Kuna msemo mmoja unasema hivi, ukitaka kumficha mtu kitu hasa mtanzania, kiweke kwenye maandishi. Hapo utakuwa umemaliza kila kitu, maana hatokijua au hatokiona, kwa sababu ya kutopenda kusoma vitabu.
Msemo huu unaonekana kama hauna ukweli ila ukiutazama vizuri, utajua kuna ukweli mkubwa sana ndani yake. Sio lazima utazame watu wengine, unaweza kujitazama wewe mwenyewe, ukajiuliza umesoma vitabu vingapi mpaka sasa vya watumishi mbalimbali wa Mungu?
Unaweza kujiuliza ndani yako una msukumo kiasi gani kutafuta maarifa yaliyo ndani ya vitabu mbalimbali. Huwa unatenga bajeti ya kununua kitabu hata kimoja kwa mwezi? Jipe jibu mwenyewe bila kunishirikisha jibu hilo.
Jiulize umakini wako wa kusoma Neno la Mungu uko vipi, unajibidiisha kusoma Neno la Mungu kwa bidii zako zote au mpaka usukumwe kwa nguvu. Au huwa unasoma ukijisikia kufanya hivyo, yaani ndani yako hauna msukumo wa upendo. Jipe jibu mwenyewe.
Hadi hapo unaweza kukubaliana nami kwamba, wengi hatupendi kusoma vitabu, wengi hatupendi kusoma Neno la Mungu. Ni wasomaji wazuri wa midomoni ila kwenye matendo huwa hakuna kitu.
Unaweza kuwa wewe unayesoma hapa ni msomaji mzuri wa vitabu, unaweza kuwa ni msomaji wa Neno la Mungu. Hebu tazama ndugu zako, majirani zako, wafanyakazi wenzako, wanafunzi wenzako, wafanyabiashara wenzako. Ni wangapi unawaona kwenye muda wao wa mapumziko wanakuwa na zoezi la usomaji vitabu?
Hili tunaliona ni jambo la ziada sana, tunaona kusoma vitabu ni jambo ngumu sana, ndio maana wengi wetu tumekosa mambo mengi ya msingi yaliyo ndani ya vitabu.
Katika kusoma vitabu vya watumishi wa Mungu, unaongeza ufahamu ndani yako, katika kusoma kitabu kitakatifu cha Biblia. Utajua mengi usiyoyajua, Mungu wetu ameweka kila kitu ndani ya Neno lake, ili uweze kuelewa mengi unahitaji kuwa msomaji mzuri na makini.
Sio usomaji tu uonekane na wewe unasoma, unahitaji umakini mkubwa katika usomaji wako wa vitabu/kitabu. Katika umakini wako yapo mengi sana utayafahamu na kupata mwanga, kama ni kuchukua hatua, utaichukua mapema.
Hili tunajifunza kwa mtumishi wa Mungu Daniel, Daniel alikuwa msomaji wa vitabu, hii ilimfanya kufahamu mengi. Alijua yanayokuja mbele baada ya miaka fulani, kujua kwake kulitokana na usomaji wake wa vitabu.
Rejea: Katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danieli, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la BWANA lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini. DAN. 9:2 SUV.
Daniel alifahamu yale Mungu alizungumza na Nabii Yeremia kipindi hicho, alipata kufahamu kuhusu ukiwa ukatakaoupata Yerusalem. Kitendo cha kufahamu hayo kupitia vitabu kilimfanya achukue hatua ya maombi, maombi yaliyochukua majuma kadhaa.
Nini kilimfanya Daniel aingie kwenye maombi ya toba, nini kilimsukuma Daniel kumwendea Mungu. Ni yale maarifa aliyoyapata kwenye vitabu, vitabu vilivyohifadhi ahadi za Mungu.
Sijui unalichukuliaje hili la kusoma Neno la Mungu au vitabu mbalimbali, sijui umeona nini kupitia andiko hili takatifu. Kuna ujumbe mzito sana limebeba andiko hili, ujumbe unaotukumbusha umhimu wa kujifunza Neno la Mungu.
Unapojifunza yapo mambo utayafahamu na kuchukua hatua, katika kusoma Neno la Mungu utajua ahadi za Mungu, utajua wakati/majira ya Mungu kutimiza ahadi zake kwako. Utafahamu wakati tuliopo ni wakati wa namna gani.
Unaweza ukawa umeokoka sawa ila ukawa hujui haki zako nyingi mbele za Mungu, unaweza kunyanyaswa na changamoto ndogo kwa kukosa maarifa ya kiMungu ndani yako.
Kuna mambo ya kupuuza katika safari ya maisha yako, wewe ukawa unashikilia kiasi kwamba yanakunyima amani moyoni. Kumbe shida yako haipo kwenye hayo yanayokusumbua, shida yako ipo kwenye ufahamu wako, vile unachukulia mambo ndivyo yanavyokutesa.
Biashara yako inawezekana kabisa haendi vizuri sio kwa sababu ya shetani, ni kwa sababu huna maarifa sahihi ya kuweza kuendesha biashara yako.
Ndoa yako inawezekana kabisa inakusumbua sana, elewa sio wakati wote ni shetani hapendi uwe na amani. Ni vile umekosa maarifa yanayopatikana kwa gharama ndogo ndani ya vitabu.
Unahitaji kusoma vitabu mbalimbali, jenga nidhamu hii maisha yako yote, upo kwenye gari soma kitabu, upo stand unasubiri gari liondoke, soma kitabu. Upo uwanja wa ndege unasubiri muda ufike uondoke, soma kitabu, upo mahali unasubiri mtu, chukua kitabu soma.
Utaanza kuona mabadiliko makubwa katika maisha yako, utaanza kuona mengi ambayo hukuyajua hapo kabla. Utachukua hatua sahihi kwa sababu una ufahamu ndani yako.
MUHIMU: Kama bado hujajiunga na group la WhatsApp la kusoma Neno la Mungu kila siku, group linalokujengea nidhamu ya kujifunza maneno ya Mungu kila siku. Unakaribishwa sana ujiunge na group hili, kama unasikia moyoni mwako kuungana nasi, tuma ujumbe wako kwa WhatsApp namba +255759808081. Tumia WhatsApp tu na sio sms ya kawaida.
Mungu akubariki sana.
Samson Ernest.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081