi kuwasaidia mayatima na wajane.

Tuna kitu gani cha kujivunia sisi wenyewe kabla kaburi halijatumeza, na Kabla watu hawajasoma historia ya marehemu alikuwa anatenda mema. Wewe mwenyewe unajishuhudia vipi moyoni mwako.

Je unaposikia michango ya kanisa kwenda kuhubiri injili huwa unashiriki?
Je unaposikia rafiki yako anahitaji umsaidie fedha, huwa unafanya hivyo hata kama sio mara zote unakuwa na pesa?
Je nafasi yako ya dokta/Nesi, wakristo wenzako na jamii kwa ujumla wanajivunia uwepo wako? Hata watu wakisikia dokta fulani hatunaye…waanze kulia huko makwao kwa vile ulikuwa unatoa huduma njema.

Je nafasi yako kama mwalimu wa shule/chuo wale waliopita mikononi mwako, wanajua mchango wako na bidii yako katika kuweka kitu ndani yao? Au unafanya ilimradi siku za mshahara zifike.

Swali la Kujiuliza; utakumbuka lipi jema ulilolitenda na watu washuhudie kweli ulitenda, na unaweza kukumbukwa kwa lipi ulilolitenda likaa mioyoni mwa watu? Jibu unalo mwenyewe.

Ushauri wangu kwako, shiriki matukio ya wenzako, cheka na wenzako, lia na wenzako, toa muda wako, toa mali zako, toa ujuzi wako, toa ushauri wako. Hakikisha unapokuwa na nafasi ya kufanya jambo fanya, kama huna pesa shiriki kwa njia ya kutoa nguvu zako na muda wako.

Haya yote tunajifunza kwa mtumishi wa Mungu Ayubu, Ayubu alifika kipindi akakumbuka wema aliowahi kuwatendea wengine. Hata kabla hajafa ili watu wasome historia yake, ila yeye alikumbuka wema aliowahi kuutenda wa wengine.

Rejea; Kwa sababu nalimwokoa maskini aliyenililia; Yatima naye, na yule asiyekuwa na mtu wa kumsaidia. Baraka yake yeye aliyekuwa karibu na kupotea ilinijia; Nikaufanya moyo wa mjane kuimba kwa furaha. AYU. 29:12‭-‬13 SUV.

Hebu kaa chini ujitafakari mwenyewe, tutakukumbuka kwa lipi jema ulilowahi kutufanyia wengine. Basi tusipokukumbuka sisi, wewe unakumbuka jema gani ulilowahi kuwatendea wengine? Hata kama umekaa unamkumbusha Mungu, uwe na ujasiri wa kumwambia Mungu nikumbuke kwa hili.

Doricas alipata fursa ya kukufuliwa tena kwa vile vitu alivyokuwa anawatendea wengine. Watu wakaona hapana, Mungu akabidi akubali kumrejesha tena uhai wake. Sasa wewe kipi kitakufanya tusilie tu kwa mazoea, bali tulie kwa sababu tumempoteza mtu muhimu.

Vipi wewe leo ukifukiwa kwenye kaburi ndio habari yako imeishia hapo au watu watazidi kushuhudia habari zako njema. Haya yote yapo mikononi mwako, kuamua kujitoa kuanzia leo kwa wengine, kwa nafasi aliyokupa Mungu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.