Kadri unavyozidi kumjua Mungu kupitia kujifunza Neno lake na mafundisho mbalimbali ya Neno la Mungu, kiwango chako cha kufikiri juu ya Mungu, vile unatazama mambo. Ni tofauti kabisa na mtu ambaye hajaokoka, ni tofauti kabisa na mtu ambaye hajishughulishi na kujifunza Neno la Mungu.

Utofauti huu unakuja pale unapokuwa na Neno moyoni mwako, pale watu wanasema haiwezekani, kutokana na Neno lililo moyoni mwako utakuwa unaona hilo jambo linawezekana. Hata kama madaktari watathibisha tatizo ulilonalo haliwezekani kabisa kupona kwa dawa yeyote ile, bado hilo haliwezi kuleta mashaka kwa mtoto wa Mungu.

Unapojikuta upo kwenye kundi la wanaomwamini sana Mungu kwenye maisha yao, muda mwingine unaweza kuonekana kama mtu uliyechanganyikiwa. Maana wakati wenzako wanasema ugonjwa huu ndio basi tena umeshindikana kupona, wewe utakuwa unaona unawezekana kupona.

Wakati vipimo vyote vinaonyesha wewe ni mgumba, yaani haiwezekani kabisa mimba ikatungwa kwenye tumbo lako. Kwa mtoto wa Mungu mwenye Neno la Mungu la kutosha moyoni mwake, hana mashaka juu ya taarifa aliyopewa.

Mtu yeyote anapokuwa anaona matatizo yake kwa mtazamo wa kushinda, wengi hugeuka kicheko kwa wale wanaotazama mambo kibinadamu. Wale wanaotazama mambo kibinadamu, wana tofauti kubwa sana na wale wanaotazama mambo kiMungu.

Ukikaa na watu wanaotazama mambo kibinadamu, ukiwaeleza vile unaona wewe moyoni mwako, vile una imani kubwa mbele za Mungu, kuwa inawezekana. Mnaweza kupishana mbali sana, na unaweza kuambulia maneno ya kejeli mengi sana.

Pamoja na kuchekwa na watu wasiojua tunaona nini mioyoni mwetu, hawawezi kubadilisha ukweli tunaouona. Kama kwa mwanadamu imeshindikana, kwa Yesu Kristo inawezekana kabisa.

Hili jambo alikumbana nalo Yesu Kristo kwenye huduma yake, walivyowaambia mtoto hajafa bali amelala, walimcheka sana. Unaposikia mtu amechekwa sana, tena mbele ya kusanyiko kubwa la msiba ghafla likageuza kulia kwao hadi kuanza kumcheka mtu, utakuwa unaelewa vizuri vile huyo mtu amechekwaje.

Rejea: Na watu wote walikuwa wakilia na kumwombolezea; akasema, Msilie, hakufa huyu, bali amelala usingizi tu. Wakamcheka sana, maana walijua ya kuwa amekwisha kufa. LK. 8:52‭-‬53 SUV.

Hii ipo katika maisha yetu ya kila siku, kuna kitu unakiona kabisa ndani ya moyo wako kuwa kinawezekana, ukijaribu kumshirikisha rafiki yako au ndugu yako au mzazi wako. Unaweza kuishia kukatishwa tamaa, unaweza kuishia kuchekwa na kuambiwa wa kuweza ni wewe!

Ukishakutana na hali kama hii, usianze kushindana nao, nyamaza kimya, acha vitendo vizungumze vyenyewe. Yesu Kristo hakushindana nao, alivyowaambia mtoto hajafa bali amelala tu, wao wakaibua vicheko, vicheko vyao havikuibadilisha maneno ya Yesu Kristo.

Rejea: Akamshika mkono, akapaza sauti, akisema Kijana, inuka. Roho yake ikamrejea, naye mara hiyo akasimama. Akaamuru apewe chakula. LK. 8:54‭-‬55 SUV.

Sijui ulikuwa na maono gani makubwa, ulivyowashirikisha watu walikuambia haiwezekani kabisa. Kama ulikubaliana nao, utakuwa hukujua Neno la Mungu linasemaje, kama ulikuwa na Neno la Mungu, ungeitii ile sauti ya Roho Mtakatifu wakati inakusisitiza inawezekana.

Kucheka watu kwa sababu umewaambia unataka kuwa Daktari bingwa, na wewe ulipo hapo umeishia tu darasa la saba. Hawawezi kuubadili ukweli hata kama watakucheka sana, endelea kujibidiisha kufikia ndoto yako.

Kuchekwa isiwe sababu ya wewe kuacha kutenda kile ulikikusudia, kama Yesu angejisikia vibaya baada ya kuchekwa, yule mtoto asingemfufua. Alimfufua yule mtoto kwa sababu hakuyumbishwa na vicheko vya watu.

Unajua mwenyewe umechekwa katika eneo gani la maisha, ila hakikisha unaendelea kusonga mbele. Wanaokucheka hawajui kabisa mapatano yako na Mungu, wanaokucheka wanakujua mtoto wa fulani, ama wanakujua kama mama fulani, ama wanakujua kama mwalimu fulani, ama wanakujua kama muuza mbogamboga. Mbele ya ufalme wa Mungu haupo kama wanavyokutazama wanadamu, wewe ni mwingine kabisa.

Karibu darasa la kujifunza Neno la Mungu kila siku kwa njia ya whatsApp group, ukiwa ndani ya group la CHAPEO YA WOKOVU, utajengewa tabia ya kusoma Neno la Mungu kila siku. Ili uunganishwe kwenye group, tuma ujumbe wako kwenda +255759808081 (tumia wasap tu)

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com
+255759808081