
Unajua uhusiano wako na Mungu, ni bora sana, bila kuangalia nani anakuona, yaani ukiondoa mawazo ya kutaka kuonekana kwa watu upo vizuri. Uhusiano wako na Mungu unapaswa kuanzia chumbani mwako, wakati hakuna mtu yeyote anayekuona. Ndio wakati ambao unapaswa kujiangalia upoje na Mungu wako.
Maana kuna watu wana wokovu wa kuonekana kwa watu, lakini ukimfuatilia unamkuta anafanya mambo ya ajabu hujawahi kufikiri kama mtu kama yeye anaweza kufanya hayo. Kutokana na unavyomfahamu kwa nje.
Pamoja na mtu wa namna hiyo kujitahidi kujificha kwenye mwavuli wa wokovu, bado kuna vitu vinaonekana kwa watu kuwa havipo vizuri. Wale wale wanaoshirikiana nao kwa mambo mabaya ndio wanaotoa habari zao au ndio wanaojua kuwa wanadanganya jamii kuwa wameokoka ila sio kweli.
Kuingiza umeokoka vizuri, alafu unajua kabisa njia zako hazipo vizuri, unajua una michanganyo fulani fulani, huko ni kujisumbua bure. Maana Yesu Kristo akiamua kukuumbua utaumbuka vibaya sana mchana kweupe.
Ndicho kilichowakuta watu hawa ambao nyendo zao hazikuwa vizuri, wakaamua kukemea pepo wachafu, hao pepo wachafu waliwaumbua watu wale.
Rejea: Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa. MDO 19:15-16 SUV.
Na nikuambie ukweli hata kama hutokubaliana na mimi, kama haupo vizuri na Mungu na moyoni mwako unashuhudiwa hivyo. Bora kukaa pembeni ukawaachia watu wengine wakakemea pepo.
Pepo litakuebisha ndugu, nakueleza ukweli, kwa sababu hiyo ni roho chafu, ambayo inajua matendo yako machafu. Hata kama kuna watu ulikuwa unawaficha, pepo anajua.
Sikuelezi haya ili kukutisha, nakueleza ukweli ili ujikague upya, tabia zako zinapaswa kuwa nzuri bila kuangalia nani ananitazama. Hatuwi na tabia njema ili watu watuone, elewa hilo, tunakuwa na tabia njema ili kuendelea kuwa na ushirika mzuri na Mungu wetu.
Ukilijua hili, hutotembea na waume za watu kwa sababu unamwogopa mume wako, wala hutotembea na wake za watu kwa sababu unamwogopa mke wako. Wala hutofanya jambo lolote baya kwa sababu ya kumwogopa mtu, utajilinda mwenyewe kwa kulinda uhusiano wako na Mungu.
Ukielewa haya yote, maisha yako ya wokovu yatakuwa salama, maana wokovu wako sio wa kujilinda ili watu wakuone upo vizuri. Utajilinda ili kulinda uhusiano wako na Mungu wako.
Kama bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, hakikisha unajiunga sasa, tuma ujumbe wako wasap namba +255759808081 utapatiwa taratibu za kundi.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com