Mtu anaweza akawa na kiburi cha kazi yake nzuri, kwa vile uhakika wa usalama wa kazi yake upo wa kutosha. Pia mtu anaweza akawa na kiburi cha afya yake nzuri, hakuna magonjwa yanayomsumbua. Wala upande wa kula chakula kizuri hakuna kinachomsumbua.

Mwingine anakuwa na kiburi cha utajiri wa familia yake yenye uwezo mkubwa, ukimgusa anakwambia unanifahamu mimi ni mtoto wa nani? Acha kunichezea nitakufunga uozeee jela.

Mwingine anaweza akawa na kiburi, kwa sababu anasoma shule nzuri ya kiwango, akawa kikwazo kwa yule ambaye anasoma shule ya kawaida. Na kuona mwenzake si kitu wala si chochote kwake.

Mwingine anaweza akawa na kiburi kwa sababu babu/bibi yake ni mshirikina(mchawi) anageuka kero na usumbufu kwa wenzake, kwa sababu ya uchawi babu/bibi yake. Hasa kwa watu wasio na imani thabiti kwa YESU Kristo, atawasumbua na wengine kuharibiwa kweli maisha yao.

Tumeona maeneo mbalimbali yanayoleta au yanayoweza kusababisha kiburi kwa mtu. Yapo maeneo mengi ila nimekushirikisha machache ili kuweza kupata mwanga kuhusu kiburi.

Haijalishi kiburi kitakuwa kwenye eneo gani, kinaweza kikawa kwenye huduma yako ama kinaweza kikawa kwenye kazi/biashara zako.

Unachopaswa kufahamu kiburi hakijawahi kumwacha mtu salama, kiburi ni sumu mbaya sana katika eneo lako lolote lile katika maisha yako.

Kiburi kinaweza kukushusha kwa haraka sana kwenye eneo ulilofanikiwa, iwe eneo la kiroho au kimwili. Ikiwa utajawa na kiburi, lazima uanguke katika eneo hilo lililokufanya uwe na kiburi.

Tunaweza kuliona hili jambo kwa mapana zaidi kupitia Neno la Mungu, unaweza kuona ni jinsi gani kiburi kimeweza kumwangusha yeyote yule aliyekuwa nacho.

Rejea: Tazama, mimi ni juu yako, Ewe mwenye kiburi, asema Bwana, BWANA wa majeshi; maana siku yako imewadia, wakati nitakapokujilia. Na mwenye kiburi atajikwaa, na kuanguka, wala hapana atakayemwinua; nami nitawasha moto katika miji yake, nao utawala wote wamzungukao pande zote. YER. 50:31‭-‬32 SUV.

Umeona hapo, Mungu anasema hivi; Na mwenye kiburi atajikwaa, na kuanguka, wala hapana atakayemwinua. Ukishaanguka na kiburi chako hakuna mtu yeyote ambaye atakuinua, labda ugundue mwenyewe na kumrudia Mungu wako kwa toba ya kweli.

Kiburi ni kibaya sana, na kiburi hichi humkuta mtu pale atakapokuwa amefanikiwa katika jambo/kitu fulani katika maisha yake. Muhimu sana kujilinda na kiburi usije ukaingia katika anguko ambalo hakuna atakayekuinua.

Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.