Sio wote huwa tunakubali tulikosea/tumekosea, wengi wetu tunapoletewa taarifa za kukosea na kutakiwa kumrudia Mungu. Huwa hatupo tayari kukubali na kuanguka mbele za Mungu kwa toba.

Kupona kwa mtu yeyote yule na hukumu ya Mungu iliyopagwa juu yake, mtu huyo anapaswa kuchukua hatua mapema pale anapoambiwa usipoacha hii dhambi ipo hukumu juu yako.

Sasa wengi anapoambiwa acha dhambi, usipoacha utaenda jehanamu. Mtu huyo anaona kama vile umekosa kazi ya kufanya.

Muda anaoupoteza kwenye kufikiri umekosa kazi ya kufanya, ule muda wa hukumu uliopangwa na Mungu juu yake. Muda huo unazidi kukaribia, wakati angechukua hatua mapema kwenda mbele za Mungu angepona.

Si umewahi kuona mtu anafia dhambini kabisa, sio kana kwamba huyu mtu hakusikia habari njema za Yesu Kristo aliye hai. Amesikia vizuri sana ila alifanya shingo ngumu, aliona bado anao muda wa kutosha kuishi hapa duniani.

Hili tunajifunza kwa mji wa Ninawi, Yona baada ya kutii agizo la Mungu kupeleka ujumbe wake juu ya watu wa Ninawi. Yona aliposema na watu wa Ninawi, watu hawa walimsadiki/walimwamini Yona maneno aliyowaeleza.

Hawakuishia kumwamini tu, walichukua hatua ya pili kwenda mbele za Mungu kwa kufunga na kuomba. Tena mifungo yao yote nayo ilifungishwa bila kula chochote, ilikuwa ni toba ya kiwango cha juu sana.

Tena haikuwa kiwango cha juu tu, walikuwa wanamaanisha kweli kweli. Kumbuka ni watu waliokuwa wakimtenda Mungu dhambi ila baada ya kuwaambia siku 40 zikifika, Mungu ataungamiza mji wa Ninawi. Watu wale walichukua hatua.

Rejea: Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa. Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo. YON. 3:4‭-‬5 SUV.

Neno la Mungu linasema, wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo. Sijui unapata picha gani katika hili, binafsi naona watu hawa wamekuwa na moyo wa kuanguka mbele za Mungu kwa kumaanisha kweli kweli.

Tena wanasema hivi; Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe? YON. 3:9 SUV.

Watu hawa walipata imani fulani mbele za Mungu, maana walijua wamekosea sana mbele za Mungu. Imani yao ikawa inawapeleka kwamba Mungu anaweza kubadilisha mpango wake wa kuwaangamiza, wakimwendea kwa maombi ya toba ya kweli.

Na tunaona baada ya maombi yale, Mungu aliwasemehe watu wote wa Ninawi. Hili ni fundisho kubwa sana kwetu, tukiwa kwenye safari ya kwenda mbinguni.

Rejea: Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende. YON. 3:10 SUV.

Ndugu yangu, unapogundua umemkosea Mungu, na unapojiwa na mtumishi wa Mungu kukuonya kuhusu hilo. Usiwe mtu mwenye shingo ngumu, nenda mbele za Mungu haraka sana kuomba toba ya kweli na uamue kubadilika kweli.

Matendo yako yaonyeshe wazi kuwa wewe si mwana wa ibilisi tena, ni mwana wa Mungu aliye hai. Kama Mungu alipanga pigo kwako, hilo pigo ataliondoa kwako, yeye ni mwingi wa Rehema.

Shida yetu kubwa huwa tunakuwa wagumu kukubali makosa yetu, kumbe kadri unavyozidi kubishana na sauti ya Mungu kupitia mtumishi wake. Zile siku zilizoamriwa kwako kwa maangamizo, zitafika na wewe ukiwa kwenye hali ya kupuuza.

Usiwe mgumu, unapoambiwa acha dhambi mgeukie Mungu wako, acha maswali mengi, acha kuona watu wanakufuatilia maisha yako. Sio wanakufuatilia maisha yako, bali wanatii agizo la Mungu juu yako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.