Mahusiano yangu ya kwanza wakati nimepanga huyu ndiye atakuwa mke wangu, ilivyofika mahali yakaharibika, licha ya kuwa ilikuwa ni mpango wa Mungu mahusiano yale yavunjike.

Ilinipa shida sana kuanza tena uhusiano mpya(uchumba) ilinipa shida pia kumpata yule ambaye Mungu mwenyewe alimtaka awe mke wangu. Kipindi chote hicho nilipata mhangaiko mkubwa sana ndani yangu.

Wakati mwingine nilikuwa naona kama mambo ya mahusiano yanakuwa magumu sana, kila nikijaribu kuangaza huku na kule naona giza tupu.

Pamoja na kuokoka kwangu, nilifika wakati imani yangu ikashuka chini sana, badala ya kumsikiliza Mungu, nikawa natumia akili zangu kuangaza macho huku na kule.

Basi bwana, macho yakatua sehemu fulani hivi kwa binti mmoja(jina namhifadhi) cha kushangaza moyoni nikawa sipati amani kabisa. Nikajilazimisha ila nikajionya kwamba sitamwambia chochote mpaka nijiridhishe vitu fulani. Nampenda sana Yesu, nitakwambia kwanini nampenda Yesu.

Wakati naendelea kumfuatilia huyu dada nilipata habari zake, sikuamini sana zile habari kutokana na vile alikuwa anajituma sana kwa mambo ya Mungu. Kwenye maombi ya kufunga siku tatu kavu bila kula, alikuwa mshiriki mzuri sana na huduma zingine.

Nampenda Yesu kwa sababu, ukiwa mwaminifu kwake, hata kama utakosea kuchagua, yeye ataingilia kati kwa kukuonyesha wazi matendo ya yule mtu. Labda wewe uwe mkaidi/king’ang’anizi. Basi bwana, baada ya siku kadhaa, nilisikia mengine ya kunishtua zaidi kuhusu yule dada.

Baada ya Yesu kunitoa kwenye muhangaiko ule wa moyo, niliona ni busara kutulia kwanza mpaka nitakapopata utulivu moyoni. Kuliko kuendelea kujingaisha mwisho wa siku nije ningie tena kwenye mahusiano yasiyo sahihi.

Nimekupa huu ushuhuda ili uelewe kwamba, haya mambo yanawapata wengi na yanawaumiza sana kabla ya kumpata yule aliyekusudiwa na Mungu. Hii nafikiri inatokana na kutokuwa na elimu sahihi ya kiMungu kwa vijana walio wengi.

Unapojikuta umepita kwenye changamoto kadhaa za mahusiano ya uchumba/urafiki wa kuelekea kwenye ndoa. Usije ukajiloga, ukajiingiza ilimradi mahusiano, yaani usije ukajitupia kwa mwanaume/mwanamke yeyote atakayekuja mbele yako.

Kuchelewa kwako kuoa/kuolewa, isije ikakufanya ukajidumbukiza kwa ilimradi mwanaume/mwanamke. Hakikisha ndani ya moyo wako, Roho Mtakatifu amethibitisha ndiye wa kwako, na hili utalijua kwa kupata amani ya Kristo moyoni mwako. Nimesema amani ya Kristo, na sio amani ya magari yake, ya kazi yake, ya elimu yake na ya biashara zake.

Unachopaswa kufahamu/kujua ni kwamba mume/mke wako yupo, utasema mbona mimi simwoni siku zote hizo. Tulia mbele za Mungu utamwona, anaweza asiwe kanisani kwako, anaweza akawa kanisani kwako, anaweza asiwe mkoa wako, na anaweza akawa mkoa wako.

Anaweza akawa kabila lako, anaweza asiwe kabila lako, cha kuzingatia wewe atakuwa wa imani yako, na wa kufanana na wewe. Utakayempenda kweli kweli, na atakayekupenda kweli kweli.

Atakayeweza kubeba kusudi la Mungu aliloweka ndani yako, na utakayeweza kubeba kusudi lake aliloweka Mungu ndani yake.

Nakukumbusha tena, huenda hapo umekata tamaa kuhusu kuoa/kuolewa, na umefika mahali umesema atakayekuja yeyote sahihi hivi mbele yangu ni halali yangu. Usije kufanya hivyo, wa kwako yupo, tulia mbele za Mungu, huku ukiendelea kumjua yeye kupitia Neno lake. Atakupa wa kwako.

Tumekubaliana mume/mke wako yupo, usije ukajitupia kwa mwanamke/mwanaume yeyote ambaye moyoni mwako hujampenda/hukumpenda. Ukifanya hivyo utakuwa umejiingiza kwenye majuto ambayo hayakuwa lazima wewe kuingia humo.

Mtumaini Bwana siku zote.
Samson Ernest.
+255759808081