“Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi”, Mt 1:23 SUV.

Mathayo na Luka katika vitabu vyao vya injili, wote wanakubaliana kuwa Yesu Kristo alichukuliwa/ilitungwa mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu na alizaliwa na mama bikira bila ya kulala au kuingiliwa na baba wa kibinadamu.

“Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu”, Mt 1:18 SUV

“Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu”, Lk 1:34-35 SUV

Mafundisho ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo na mwanamke bikira yamepingwa sana kwa miaka mingi na WANATHEOLOJIA HURIA. Pamoja na upinzani huo, ni jambo lisilopingika kuwa nabii Isaya alitabiri mtoto atakayezaliwa na bikira ataitwa “Imanueli”, neno hili la kiebrania linalomaanisha “Mungu pamoja nasi”

“Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli”, Isa 7:14 SUV.

Utabiri huu ulitolewa miaka 700 kabla ya kuzaliwa kwa Kristo, unaweza kuona ni jinsi gani unabii huu ulichukua miaka mingi sana hadi kutimia kwake. Kwa hiyo halikuwa tukio la ghafla, lilishatabiriwa miaka mingi nyuma.

Neno “bikira” katika Mathayo 1:23 ni tafsiri sahihi ya neno la Kiyunani “parthenos” linalopatikana katika nakala za Septuaginta (tafsiri ya Agano la Kale la Kiyunani) katika Isaya 7:14.

Neno la Kiebrania la bikira (almah) lililotumiwa na Isaya lina maana ya bikira aliye na umri wa kuolewa na ambaye hajakutana na mwanaume, na halitumiki katika Agano la Kale kwa hali yoyote ile nyingine isipokuwa ile ya ubikira (Mwa 24:43; Wimb 1:3; 6:8).

Hivyo, Isaya katika Agano la Kale pamoja na Mathayo na Luka katika Agano Jipya wote wanampa sifa ya ubikira mama yake Yesu (Rejea Isa 7:14). Hawa wote watatu wanaweka wazi mwanamke bikira atakayemzaa Yesu Kristo, sio hao tu ukisoma vitabu vingine utaona wanamtabiri Yesu.

Umuhimu wa kuzaliwa na bikira hauwezi kutiwa mkazo kupita kiasi. Ili Mkombozi wetu aweze kuwa na sifa ya kulipia dhambi zetu na kuleta wokovu, ni lazima awe katika mtu mmoja, mwanadamu kamili asiye na dhambi na Mungu kamili. Kumbuka hili usisahau, hizi ni sifa muhimu sana alizokuwa nazo Yesu na hakuna mtu mwingine mwenye nazo.

“Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee. Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lo lote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu”, Ebr 7:25-26 SUV.

Yesu kuzaliwa na bikira kunatimiza vigezo au matakwa yote haya matatu;

  1. Njia pekee ambayo Yesu angeliweza kuzaliwa mwanadamu ilikuwa kuzaliwa na mwanamke, nje na hapo ingeleta shida.
  2. Njia pekee ambayo ingemfanya azaliwe pasipo dhambi ilikuwa kwa kuchukuliwa mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu (Mt 1:20; Ebr 4:15). Hili lilifanyika kwa asilimia zote na tukaona kwa Yusufu kutaka kumkimbia baada ya kugundua mchumba wake ana mimba.
  3. Njia pekee ambayo kwayo angekuwa Mungu, ni Mungu kuwa Baba yake. Matokeo yake, hakuchukuliwa mimba kwa njia ya kawaida ya asili, bali kwa njia kiungu: “hicho kitakachozaliwa kitakuwa kitakatifu, Mwana wa Mungu” (Lk 1:35). Hili ni muhimu sana kufahamu na kulikumbuka.

Hivyo Yesu Kristo anafunuliwa kwetu kama nafsi ya Mungu yenye asili mbili ya Mungu na ya mwanadamu asiye na dhambi kabisa. Kwa kuishi maisha ya hapa duniani na kuteseka kama mwanadamu mwingine yeyote, Yesu anatuhurumia katika udhaifu wetu (Ebr 4:15-16).

Yesu kama Mwana wa Mungu wa kiungu anazo nguvu za kutukomboa na utumwa wa dhambi na nguvu za Shetani (Kol 2:15; Mdo 26:18; Ebr 7:25; 2:14). Akiwa Mungu na mwanadamu kwa pamoja, yaani Mungu asilimia 100 na mwanadamu asilimia 100, anastahili kutumika kama dhabihu kwa dhambi za kila mtu, na kama kuhani mkuu kuwaombea wote wanaomjua Mungu (Ebr 10:4-12; 2:9-18; 7:24-28; 5:1-9).

Hii ni fursa ya pekee uliyonayo wewe, ukiwa bado hujaokoka au ukiwa bado hujampokea Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako, utakuwa unajinyima kitu cha muhimu sana katika maisha yako ambacho hakipatikani popote isipokuwa kwa Yesu Kristo.

Hujachelewa, unayo nafasi ya kumwamini huyu Yesu niliyekueleza habari zake hapa, huenda ulikuwa unasita kuokoka, baada ya kusoma Makala hii ukawa umejifunza kitu cha pekee, na usikia moyoni mwako kumpokea. Usiache kuchukua hatua ya kumpokea huyu Yesu Kristo, maisha yako yatakuwa ya tofauti sana.

Mwisho, nikukaribishe katika kundi la wasap la kusoma neno la Mungu kila siku na kushirikisha tafakari zetu, hili kundi litakujenga kiroho, utakua kiroho kwa kumfahamu Mungu vyema. Hii itakusaidia kuwa imara katika Imani yako na kujua haki zako za msingi kama mwana wa Mungu, wasiliana nasi kwa wasap namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.

Soma neno ukue kiroho

Samson Ernest

+255759808081