
Jambo hili linashangaza sana, na linazidi kuenea kwa watu wengi waliomwamini Yesu Kristo, sijui huwa wanafikiri ni busara kufanya hivyo, au sijui huwa wanaona ni moja ya kuonyesha utu wao.
Watu wengi wakishamwambia mtu ukweli, na ukweli ule ukamchoma moyo wake, na baada ya kuchomwa moyo wake. Wengi hushindwa kujizuia na kuonyesha hasira yao wazi wazi kwa wale waliokuwa wanawaambia maneno ya kweli.
Sasa tunapokuwa tunahubiri habari za Yesu Kristo, na kuiweka kweli yote wazi, haijalishi nani anaenda kuguswa na hiyo injili. Na akishaguswa na hiyo injili, wapo huwa wanatamani kuzaliwa upya, na wapo huwa wanakasirika na kuona wameingiliwa kwenye maeneo yao.
Wale wanaochomwa na maneno uliyosema kwa msaada wa Roho Mtakatifu, wakaamua kubadili njia zao, hao wanaweza wasihoji mambo mengi sana. Na hawana usumbufu wa aina yeyote, hawawezi kugeuka kikwazo kwako, wala hawawezi kugeuka maadui kwako, kiu yao watataka kutoka kwa yale mambo mabaya waliyokuwa wanafanya.
Rejea: Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? MDO 2:37 SUV.
Hawa ndugu baada ya kuchomwa mioyo yao na maneno ya Petro aliyokuwa anawahubiria, walichukua hatua ya pili kumuuliza wafanyeje? Petro hakuwacheweshea jibu lao, akawajibu hivi;
Rejea: Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. MDO 2:38 SUV.
Unaona hapo mtu wa Mungu, Petro aliwapa suluhisho lao, hakuwaacha waendelee kuumia kwa maneno aliyowaambia. Maana yalikuwa ni maneno ya kweli, maneno yaliyotokana na Neno la Mungu, hayakuwa maneno tu ya mtaani.
Baada ya maneno hayo, wapo walioamua kufanya vile waliambiwa na Petro, hawakuishia kuugua tu mioyo yao, walipopata maelekezo ya namna ya kufanya. Tunaona kupitia andiko hili takatifu, walichukua hatua ya kumwamini Yesu Kristo.
Rejea: Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu. Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali. MDO 2:41-42 SUV.
Hao ni watu wanaliochomwa mioyo yao kwa maneno ya Mungu kupitia kinywa cha Petro, wakaamua kubadili njia zao mbaya na kumgeukia Yesu Kristo. Sasa wapo watu ambao wakishaambiwa kweli ya Mungu kupitia kinywa cha mtumishi wake, yale maneno yakawachoma mioyo yao.
Watu wale hawataka kubadili njia zao mbaya, wataanza kutafuta njia ya kumdhuru yule mtumishi aliyewaambia maneno yakawachoma mioyo yao. Hawa ni tofauti kabisa na wale ambao walisikia maneno yakawachoma mioyo yao, wakachukua hatua ya kutaka kubadilika.
Hawa wanaosikia Neno la Mungu, alafu wakachomwa mioyo yao, mara nyingi humchukia yule mtu aliyesimama kuisema kweli, na wapo huanza kufikiri ni namna gani wataweza kumdhuru aache kuwachoma mioyo yao.
Rejea: Wao waliposikia wakachomwa mioyo yao; wakafanya shauri kuwaua. MDO 5:33 SUV.
Hapa ndipo watu wengi huanza kuomba msamaha kwa kuzungumza kweli ya Mungu, baada ya kuibaini wanataka kuawa; hapa ndipo inashangaza tena, unajiuliza, mtu unaanzaje kuomba msamaha kwa sababu ya kuisema kweli ya Mungu?
Wakristo wengi au watumishi wengi tumekosea eneo hili, kuomba msamaha kwa sababu tuliisema kweli ya Mungu. Baada ya kuisema kweli, watu walichomwa mioyo yao na kutukasirikia, kuomba msamaha huko ni kukosa ujasiri wa Roho Mtakatifu au kukosa maarifa sahihi ya Neno la Mungu.
Ukweli siku zote ni mchungu sana, tena unaweza kukuletea madhara makubwa sana kama utausema kwa watu ambao hawataki kuusikia huo ukweli. Haya madhara yapo hata kwa mambo ya kawaida kabisa ambayo sio injili ya Yesu, ukiwa mkweli na muwazi, utatengeneza maadui wengi sana.
Maadui wengine hawataishia kukuchukia tu moyoni, watachukua hatua ya kutaka kukuua kabisa, furaha yao ni kuona umepotea katika uso wa Dunia hii. Ili wao waendelee kuwa huru kufanya mambo yao, hawajui kuwa ukweli huwa haufi, bali unaishi.
Wengi wetu tunapoona chuki imekuwa kubwa hata kwa ndugu zetu, kwa sababu ya kuisema kweli ya Mungu au kwa sababu ya kusimama katika kweli ya Mungu. Wengi wetu huanza kuwaomba radhi/msamaha wale wote ambao hawakupendezwa na maneno yetu ya ukweli tuliyowaambia, au hawakupendezwa na misimamo yetu ya kusimamia kweli ya Mungu.
Watu kuchomwa mioyo yao na maneno ya kweli, haijaanza leo, imeanza siku nyingi, na Yesu Kristo alikutana na hilo wakati yupo Duniani. Watumishi wengi wa Mungu waliingia kwenye matatizo makubwa kwa sababu ya kuisema kweli ya Mungu, moja wapo ni stefano, pamoja na mateso makali aliyokuwa anateswa, hakuacha kusema kweli.
Rejea: Basi waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia meno. Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu. Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake. MDO 7:54, 59-60 SUV.
Ndugu msomaji wangu, sijui ni mara ngapi umewaambia watu kweli ya Mungu, ulivyoona umegeuka adui kwao na kukosa marafiki. Uliona bora kuacha kuisema kweli au uliona bora kuomba msamaha yaishe, huko tunasema ni kukosa msimamo wa kiMungu.
Sijui ni mara ngapi umesimama upande wa kweli, baada ya kuona unazidi kukosa marafiki na kugeuka kuwa adui kwa watu wengi. Uliamua kuachana na msimamo wako, ili uwapendeze wale wanaopenda kusifiwa tu, hawataki kuambiwa ukweli. Kama ulifanya hivyo, utakuwa ulikosea sana, na utakuwa umejiondoa kwenye kundi la watumishi wa kweli wa Mungu.
Simama kwenye kweli ya Mungu, kweli ya Mungu ni Neno la Mungu, Neno la Mungu linajieleza lenyewe, linajifafanua lenyewe, ukiamua kulihubiri au kulifundisha lenyewe kama lenyewe, linajitosheleza kabisa. Wala huhitaji kutaja dini ya mtu, ukilihubiri Neno lenyewe linamgusa mtu moja kwa moja, bila hata kutaja dini yake.
Sitegemei kama utaomba msamaha tena, kwa sababu ya watu walikuchukia ulivyowaeleza maneno ya ukweli. Usiwe na mashaka na kufikiri labda utakuwa umefanya dhambi, kusema kweli sio dhambi, haijalishi watu watakuchukia sana na kutafuta kukuua. Simama siku zote kwenye kweli ya Mungu.
Nakukaribisha kwenye kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, tuma ujumbe wako wasap kwa namba +255759808081.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com