Kusema kwa mdomo Mungu anaweza mambo yote ni rahisi sana ila ukija katika kuamini hasa pale unapokuwa unapitia kwenye mazingira magumu yanayomhitaji Mungu hausike. Kauli ya Mungu anaweza mambo yote inaweza isifanye kazi kwako, na uhakika wa Mungu anaweza kutenda kila jambo katika maisha yako unaweza usiwepo kabisa.
Kutokuwa na imani/uhakika kuwa Mungu anaweza kutenda yale magumu yanayoonekana kwa akili za kibinadamu hayawezekani. Kunatufanya tuendelee kuzuia majibu ya maombi yetu mengi, ambayo tulienda mbele zake kumwomba atutendee/atufanyie.
Kukosa kwetu imani mbele za Mungu, inaweza ikawa imesababishwa na mambo mengi. Mazingira husika yalivyo yanaweza kututia hofu ya kile tunachofikiri Mungu anaweza kukirejesha katika hali yake ya awali/kawaida.
Kitu kingine ambacho kinatufanya tushindwe kuamini Mungu anaweza kufanya mambo makubwa na magumu kwa akili za kibinadamu. Ni uhusiano wetu na Mungu, uhusiano wetu hafifu mbele za Mungu unatufanya tusiwe na uhakika sana kwa yale tuliyomwomba.
Wakati mwingine tunaweza Kuvunjika moyo kutokana na yale tuliyomwomba kuchelewa kujibiwa, bila kufahamu Mungu huwa hachelewi. Bali Mungu hujibu kwa wakati wake sahihi, kwa maana ahadi zake ni za kweli.
Rejea: Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba. 2 Petro 3:9.
Wengine wanaweza kudhani Mungu anakawia hilo haliwezi kuondoa ukweli wa Mungu, Mungu akishasema amesema. Inabaki kwetu kuwa wavumilivu kwa yale tuliyomwomba atutendee, yapo yatatimia kwa wakati wake, na yapo utamwomba na kutupa pale pale.
Kama nilivyoanza kusema, mambo mengi au miujiza mingi ya Mungu, huwa tunaizuia wenyewe kutokana na imani zetu haba. Vile Watu wameona hilo jambo haliwezekani, na wewe unavunjika moyo kwa kujazwa hofu na wale wanaoona kutowezekana hilo ulimwomba Mungu akutendee/akusaidie.
Sijui unakabiliwa na nini katika maisha yako, amini ya kwamba, Mungu anaweza kukusaidia ukainuka tena. Haijalishi watu wamesema nini, uwe na uhakika Mungu anaweza kukusaidia na jina lake likatukuzwe kupitia hilo alilolitenda kwako.
Ikiwa Mungu aliweza kuifanya mifupa mikavu kuwa watu hai, hata kwako anaweza kulifufua lile lililokufa katika maisha yako likawa hai. Mazingira yasikusumbue, unapaswa kuliamini Neno la Mungu vile linakuelekeza.
Rejea: Akaniambia, Mwanadamu, je! Mifupa hii yaweza kuishi? Nami nikajibu, Ee Bwana MUNGU, wajua wewe. Akaniambia tena, Toa unabii juu ya mifupa hii, uiambie, Enyi mifupa mikavu, lisikieni neno la BWANA. Bwana MUNGU aiambia mifupa hii maneno haya; Tazama, nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi. Nami nitatia mishipa juu yenu, nami nitaleta nyama iwe juu yenu, na kuwafunika ngozi, na kutia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi BWANA. EZE. 37:3-6 SUV.
Inawezekana kabisa ndoa yako imesambaratika siku nyingi sasa zimepita, na katika mazingira ya kawaida kabisa watu wanaona haiwezekani tena kurejea kwa ndoa yako. Uwe na uhakika inaweza kurejea tena, ukiwa na imani mbele za Mungu, na ukiwa uhusiano wako na Mungu upo vizuri, cha msingi usichoke kumwomba Mungu.
Inawezekana kabisa tangu uingie kwenye ndoa yako, hujawahi kupata mtoto, uwe na uhakika mbele za Mungu Inawezekana kabisa kumpata mtoto. Haijalishi miaka mingi imepita ukiwa unatafuta mtoto, mwamini Mungu atakupa mtoto/watoto wazuri wakumpenda na kumtumikia Mungu.
Inawezekana kabisa umepoteza matumaini ya kuolewa, na ukiangalia umri umeenda sana, hilo lisikutoe kwenye uwepo wa Mungu. Tulia mbele za Mungu, na uendelee kutunza utakatifu wako mbele za Mungu, mume wako atakuja na utamfurahia kabisa, na hutojuta kwa chochote.
Haijalishi umekwama kwenye jambo gani, ikiwa Mungu aliifufua mifupa mikavu ikawa watu hai. Na kwako anaweza kuleta uhai kwa yale yaliyoonekana kufa katika maisha yako.
Nimesikia sana maneno kama yako, ndivyo akili yako inavyokukumbusha hivyo sasa, lakini amini nakwambia sikuelezi habari za kufikirika, wala za kusadikika. Nakueleza habari ambazo zimethibitishwa na Mungu mwenyewe kupitia Neno lake.
Rejea: Basi nikatabiri kama alivyoniamuru; pumzi ikawaingia, wakaishi, wakasimama kwa miguu yao, jeshi kubwa mno. EZE. 37:10 SUV.
Neno la Mungu linasema “wakasimama kwa miguu yao” Sijui kama unanielewa ninachosema hapa, waliosimama tena muda mchache uliopita ilikuwa mifupa mikavu. Ghafla historia ikabadilika na kuwa watu hai, tena likaonekana jeshi kubwa mno.
Mungu akalete uhai tena kwenye mambo yako yote yaliyoonekana mifupa mikavu, yawe mambo ya kiroho ama ya kimwili. Uhai ukaonekane sasa katika jina la Yesu Kristo aliye hai.
Mungu akubariki sana.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.