Haleluya,
Muda mwingine tumejinyima fursa wenyewe mbele za Mungu kutokana na ugumu wa mioyo yetu. Hatutaki kufuata kile tunaelekezwa tukifuate, tukiona ni mateso kwetu ila madhara yake huwa makubwa kuliko tungetoa gharama hiyo.
Sawa na mtu anayeona kununua chandarua ataingia gharama, anaacha mbu wanamng’ata kweli kweli. Mwisho wa siku anaugua malaria kali sana, gharama iliyotumika kumtibu ugonjwa wake inazidi hata ile bei ya chandarua.
Sawa na mtu anayebania kumtolea Mungu ZAKA alafu kile kiasi alichokibana, utashangaa kinaishia kwenye vitu ambavyo akija kutulia anaona bora angewagawia hata maskini. Maana pesa imepotea kizembe kizembe, mara watoto wanaumwa, mara wazazi wanaumwa, mara yeye mwenyewe anaumwa, mara amepoteza pesa katika mazingira asiyoyajua.
Katika ufahamu wake alisema anaokoa gharama kwa kubana matumizi kumbe amefungua mlango mwingine mbaya zaidi. Ukweli ni kwamba suala la matumizi na kupanga bajeti ni suala la msingi sana kwa kila mmoja wetu. Ila inapofika suala la kumtolea Mungu wako uwe na moyo wa kupenda katika kufanya hivyo.
Ndivyo walivyo watu wengi katika dunia ya leo, wanafikiri kuishi maisha matakatifu ni utumwa, wanafikiri kuokoka kunaondoa uhuru wao. Wanachoamua ni kutookoka, ili waendelee kula starehe za dunia hii.
Wanapoendelea kupuuza baadhi ya mambo mbalimbali ya Mungu, ndivyo Mungu naye anazidi kuwa mbali nao Wakati mwingine Mungu angeweza kumwokoa na hatari fulani katika maisha yake, inakuwa ngumu kwa sababu tayari ameshamwekea Mungu mipaka ya kutoweza kumsaidia.
Hili ndilo linawatesa watu wengi sana, mama anaenda kanisani kumwomba Mungu amsaidie mume wake aache kumtesa. Wakati huo anatembea na kijana mdogo kwa uzinzi.
Unakutana na kijana anaomba Mungu ampe mke mwema, alafu anaye dada ndani anaishi naye au kama haishi naye wanakuwa wanafanya naye mapenzi kama mke na mume.
Mungu anapotazama hivi anashindwa amsaidie vipi maana tayari amechanganya mafaili. Maana Mungu wetu hakai katika uchafu, anahitaji mtu wake aliyemsafi mbele zake na anayetii maagizo yake.
Tumezuia mambo mengi Mungu kutotundea kwa kutokuelewa au kwa kuelewa kabisa tunachofanya Mungu hataki tufanye tukiwa kama watoto wake.
Tunaweza kulalamika Mungu hasikii maombi yetu, ila tukija katika uhalisia tunaona mambo mengi bado hujatengeneza na Mungu wako. Kama umeamua kuokoka, kubali kusikiliza Mungu anasema nini, anataka nini, ili uwe na uhakika na wokovu ulionao.
Rejea: Laiti watu wangu wangenisikiliza, Na Israeli angeenenda katika njia zangu; Ningewadhili adui zao kwa upesi, Na juu ya watesi wao ningegeuza mkono wangu; ZAB. 81:13-14 SUV.
Hebu usizuie baraka za Mungu juu ya maisha yako ya wokovu, kwa sababu tu umemweka mtu moyoni tangu alivyokukosea mwaka juzi. Umeshindwa kumwachilia moyoni mwako na hilo limekuwa gereza lako.
Mungu wetu ni mwaminifu sana kwetu, anahitaji utiifu wetu sana na kuishi maisha matakatifu. Ili tuweze kupata hizo ahadi alizotuahidia sisi wanadamu.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu
www.chapeotz.com
+255759808081.