“Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao”, Mt 5:10 SUV.

Sio habari jema sana kukuambia maneno haya, hasa wewe ambaye umeshaokoka, yanaweza yasiwe sehemu ya kuufurahisha sana moyo wako ila ni maneno ambayo yatakujenga sana katika maisha yako ya Imani.

Wakati mwingine ni vizuri kuujua ukweli, unapoujua ukweli kuna maeneo Shetani hatakuonea, unaweza kufika wakati ukajiona una mikosi wakati huo umeokoka na Yesu ni Bwana na Mwokozi wa maisha yako. Wakati kiuhalisia hauna mikosi isipokuwa kuna kweli ya Mungu bado hujaifahamu kupitia neno lake.

Unapaswa kuelewa hili na kama ulikuwa na mtazamo mbaya juu ya wale wanaopitia mateso, ninaamini baada ya kusoma Makala hii mtazamo wako utakuwa umebadilika. Fahamu kwamba mateso yatakuwa ni sehemu ya wale wote wanaotafuta kuishi kulingana na Neno la Mungu kwa ajili ya haki.

Wale wote wanaoshikilia viwango vya Mungu vya kweli, haki na usafi, na ambao kwa wakati huo huo wanakataa kufanya upatanisho na jamii ya sasa ya uovu au maisha ya uvuguvugu ya waamini wenzao.

“Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa change”, Ufu 3:15-16 SUV.

Watu hao lazima watapitia hali ya kutopendwa, kukataliwa na kukosolewa vikali mno. Mateso na upinzani mkali vitatoka duniani na wakati mwingine utatoka kwa wale walio ndani ya kanisa linalomkiri Mungu wa kweli, yaani wapendwa wenzao.

Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa-mwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi; tena katika ninyi wenyewe watainuka watu wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao”, Mdo 20:29-30 SUV.

Wale Wakristo wote wanaopitia mateso haya kwa ajili ya haki, wanapaswa kufurahi na sio kujiona wana mikosi na balaa (Mt 5:12), kwa kuwa wale wanaoteseka Zaidi Mungu huwapa Baraka ya juu Zaidi.

Kwa kuwa kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi kwetu, vivyo hivyo faraja yetu inazidi kwa njia ya Kristo”, 2 Kor 1:5 SUV.

Ukiwa mkristo unapaswa kuwa macho sana na umakini wa hali ya juu, juu ya jaribu la kuafikiana ukiukwaji wa mapenzi ya Mungu ili kuepuka aibu ya watu. Yapo mambo mabaya yasiyompendeza Mungu unapaswa kuyaepuka, hata kama watu watakuona mshamba.

Elewa kwamba kanuni za ufalme wa Mungu kamwe hazitakaa zibadilike, wote wanaopenda kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa tu. Unapoudhiwa usijione umetengwa/umeachwa na Mungu au huna nguvu za Mungu, jua hiyo ni hali ya kawaida kwa mwamini.

Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa”, 2 Tim 3:12 SUV.

Wale ambao wanateseka na kuvumilia mateso kwa ajili ya Imani yao ndani ya Kristo wameahidiwa ufalme na thawabu za mbinguni. Hii ni ahadi nzuri sana kwa mkristo, ambayo anapaswa kuifahamu.

Simama imara, usiyumbishwe na dunia hii, ipo mitazamo mingi iliyo kinyume na Neno la Mungu inayoshawishi kumtenda Mungu dhambi, ukiwa kama mwana wa Mungu usiingie kwenye jaribu hilo.

Usisingizie maisha yamekuwa magumu ukajiingiza kwenye vitendo vya ujambazi au uporaji, ukahaba, utapeli na mengine yanayofanana na hayo. Vumilia hata kama unapitia kwenye hali ngumu ya uchumi, akija mtu akakushawishi kufanya kitendo kibaya ili kujipatia pesa usikubali.

Asije mtu akatumia neno vibaya, akakuambia majaribu unayopitia ni kwa sababu ya ujinga wako, kisa umekuwa mwaminifu ofisini kwako, au kwenye nafasi uliyowekwa, au kwenye maisha yako ya wokovu. Wengine wakiwa chuoni wanashindwa kutunza ushuhuda wao, wanajiingiza kwenye vitendo viovu kujitafutia fedha.

Maarifa haya utayapata kupitia usomaji wako wa neno la Mungu, usiache kutenga muda wako kusoma na kufakari neno la Mungu. Kama unahitaji kuungana na wenzako wanaosoma biblia kila siku, unaweza kuungana nao kwenye kundi la wasap kwa namba +255759808081.

Soma neno ukue kiroho

Mungu akubariki sana

Samson Ernest

+255759808081