IFAHAMU CHAPEO YA WOKOVU.
(Chapeotz)
Tunakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai.
Ukisoma bibilia kitabu cha neno la Mungu, Waefeso 6 :17 inasema; “Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu.” Neno hilo la Mungu katika kitabu hicho ndilo lililotufunua na kuanzisha mtandao wa kijamii ambao tumeupa jina la CHAPEO YA WOKOVU. Sababu ya kuanzisha mtandao huu ni kuwafikia watu wengi zaidi kwa urahisi, na kwa muda mfupi, hasa kwa kuzingatia mabadiliko ya ulimwengu wa leo.
Tulisukumwa zaidi kutumia jina hili la chapeo ya wokovu, kwa kuwa limebeba neema ya ulinzi wa roho pamoja na mwili. Kwa kuwa kusoma neno la Mungu ni chanzo cha ufahamu, na maarifa ambayo ndio afya ya akili zetu. Lakini pia kusoma neno la Mungu ni chanzo cha amani ndani ya mioyo yetu, hivyo NENO hutengeneza afya ya mwili na roho, si hayo tuu bali NENO la Mungu ni faraja, ni uzima, ni afya, ni upendo, ni furaha, na amani.
Kwa kuyajua hayo Chapeo Ya Wokovu tuliona ni vyema tukalisambaza neno la Mungu kupitia mtandao, ili watu waijue kweli ya Mungu na njia sahihi ya kumfuata. Kumwabudu na kumtukuza, hivyo mtandao huu utakuwa na vipengele vifuatavyo;
1. Neno la leo
Ni sehemu ambayo itakuwa inabeba ujumbe wa neno la Mungu na mafundisho mbalimbali yanayokujenga kimwili na kiroho.
2. Vuka ujana.
Sehemu hii itakuwa maalum kwa makala mbali mbali zitakazokuwa na mafunzo ya neno la Mungu, kwa ajili ya kuwaonesha vijana njia iliyo njema ya kufuata mapendo ya Mungu. Maana vijana ndio kundi kubwa ambalo shetani hupendelea kulitumia sana.
3. Jinsi ya kukua kiroho.
Patakuwa na mafundisho mbalimbali yatakayokuwa na lengo la kumfanya mwanadamu amjue Mungu, na kumtegemea Mungu katika maisha yake ya wokovu. Kutokana na changamoto/shida mbalimbali ambayo hutukabili wanadamu, inatulazimu kumjua Mungu zaidi.
4. Picha na matukio.
Sehemu hii itakuwa na mjumuiko wa picha, na matukio mbalimbali yatakayokuwa na uhusiano na mambo yote ya dini.
5. Video za injili.
Hapa patakuwa na nyimbo mbalimbali za injili ambapo zitakuwa na lengo la kufikisha ujumbe wa neno la Mungu ulimwenguni kote, kwa njia ya uimbaji.
Dhumuni na malengo ya mtandao huu ni kufikisha kwa urahisi zaidi neno la Mungu ulimwenguni kote. kwa kuwa mtandao huu unaweza kumfikia mtu popote pale alipo bila ya kuathiri ubebaji wa vitu vingine. Kwani unaweza ukaupata kwa kutumia simu/tablet au Compyuta yako. Ambayo huitumia katika shughuli zako nyingine za kila siku, hivyo kusoma neno la Mungu kupitia Chapeo Ya Wokovu, hakukuhitaji ubebe kifaa chochote cha ziada.
Mwisho tunapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa neema na ufahamu wa kulianzisha jambo hili. Pia tunamshukuru mbeba maono wa huduma hii SAMSON ERNEST ambaye amehakikisha NENO la MUNGU linawafikia wengi zaidi. Pia tunawashukuru watu wote ambao kwa namna moja ama nyingine walishiriki katika ufanikishaji wa jambo hili KIFEDHA NA KIMAOMBI.
Pongezi za kipekee kwa wanachapeo wote ambao tumekuwa nao pamoja tangu uanzishwaji wa mtandao huu mwaka 2014 mpaka leo. Uwepo wao na bidii yao katika kumtafuta Mungu imefanya kupanuka zaidi kwa huduma hii.
MUNGU AWABARIKI SANA.