“Naye, alipokwisha kufika na kuiona neema ya Mungu akafurahi, akawasihi wote waambatane na Bwana kwa kusudi la moyo,” Mdo 11:23 SUV.

Tunasoma na kuona mitume wa agano jipya hawakuwaacha wale waongofu wapya waliompa Yesu maisha yao, walijua wasingeendelea kudumu katika imani hiyo bila kujengwa kiimani.

Walijua majaribu yasingewaacha, Shetani angeendelea kuwafuatilia nyuma kuhakikisha anawarudisha tena dhambini na kuacha wokovu wao.

Barnaba anatuonyesha wazi vile tunapaswa kuwatendea waamini wapya, tunapaswa kuwafundisha na kuwajenga vizuri katika msingi wa imani sahihi.

Tunapaswa kuendelea kuwaonyesha upendo na kuwatia moyo katika maisha yao mapya ya wokovu, huku tukiendelea kuwaombea wadumu katika imani yao mpya.

“Sinagogi ilipofumukana, Wayahudi na waongofu watauwa wengi wakashikamana na Paulo na Barnaba; ambao, wakisema nao, wakawatia moyo kudumu katika neema ya Mungu”, Mdo 13:43 SUV.

Tunapaswa kuwa makini sana, mtu anapookoka huwa anakutana na maneno mengi ya kumvunja moyo, wengine hutengwa na ndugu zao, na wengine fukuzwa nyumbani kwa sababu ya imani.

Kuwajenga katika imani yao mpya ni jambo la msingi kwao, inawapa uwezo wa kuweza kujisimamia vyema, wakishakuwa imara wanaweza kusimama kwa miguu yao wenyewe.

Hakikisha unakumbuka hili, kama wewe huwezi kuwafundisha au kumfundisha mwongofu mpya, hakikisha unamkabidhi mahali ambapo apata mafundisho ya awali ya kuukulia wokovu.

Usifurahie idadi kubwa ya watu kuokoka alafu hujawatengenezea utaratibu mzuri wa kufundishwa mafundisho ya awali ya kuwajenga kiroho.

Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081