Sifa na utukufu tunamrudishia Bwana wetu YESU Kristo, kwa uweza wake mpaka kufikia wakati huu. Nakusalimu katika jina la Bwana wetu YESU Kristo aliye hai, habari za muda huu mpendwa.
Maeneo mengi tunaongozwa, kama unaongoza lazima kutakuwepo eneo kuna mtu anakuongoza pia. Unaweza kuwa mkurugenzi kwenye kampuni yako, ila ukawa chini ya balozi wa nyumba kumi. Unaweza kuwa kiongozi wa idara fulani kubwa nchini, ila ukawa chini ya mchungaji/Askofu wako.
Kila mahali kuna uongozi wake, zipo sehemu utaheshimiwa kwa nafasi yako uliyonayo katika jamii. Ila kuna sehem utapaswa kuwa chini ya kiongozi fulani, kwa eneo ambalo upo wewe pamoja na nafasi yako utalazimika kuongozwa na kuheshimu ngazi husika.
Unapaswa kutii mamlaka iliyo juu yako, haijalishi hiyo mamlaka inaenda ndivyo sivyo, ilimradi tu haikulazimishi kuabudu miungu mingine. Unapaswa kuitii na kufuata yale maagizo inakupa ufanye/utende.
Sawa na askari akapewa amri ya kusonga mbele na mkuu wake akaanza kurudi nyuma kwa kuona hatari mbele, kufanya hivyo kuna weza kumsabishia madhara ya kuawa kwa kushindwa kutii amri ya mkuu wake.
Mungu kukutumia katika nafasi yako ya utumishi/uongozi unaweza kusabisha madhara, pamoja na Mungu kututumia kule, shetani akatumia mwanya ule ule kukuingizia mawazo potofu ya kumkosea Mungu wako.
Tunapata sifa nyingi sana za mfalme Daudi jinsi alivyomtegemea na alivyomtanguliza Mungu kabla hajapigana vita vyovyote. Ila ikatokea shetani akamwingizia wazo ambalo halikuwa la Mungu, Daudi akachukua hatua moja kwa moja pasipo kujua ni maagizo potofu ya shetani na si ya Mungu.
REJEA; Tena shetani akasimama juu ya Israeli, akamshawishi Daudi kuwahesabu Israeli. Basi Daudi akamwambia Yoabu, na wakuu wa watu, Nendeni kawahesabu Israeli toka Beer-sheba mpaka Dani; mkanipashe habari, nipate kujua jumla yao.
1 NYA. 21:1-2 SUV.
Daudi alimpa amri Yoabu aende kuwahesabu watu kama alivyoagizwa na bwana wake, ila Yoabu alishtukia hilo jambo si jema. Pamoja na kutokuwa na amani na agizo la bwana wake, Yoabu ilimbidi afuate maagizo ya bwana wake Daudi pasipo kukataa.
REJEA; Naye Yoabu akasema, BWANA na awaongeze watu wake mara mia hesabu yao ilivyo; lakini, bwana wangu mfalme, si wote watumishi wa bwana wangu? Mbona basi bwana wangu analitaka neno hili? Mbona awe sababu ya hatia kwa Israeli? Lakini neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu. Kwa hiyo Yoabu akaenda zake, akapita kati ya Israeli wote, akafika Yerusalemu.1 NYA. 21:3-4 SUV.
Umeona hapo, nazungumzia kutii amri na mamlaka iliyo juu yako, inaonekana hapa Yoabu kuna alarm nyekundu iliwaka ndani yake, ila agizo la bwana wake likawa na nguvu zaidi, akalitii.
Kumbe alarm ile ilikuwa ni tahadhari kwa jambo analoenda kulifanya ni chukizo mbele za Mungu. Ambalo hili chukizo lilimfanya Daudi kuingia hatiani mbele za Mungu.
Shetani anaweza kutumia mamlaka aliyonayo kiongozi, kuleta madhara katika kanisa/jamii. Kiongozi/mtumishi anaweza kuona yupo sahihi kumbe ameingiziwa wazo potofu na shetani.
Mhimu sana kuwaombea viongozi wetu wa serikali na watumishi wetu wanaotuongoza, na kutulisha NENO LA MUNGU. Wakati mwingine shetani anaweza kujichomeka pasipo kujua haraka akaleta madhara makubwa, wakati tungezuia haya kwa maombi yetu.
Rejea; Neno hilo likawa baya machoni pa Mungu; kwa hiyo akawapiga Israeli. Naye Daudi akamwambia Mungu, Nimekosa sana, kwa kuwa nimelifanya jambo hili; lakini sasa uuondolee mbali, nakusihi, uovu wa mtumwa wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa.1 NYA. 21:7-8 SUV.
Huwezi kupingana na mamlaka iliyowekwa na Mungu, ila unaweza kuiombea mamlaka iliyowekwa na Mungu. Ili shetani asije akatumia mwanya wa kiongozi/mtumishi kuingiza/kuruhusu kitu kibaya cha kumkosea Mungu.
Mungu awasaidie viongozi wetu wa nchi/dini wapate kuenenda katika mapenzi ya Mungu, wasije wakatuhimiza kutenda yasiyompendeza Mungu tukaingia katika hatia.
Mungu akubariki sana.
Samson Ernest.
+255759808081.