“Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu”, Yn 21:17 SUV.

Moja ya swali muhimu alilokutana nalo Petro ni hili, Yesu anamuuliza kama anao upendo wa kweli wa kujitoa kwa Bwana wake, alijibu kwa ujasiri anao huo upendo.

Swali hili aliliuza Yesu mara tatu, na tunaona mara zote Petro alimjibu Yesu kuwa anampenda, hii inaonyesha msisitizo wa jambo hili na Yesu alimtaka Petro athibitishe kwa kinywa chake.

Mara nyingi maswali kama haya tunaweza kukutana nayo hata kwa watoto wetu, mtoto anaweza kukuliza hili swali na ukabaki na maswali mengi, unachotakiwa ni kumjibu kuwa unampenda.

Mke/mume anaweza kukuuliza hili swali, je unanipenda kweli? Unaweza kushangaa huyu mwanamke au mwanaume nimekaa naye miaka yote kwanini anauliza swali la namna hii? Unaweza kumuuliza na yeye kwa mshangao ila ujue anachotaka ni uthibitisho wa upendo wako kwake.

Mtu anapotaka kukuachia wajibu kwa familia yake lazima athibitishe hili la upendo, mtu hawezi kukuachia maagizo ya kumtunzia watoto wake kama hakuamini, hamna uhusiano mzuri, na hamna upendo wa kweli kati yenu.

Mara nyingi anayekuuliza unanipenda huwa anataka kusikia tu sauti yako ila anakuwa ameshaona vishiria vingi vya upendo kwako, binadamu tunapenda kusikia tu mtu mwenyewe akithibitisha lile tunaliona kwake.

Nguvu ya upendo

Yesu aliona upendo ndio sifa pekee na ya msingi kwa ajili ya utumishi wa Kikristo, japo zipo zingine ila hii inapaswa kuanza kwa mtu ndipo ataweza kutumika vyema kwenye eneo aliloitiwa.

Sifa nyingine kwa mtumishi zinapatikana katika kitabu cha “1 Tim 3:1-13” hapa zimeelezwa sifa zingine za muhimu, lakini upendo kwa ajili ya Kristo na kwa ajili ya watu wengine ni wa lazima kwa mwamini.

“Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu”, 1 Kor 13:1‭-‬3 SUV.

Huduma ikitangulia alafu upendo ukawa nyuma, uwe na uhakika huduma hiyo itakuwa ina shida kubwa, maana kinachotufanya tumtumikie Mungu pasipo kuyumbishwa na jambo lolote ni ule upendo kwa Kristo ulio ndani yetu.

Kinachotufanya tusipende mapato ya kizalimu au tusipende fedha ni ule upendo wa Kristo ndani yetu, ndio sababu Yesu kumuuliza Petro swali hilo hilo mara tatu alijua anao wajibu mkubwa katika ufalme wake hapa duniani.

Kabla hujatamani kazi ya uchungaji, uinjilisti, utume, uaskofu, uimbaji, uzee, hakikisha upendo wa Kristo umo ndani yako kwanza, ule upendo wa kweli usio vuguvugu au baridi.

Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081