Tabia ya mtu kuijua haraka inaweza isiwe rahisi sana, hasa akiwa kwenye hali fulani hivi ya chini. Ili uanze kuijua tabia yake vizuri, ni pale anapoanza kufanikiwa kwa kile alichokuwa anakifanya.
Leo unamwona mwimbaji wa nyimbo za injili ni mnyenyekevu na msikivu, ni kwa sababu bado hajajulikana na watu wengi, na bado hajapata mafunikio makubwa kupitia uimbaji wake.
Leo unamwona mtu kazini ni mtu wa watu mkiwa cheo kimoja, ngoja anapandishwe daraja awe juu yenu. Hapo ndipo utajua tabia yake vizuri, utafika mahali utaanza kujiuliza huyu ndiye fulani au amegeuka mtu mwingine.
Watu wengi sana wakishafanikiwa huwa wanabadilika sana, wachache sana huwa wanaendelea kuwa na tabia zao za awali kabla hawajafanikiwa. Wengi wakishafanikiwa anabadilika kabisa na kuwa sio yule mnyenyekevu aliyekuwa anajali kila mtu.
Ukimkuta mtu aliyefanikiwa anaonyesha unyenyekevu, uwe makini sana, ukifuatilia vizuri utajua unyenyekevu wake ni kwa ajili ya manufaa fulani. Lakini yeye kama yeye huo unyenyekevu unakuwa haupo kabisa ndani yake, kwa sababu ya mafanikio yake.
Ukimkuta mtu aliyefanikiwa na hajabadilika tabia yake nzuri aliyokuwa nayo kabla ya kupata mafanikio makubwa. Ujue huyo mtu ana Mungu wa kweli ndani yake, ujue huyo mtu ni wa ibada sana, ujue huyo mtu Neno la Mungu limejaa kwa wingi ndani yake.
Wengi sio wanakuwa tu wanaondoka katika hali zao za awali, huwa wanafika mahali wanaanza kujiita Mungu. Vile alivyo na mafanikio yake ya kimwili/kiroho anajiona tayari anastahili kuitwa Mungu.
Hakuna kitu kibaya kinamchukiza Mungu kama mtu kufika mahali ajifananishe naye, hicho kitendo huwa kinamchukiza mno Mungu. Lakini kwa kiburi cha mwanadamu, huwa anafika wakati anaanza kujiona yeye ana uwe kama Mungu.
Hili tunaliona kwa mkuu mmoja wa Tiro, alifika mahali akajiona yeye ni Mungu. Hicho kitendo cha kujiona yeye ni Mungu, Mungu aliondoa ulinzi wake kwa mfalme Tiro, na kuachilia hasira yake juu yake. Hii ni kwa sababu ya kukosa heshima mbele za Mungu, hadi kujiita Mungu.
Rejea: Mwanadamu, mwambie mkuu wa Tiro, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa moyo wako umeinuka, nawe umesema, Mimi ni Mungu, nami nimeketi katika kiti cha Mungu, kati ya bahari; lakini u mwanadamu wala si Mungu, ujapokuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu. EZE. 28:2 SUV.
Kilichomfanya mfalme wa Tiro ajione yeye ni Mungu, ni ule utajiri wake mwingi aliokuwa nao, na hekima zake nyingi alizokuwa nazo. Ndio zilimfanya moyo wake uinuke na kujiona yeye ni Mungu mwenyewe.
Unaweza kuona mafanikio ya mtu yanaweza kukutambulisha tabia ya mtu ilivyo, unaweza kumwona mtu ni mkarimu sana. Kumbe ni unyonge tu wa umaskini wake, siku akitoka kwenye hiyo hali ya umaskini ndio utajua tabia halisi ya huyo mtu.
Mungu aliona mfalme Tiro alipofikia ni mbali sana, mwanadamu aliyeumbwa na yeye kujiita Mungu, mwanadamu anayetumia pumzi yake aliyompa kujiita yeye ni Mungu. Mwanadamu asiyejua kesho yake itakuwaje anajiita Mungu, hayo yalimfanya Mungu achukie sana.
Rejea: kwa hekima yako nyingi, na kwa biashara yako, umeongeza utajiri wako, na moyo wako umeinuka kwa sababu ya utajiri wako; basi, kwa hiyo, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu; basi, tazama, nitaleta wageni juu yako, watu wa mataifa wenye kutisha; nao watafuta panga zao juu ya uzuri wa hekima yako, nao watautia uchafu mwangaza wako. Watakushusha hata shimoni; nawe utakufa kifo chao waliouawa kati ya bahari. EZE. 28:5-8 SUV.
Hupaswi kutumiwa watumishi wa Mungu kuja kukuonya kuhusu tabia yako mbaya, unapaswa kujichunga mwenyewe usiwe na moyo wa kiburi. Moyo utakao kusababishia ufike mahali ujione wewe ni Yesu/Mungu.
Neno la Mungu ndio mtumishi wako wa kwanza, limekuonyesha ni jinsi gani hupaswi kujiinua ovyo. Usikubali shetani akushike ufahamu wako haraka, ukafika mahali ukaanza kujiita Mungu.
Mungu akubariki sana.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.