“Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari”, Yn 16:14 SUV.

Roho Mtakatifu huchukua kile kilicho cha Kristo na kukifunua kwa muamini, kile ambacho kingemletea ugumu kukifahamu yeye anamsaidia kukielewa vyema kama kilivyokusudiwa.

Wengi hufikiri ujuzi na ufunuo wa jambo wanapopata watu ni kwa sababu wao wana bahati sana au wana upendeleo fulani, Mungu humgawia kila mmoja sawa sawa na mapenzi yake.

Tunapokuwa na uhusiano mwema na Yesu kuna vitu vinaachiliwa kwetu, mojawapo ni Roho Mtakatifu kutusaidia kuelewa yale tunayopaswa kufahamu.

Roho Mtakatifu huutwaa uwepo, upendo, msamaha, ukombozi, utakaso, nguvu, karama za rohoni, uponyaji na yote yaliyo yetu kwa kutumia uhusiano wetu mzuri wa imani na Kristo, na kuvifanya vifanyike kweli katika maisha yetu.

Kupitia Roho Mtakatifu, Yesu anaturudia sisi akifunua upendo, neema, na ushirika wake binafsi kwetu sisi (Yn 14:16-23).

Yapo mambo Mungu ametuahidia, tunahitaji msaada wa Roho ili yaweze kutimilika kweli kwetu, bila hivyo utakuta kuna vitu havipo kwa mtu.

Jambo lingine kufahamu, Roho Mtakatifu hutenda kazi ndani yetu ili kufanya kilicho muhimu kwetu, hutuamsha na kukuza ufahamu wetu zaidi wa kutambua uwepo wa Yesu katika maisha yetu.

Tunavyozidi kujifunza kuhusu Mungu kupitia neno lake na kuona tunaongezeka kiroho, tujue kazi hiyo hufanywa na Roho Mtakatifu, humfunua Mungu kwetu na kumwona kwa namna ambayo ni tofauti kabisa na ulimwengu unavyomwona.

Roho huivuta zaidi mioyo yetu imwelekee Yesu katika imani, upendo, utii, ushirika, kuabudu, na sifa. Ndipo uhusiano wetu na Yesu unapozidi kuimarika na kukua zaidi na zaidi kiimani kila siku,

Tamani uwepo wa Roho Mtakatifu katika maisha yako, mtunze kwa maisha matakatifu mbele za Bwana, usiishi mtupu ukiwa umemwacha Yesu, utakosa mambo muhimu katika maisha yako.

Soma neno ukue kiroho
Kwetu kusoma biblia ni maisha
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081