Dhambi inamfanya mtu aonekane katika ulimwengu wa kiroho kuwa amekufa, anaweza akawa mzima kabisa kimwili lakini anakuwa amekufa.
Wote tunajua ukishakufa huwezi kusikia watu, huwezi kuona, huwezi kutembea, unakuwa upo tu ndani ya kaburi hilo.
Kadri unavyozidi kukaa kwenye kaburi la dhambi, ndivyo unavyozidi kubaki mifupa mitupu. Mifupa ambayo inakuwa vigumu kumtambua mhusika ni nani.
Unapomwacha Yesu Kristo, na kukimbilia maisha ya dhambi, moja kwa moja unakuwa unajulikana mtu aliyekufa. Katika ulimwengu wa roho ni halisi kabisa isipokuwa Katika ulimwengu wa mwili unaweza usielewe vizuri.
Kwahiyo unapomwona mtoto wako, baba yako, mama yako, mume wako, mke wako, rafiki yako, au ndugu yako yeyote yule. Ameingia kwenye vitendo viovu, ujue huyo ameshakufa tayari.
Kama Mungu alikuwa anamsemesha, Mungu ataacha kusema naye, maana uhusiano naye haupo tena. Hadi pale uhusiano wake na Mungu utakapomrudia tena kwa kutubu.
Dhambi ni gereza kubwa sana ambalo linawameza wengi, na wakishamezwa na dhambi. Huyo mtu anakuwa mgumu kukuelewa hadi pale Neema ya Mungu itakavyomrudia tena.
Hili tunajifunza kutoka kwa mwana mpotevu, alivyopewa urithi na baba yake. Alianza kufanya mambo mabaya yasiyofaa, mpaka pale alipoishiwa na kuanza kuishi maisha ya mtu ambaye ni maskini kabisa.
Rejea: Kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia. LK. 15:24 SUV.
Kumbe unaweza ukawa umekufa huku unatembea? Kama ni hivyo hakikisha unajiimarisha uhusiano wako na Mungu wako.
Usikubali kuchotwa na dhambi za Dunia hii, utakuwa ni mtu wa kudharauliwa sana kama mwana mpotevu, kijana asiye na mwelekeo wowote mzuri wa maisha yake.
Huwezi kusema nina maono makubwa wakati umemezwa na maisha ya dhambi, aliyemezwa na dhambi anakuwa amekufa. Sasa ukiwa umekufa kiroho unawezaje kuyatimiza maono makubwa uliyonayo? Inakuwa ngumu.
Rudi kwa Yesu Kristo, tengeneza na Bwana, maisha yako yatakuwa salama. Kitendo cha kutubu mbele za Mungu, ni kuleta uhai tena wa kiroho ndani yako.
Mungu akubariki sana.
Rafiki yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com