Nakusalimu katika jina la Bwana wetu YESU Kristo aliye hai. Nakuomba twende pamoja tujifunze jambo mhimu sana hapa.
Wapo watu wanaandaliwa kwa ajili ya kutengeneza njia, njia ambayo watapita wengine pasipo shida yeyote.
Watengeneza njia hawa mara nyingi huonekana sio watu wa mhimu sana, kutokana na kazi ngumu wanazofanya.
Sawa na mtu anayefanya usafi wa barabara anaoekana ni mtu wa hali ya chini sana, na wakati mwingine ana dharaulika sana na jamii. Lakini kupitia mfagia barabara huyu, mji unaonekana upo safi, na wakati mwingine mkoa unaweza kupewa zawadi ya usafi.
Sawa na mtu anayefanya kazi ya kusugua vyoo, anaonekana ni mtu aliyekosa dira ya maisha. Lakini kupitia mtu yule, tunafurahia kukaa chooni maana ni kisafi.
Watengeneza njia za watu zinazopita katikati ya mapori, wapo watu waliokata miti na kung’oa magogo/visiki ili barabara ipitike vizuri.
Hakuna anayejali sana hili, wengi wetu tunaona ni vitu vya kawaida sana. Wakati mwingine tunaweza kuwasema tunavyojua sisi bila kujua umhimu wao.
Unaweza kujivunia ng’ombe wako anatoa maziwa vizuri, ukasahau kumpongeza yule mchunga ng’ombe unayemlipa pesa kidogo.
Nasema hivi; wapo watumishi wa MUNGU waliopita katika nyakati ngumu kuipigania imani yetu, wapo waliotembea kwa miguu umbali mrefu kutangaza injili ya Bwana wetu YESU Kristo.
Watumishi wale wasipoangaliwa vizuri, wanaweza kuonekana ni watu wa kawaida kawaida tu.
Huenda huduma uliyonayo, imechangiwa asilimilia kubwa kuwa hivyo ilivyo na mtu unayemwona ni wa kawaida tu kwako.
Huenda hapo unaposali kuna jengo zuri sana, hilo jengo wapo watu waliojitoa kwa mali zao ili lisimame.
Pamoja na kujitoa kote huko, huenda hao watu hawakufaidi kabisa matunda ya matendo yao. Ni sawa na kusomesha mtoto miaka mingi lakini usije ukafaidi matunda ya mwanao wakafaidi wengine.
Huenda hapo ulipo una mali za kutosha kwa sababu wazazi wako waliweka akiba kwa miaka mingi, akiba ambayo imekuwa chachu ya mafanikio yako.
Tunazungumza na watengeneza njia, watu ambao mara nyingi hawaonekani sana katika jamii zetu.
Habari hii tunaiona kwa mtumishi Daudi, Daudi aliacha kizazi chenye kustarehe na kula raha za jasho lake.
Daudi alipigana vita sana, mpaka kupelekea Mungu kumzuia kujenga hekalu lake la kumwabudu yeye, kwa sababu ya umwagaji damu nyingi.
Badala yake mwanaye Suleiman akapata kibali cha kuja kuijenga nyumba ile ya Bwana, na kupewa fursa nyingine ya kuja kustarehe na watu wake.
Rejea; Tazama, utazaliwa mwana, atakayekuwa mtu wa kustarehe; nami nitamstarehesha mbele ya adui zake pande zote; kwani jina lake litakuwa Sulemani, nami nitawapa Israeli amani na utulivu siku zake.1 NYA. 22:9 SUV.
Usijikie vibaya kutenda kazi ya Bwana kwa bidii zote, haijalishi akina nani watakuja kufaidi juhudi zako. Tenda kazi ya Bwana kwa moyo wako wote, usivunjike moyo kwa vikwazo vilivyo mbele yako.
Tunaona mfalme Daudi akiacha hazina kubwa hemani mwa Bwana, wakati wapo watu wakishaona wanakaribia kuondoka duniani au madarakani au kustafu wanaanza kutapanya mali ili wengine waje waanze upya.
Rejea; Basi sasa, tazama, katika shida yangu, nimeiwekea akiba nyumba ya BWANA, talanta elfu mia za dhahabu, na talanta elfu elfu za fedha; na shaba na chuma isiyo na uzani; kwa vile zilivyo tele; miti tena na mawe nimeweka akiba, nawe utaweza kuongeza. 1 NYA. 22:14 SUV.
Usijikie vibaya kuachia wengine akiba ya kutosha kwenye akaunti zako bank, usione wivu kuachia wadhifa kanisa likiwa na miradi ya kutosha ya maendeleo.
Usitapanye mali kwa kuona umekuwa mzee, usivuruge/usisambaratishe vitu kwa sababu unaenda kuachia ngazi/nafasi ya kiti ulichokalia. Hiyo ni roho ya wivu mbaya, usikubali ikuingie na kukutawala.
Umewahi kuona mtu anahama nyumba ya kupingisha anang’oa hadi switch za umeme, ukimuuliza anakwambia alinunua mwenyewe. Kwani akiziacha wengine wakaja kutumia ni vibaya? Hiyo ni roho mbaya.
Tengeneza njia ukijua na wengine watapita, usitengeneze tu kwa ajili yako, ukipita unarudishia mimba ili wengine waje washindwe kupita. Acha hiyo roho, maana neno la Mungu linatufundisha hapa.
Haijalishi unaowaachia watakukumbuka au hawatakukumbuka, hilo lisikufanye ukashindwa kuweka mipango yako vizuri. Hata hicho unachojivunia leo, yupo alikesha usiku na mchana akikihangaikia.
Mungu akusaidie uelewe zaidi haya yaweze kukusaidia.
Samson Ernest.
+255759808081.