Kawaida yetu wanadamu tunapenda injili laini isiyokuwa na maneno makali, na tunapoona mtumishi wa Mungu anahubiri injili iliyojaa ukweli na yenye kuchoma mioyo yetu.

Mara nyingi mtumishi huyo hugeuka adui yetu, bila kujua ukali maneno anayotoa, anaongozwa na Roho wa Mungu ndani yake.

Wakati mwingine unaona kama vile maneno yanakuwa na ukali kiasi kwamba yanakuingia ndani, usipokaa sawa unaweza kufikiri anakusema wewe kwa visa vyake binafsi.

Unapaswa kuelewa kwamba, watumishi wa Mungu wamefanywa vinywa vyao kama upanga mkali. Na Mungu amewasitiri kwa kivuli chake.

Kwa kuwa hujui, unaweza kuanza kushindana na mtumishi wa Mungu kuwa anakusema vibaya. Umeshindwa kuelewa huyo ni mwakilishi wa Mungu, anasema badala ya Mungu.

Ndio inawezekana kabisa kupitia uovu wako, akapata ujumbe, tena ujumbe ambao utakuwa umepimwa na maandiko matakatifu.

Sasa unapofanya dhambi alafu Mungu akamtumia mtumishi wake kukuonya, badala ya kubadilika tabia yako mbaya. Wewe unaanza kushindana naye, kwa namna unazoona wewe, utakuwa unajisumbua bure.

Ulinzi aliowekewa na Mungu ni mkubwa mno, labda ukute hajui maandiko matakatifu, ila mtumishi anayejua kile anasukumwa ndani yake anapaswa kufanya, hawezi kutishwa na lolote.

Hebu tuone Neno la Mungu linasemaje kuhusu hili ninalokueleza hapa, huenda unasoma hapa lakini moyoni mwako unasema hakuna kitu kama hichi.

Rejea: Naye anifanya kinywa changu kuwa kama upanga mkali; katika kivuli cha mkono wake amenisitiri; naye amenifanya kuwa mshale uliosuguliwa; katika podo lake amenificha. ISA. 49:2 SUV.

Tena kuna jambo lingine hapo limeongezewa, Mungu anamfanya mtumishi wake kuwa mshale uliosuguliwa. Moja ya silaha za asili zinazoogopwa sana ni mshale, mshale ni silaha moja ikikupata sehemu ya mwili wako unaweza usipone.

Tena sio kumfanya mtumishi wake kuwa mshale tu, anamficha katika podo lake. Unaona kiasi gani kuwa mikononi mwa Mungu kuna usalama mkubwa sana.

Usitishwe na mtu yeyote kwenye utumishi wako, Mungu amekuteua wewe kuwa chombo chake.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081