Haleluya,

Hakuna mtu anayependa kuonekana akiwa katika hali fulani ya umasikini au kuchoka sana. Wengi wetu tunapenda kuonekana wa daraja fulani hivi la maisha ya kifahari.

Unakuta mtu hana kitu, ila maisha anayoishi ni mfano wa maigizo. Anataka kuonekana kwa watu yeye ni mambo safi, ila ukipata bahati kufika mahali anapoishi unaweza ukachoka kimwili na kiroho.

Yote ni kutaka kuonekana katika hali fulani ya maisha ya juu, mwingine atahakikisha anakopa na pesa ili kuendana na mitindo ya nguo au gari. Ila ukimwangalia katika uhalisia hana pesa za kufanya hayo yote, ila anataka na yeye aonekane yumo.

Badala yake anajikuta yupo kwenye madeni mengi sana, ambapo haikuwa na sababu ya yeye kuingia katika matatizo hayo.

Wengine wanaenda mbali zaidi, kuanzima vifaa vikubwa kama magari ili kuonekana maisha safi. Kumbe sivyo ilivyo, unakuta hata pesa ya mafuta anakopa ilimradi azunguke tu na gari ambalo wakati mwingine sio lake.

Ukija anapolala hafananii kabisa na fujo zake huko nje, ukija kwenye familia yake haifanii kabisa na jinsi alivyo yeye. Kwanini, ni kwa sababu maisha anayoishi siyo maisha halisia.

Wakati masikini anahaingaika kuishi maisha ya kitajiri, wapo matajiri wakubwa wanaopenda kuonekana wana maisha ya chini.

Kuna watu wana pesa nyingi sana, na wana mali za kutosha, ila jinsi wanavyoishi unaweza usiwatambue kabisa kutokana na vile wanaishi kinyonge kwa kulia njaa kila siku.

Wakati wengine wanali hali ngumu, na yeye huwezi kumkosa katika kundi hilo hata kama hali yake ipo vizuri. Hii ni kutaka kuonekana ni mdhaifu wakati sio kweli ni mdhaifu.

Wapo Matajiri hata kuvaa kwao vizuri ni changamoto kubwa, wakati mwingine wanasababisha watu waanze kuwafikiria vibaya kuwa huenda mali walizonazo si za halali.

Maana hata katika matukio ya kijamii huwezi kuwaona wakitoa pesa zao au mali zao kuwasaidia wahitaji. Wao siku zote wanaishi kama mtu asiyekuwa na kitu kabisa, ila kiuhalisia ni watu matajiri sana.

Wakati mwingine ni nzuri sana kama itatumika kwa hekima au busara ikiwa utajiri wake hauna masharti ya kigiza. Lakini kama wanafanya hivyo kwa ajili ya kutoonekana wanajikweza/wanajiinua, inakuwa nzuri sana.

Rejea: Kuna mtu mwenye kujitajirisha, lakini hana kitu; Kuna ajifanyaye kuwa maskini, lakini ana mali nyingi. MIT. 13:7 SUV

Usiishi maisha ambayo yapo nje ya kiwango chako, mpaka pale inapokulazimu kufanya hivyo. Ila kama haikulazimu kufanya hivyo, ishi kulingana na kiwango chako cha kipato.

Jishushe kwa faida ya kutoonekana kero kwa wengine, ila usiishi kama huna kitu mpaka unaitesa na familia yako. Yaani familia inakula chakula kisichofaa kwa sababu ambazo hazina hata msingi wowote, ni sawa unaweza kufanya hivyo kwa manufaa fulani ila usizidishe kiwango.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu
www.chapeotz.com
+255759808081