Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. [ Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.] Mk 11:25‭-‬26 SUV

Wakristo hatupaswi kujidanganya kuwa tunayo imani ya kutosha na tukiomba lolote tutajibiwa na Mungu wetu.

Ikiwa ndani ya mioyo yetu tuna chuki au uchungu dhidi ya mtu yeyote aliyetukosea au aliyetufanyia mabaya.

Tuwe na uhakika maombi yetu mbele za Mungu hayatakuwa na kibali, na tunaweza kusababisha kutopata majibu ya mahitaji yetu.

“Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake”, Mt 18:35 SUV.

Mtu akikukosea inaumiza sana, pamoja na kuumizwa sana unapaswa kusamehe, kuachilia moyoni mwako dhidi ya aliyekukosea kunaleta utulivu ndani yako.

Ukimshikilia sana moyoni mwako aliyekufanyia jambo baya, ukawa na uchungu na maumivu naye, unajinyima fursa nyingi mbele za Mungu.

Utasema unajua nimeumizwa sana Samson, mambo niliyofanyiwa ni magumu mno na ungekuwa ni wewe usingeweza kusamehe.

Siku moja ndugu mmoja alikuja ofisini, kisa alichonieleza na mateso aliyopitia, yalikuwa ni mambo mazito sana hadi nilitoa machozi bila kupenda.

Nilimwambia ili uweze kupona majeraha yako ya moyo na uwe mtu mzuri na mwenye mahusiano mazuri na Mungu, unahitaji kusamehe.

Alilia sana sana, namshukuru Mungu alinisaidia na akanielewa na tukaagana vizuri, ulipita muda mrefu kidogo bila kuonana. Siku moja alikuja ofisini kushukuru na kunieleza sababu ya kupotea, ilikuwa sababu ambayo ilikuwa kwenye mazungumzo yetu yaliyopita.

Huyu ndugu baada ya kusamehe Mungu alimfungulia mambo mengi sana na kumpa kibali cha kupata kazi, maisha aliyokuwa anaishi yalikuwa ya aibu lakini Mungu akamsaidia mambo mengi.

Nini nataka kukuambia hapa, kusamehe kunafungua mengi sana, unaweza kuzuia mambo mengi Mungu kukutendea kwa sababu ya kutosamehe kwako.

Samehe na uachilie, utamwona Mungu kwa namna ya pekee katika maisha yako.

Soma neno ukue kiroho
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081