“Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi”, Mt 2:16 SUV.

Jaribio la Herode mfalme wa Uyahudi kutaka kumua Yesu aliyezaliwa Bethlehemu, linatufundisha mambo mengi sana katika maisha yetu ya leo. Kwanini nasema hivyo, agizo la kuwaua watoto wote wa kiume wenye umri wa miaka miwili na chini ya hapo waliokuwako huko Bethlehemu, hawakuwa na hatia yeyote na wala hawakukosea jambo lolote.

Aliyesababisha watoto hawa wauawe sio mamajusi walioagizwa na Herode walete ripoti, badala yake hawakuleta hiyo habari baada ya kuonywa na Mungu wasirudi kwa Herode kumpa habari za mtoto Yesu.

“Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine”, Mt 2:12 SUV.

Ninachokiona hapa waliokuwa nafasi nzuri ya kuweza kumpa Herode taarifa sahihi za mtoto aliyezaliwa, walikuwa hawa mamajusi, mamajusi wanaozungumziwa hapa ni watu waliokuwa wasomi na waliobobea katika unajimu, tiba na sayansi ya asili.

Watu hawa walikuwa na elimu ya nyota, nyota waliyoiona walijua sio nyota ya kawaida, walijua kilichotokea huko Bethlehemu hadi wakafunga safari ya kwenda wakiwa na zawadi. Hili tunaliona kutokana na andiko hili;

“Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia”, Mt 2:2 SUV.

Ujumbe huu ulimfedhehesha sana Herode ambaye alikuwa mfalme wakati huo, akawa amewaagiza mamajusi wamletee ripoti baada ya kumwona mtoto, walikubaliana kufanya hivyo ila baada ya kumwona na kutaka kuanza safari Mungu akawa amewaonya wasirudi kwa Herode.

Wakati Herode anatangaza kuuawa kwa watoto wakiume, alikuwa anajua katikati ya watoto hao atauawa huyu mfalme aliyekuwa anazungumzwa na mamajusi, agizo lake lilitekelezwa na watoto wa kiume wakawa wameuawa vibaya sana.

Lile lengo au kusudi la Herode halikufanikiwa maana Yusufu alipewa maagizo ya kumhamisha mtoto na mama yake kumpeleka mahali pengine kukwepa kuuawa na Herode.

“Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize”, Mt 2:13 SUV.

Tunajifunza nini hapa katika kisa hichi, mtu mmoja anaweza kusababisha mauaji na hasara kwa wengine, anaweza akawa mtu mzuri au mbaya, akawaletea shida kwenye nchi yenu, mkoa wenu, wilaya yenu, kata yenu, kijiji chenu, ama ofisini kwenu unapofanyia kazi.

Hili tunaliona hata kwa Yona, alisababisha kizaazaa baharini, meli ilitaka kuzama kwa sababu ya Yona aliyepewa wajibu na Mungu alafu yeye akakimbilia mji mwingine kukwepa wajibu aliopewa na Mungu (Yona 1:1-6). Wasingemtoa na kumtupa baharini hiyo meli ingezama baharini.

Yesu alisababisha watoto wengine wauawe, hapa kusudi la Mungu lilikuwa linatafutwa kupotezwa au kufutwa kabisa, katika harakati ya kulipoteza hilo kusudi wengine wakawa wamepata shida ngumu, wazazi wakawa wamepoteza watoto wao pasipo kujua anayetafutwa ni Yesu.

Usishangae kazi yako ikaharibika kwa sababu kuna mtu mmoja ofisini kwenu alikusudiwa na Mungu akaifanye kazi yake mahali, alafu mtu huyo akawa hataki kutii wito wa Mungu. Ili mtu huyo aache kujivunia kazi yake nzuri, hicho kitengo ulichokuwa unafanyia kazi kikaondolewa na wengine mkakosa nafasi ya kazi.

Usishangae mkaletewa masheria magumu magumu kwa sababu ya mtu mmoja anayesumbua taifa, na usishangae mkakutana na kipindi kigumu cha kupoteza ndugu zenu kwa sababu kuna mtu alikuwa anatafutwa auawe ili kuzima mpango wa Mungu usitimie.

Kusudi la Mungu likiwa limekusudiwa kuwatoa watu au wananchi kutoka mahali fulani pabaya, kusudi hilo linaweza kusababisha madhara makubwa kwenye jamii au nchi. Kinachotafutwa hapo ni kuharibu mpango wa Mungu usitimie kwa lile lililokusudiwa, lakini tunaona Yesu hakuuawa na kusudi la Mungu lilitimia.

Tunapaswa kuombea sana mipango yetu, unaweza ukawa na maono makubwa sana na maono hayo yakawa yanalenga kusaidia kanisa au jamii au nchi, usifikiri yatatimia kirahisi, unaweza kukutana na upinzani na vita kali sana. Unaweza kupoteza baadhi ya vitu, hii ni kwa sababu Shetani anataka kuzima maono uliyonayo.

Habari njema ni kwamba Mungu akiwa upande wako Shetani hataweza kuzima mpango wa Mungu kwako, lile lililokusudiwa litimie kwako litatimia kwa jina Yesu Kristo, endelea kumtumainia Mungu siku zote za maisha yako.

Soma neno ukue kiroho

Mungu akubariki sana

Samson Ernest

+255759808081