Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. [ Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.] Mk 11:25-26 SUV

Kama kuna jambo ambalo wengi wetu huwa hatulioni kuwa ni la muhimu, na wengi wetu hatulichukulii kwa uzito ni hili la kuhusu kusamehe au kutosamehe aliyekukosea. Hili tutazungumza sana kwa upande wa mahusiano.

Upande ambao tutazungumza sana na mahusiano ya vijana kabla ya kuingia kwenye ndoa, mada yetu itajikita sana hapo, hata kama tutagusa mahusiano ya ndoa kwa wale walioingia tayari itakuwa kwa kiasi kidogo sana.

Kusamehe ni jambo la muhimu sana, hili limebeba mambo mengi sana, kijana asipojua hili ataona kila kitu hakiendi, kumbe kilichomzuia ni kutosamehe yule aliyemshikilia moyoni mwake.

Wote tunajua usipomwachilia mtu huwa tunapitia maumivu mabaya sana hayo maumivu huwa yanachukua nafasi kubwa, na tusipoyatibu kwa kusamehe na kuachilia huwa yanazalisha mambo mabaya.

Tunaenda kuangalia madhara 5 ya kutosamehe mchumba/rafiki uliyempenda sana akakuacha;

  1. Unazuia Mungu Asikusaidie

Kama tulivyoanza kusoma mistari ya biblia hapo mwanzo, inatuonyesha msimamo wa Mungu ulivyo kwetu, ukisoma vizuri hayo maandiko utajua kwa mkristo ni lazima kusamehe ili mambo yake yaende vizuri.

Kusamehe kunafungulia mambo mengi sana kwa mwamini, linaweza lisiwe ni jambo jepesi sana kusemehe na kuachilia moyoni yule aliyekukosea, ila ni suala la muhimu sana kwa kila mkristo mwenye kupenda kuwa na mahusiano mazuri na Mungu kusamehe.

Kutokusamehe kunamzuia Mungu asikusaidie unapotaka akusaidie uondokane na maumivu ya kuachwa, na kuwa na mahusiano mapya, unaweza kuomba sana na usione matokeo ya maombi yako. Kumbe kinachokuzuia ni wewe kushindwa kusamehe yule aliyekuacha.

Kusamehe ni suala la lazima ukitaka kuwa na uhusiano mzuri na Mungu wako, haijalishi umekosewa nini na huyo aliyeakuacha, acha kinyongo naye, msamehe, utaona utakavyofunguka na kuwa huru ndani yako.

Unapoenda mbele za Mungu unakuwa unaona kitu cha tofauti sana, waombaji wanajua, kuna wakati unaomba lakini unajiona mkavu sana, au unakuwa unaona kuna ugumu sana. Na kuna wakati unakuwa unaomba na unaona kuna kitu kinatokea, kunakuwepo na ulaini Fulani unauona ndani yako.

Ukita kuona matokeo mazuri kwenye maombi yako ya kukutanisha na mtu wako sahihi wa kuishi naye, achilia yule uliyempenda na akakuacha katika mazingira ambayo hukupenda. Hata kama hajaja kukuomba msamaha, wewe msamehe.

2. Utachelewa Kupata Mtu Sahihi

Vizuri kuijua hii hata kama haina ladha sana kwenye masikio yetu, kutokusamehe kunachelewesha sana kupata mtu sahihi, kunaweza kukufungia kwenye chumba cha giza kinene kwa muda mrefu usipogundua haraka.

Anaweza akaja mtu sahihi akamwona sio wake kutokana na vitu vigumu vilivyokaa ndani ya moyo wake na akawa hataki kuachilia, maana kila mtu anakuwa anamwona ni mbaya kwake.

Kama hamwoni ni mbaya kunakuwepo na ukuta ambao hata yeye wakati mwingine anakuwa hajui kama yupo ndani ya huo ukuta, miaka inakuwa inaenda bila mafanikio ya kumpata yule anayemtaka.

Hapa ni muhimu kuelewa na kuchukua hatua ya kusamehe aliyempenda na akamwacha, hiyo ni njia sahihi ya kufungua mlango wa Mungu kumkutanisha na mtu wake sahihi kwa wakati sahihi.

3. Utakuwa Na Picha Mbaya Juu Ya Wanaume/Wanawake

Kutokusamehe kunajenga tabia moja ya ajabu sana ndani ya moyo wa kijana aliyeachwa na mtu wake aliyemwamini na kumpenda sana, wakati mwingine wengine huwa wanatoa gharama kubwa sana kwa wachumba wao.

Anapokuja kuachwa anakumbuka mengi aliyomfanyia huyo mchumba wake, hili tulilizungumza kwenye somo lililopita la kutohudumia mchumba kwa gharama nyingi maana ina madhara pale utakapoachwa.

Picha nyingi mbaya kwa vijana zinajengwa na kutosamehe, unakuta kijana ana mtazamo wa ajabu juu ya wanaume/wanawake kwa sababu aliwahi kufanyiwa jambo baya sana katika maisha yake.

Mbaya Zaidi iwe alifanyiwa Zaidi ya mara moja, ataona wote ni wale wale, unakuta yupo kanisani ila ana mtazamo mbaya sana juu ya wanaume/wanawake. Kumbe haipo hivyo na Mungu hatazami hivyo kama anavyotazama yeye.

Ili kuondoa mtazamo mbaya juu ya wanawake/wanaume ni vyema kusamehe, hili ni sharti gumu na rahisi pia, ukijua kwanini unapaswa kusamehe utachukua hatua kubwa hata kama unasikia ndani yako huwezi. Mwambie Yesu akusaidie, ukiamua atakusaidia na utakuwa huru.

Ukishaachilia tu ndani yako utaanza kuona na mtazamo mbaya juu ya wanawake/wanaume unaondoka kabisa na upendo wa Kristo unakuwa ndani yako kwa wingi. Upendo unapokuwa mwingi ndani yako utaweza kusaidiwa hitaji lako.

4. Kuogopa Kuingia Kwenye Mahusiano

Wapo wanaogopa kuingia kwenye mahusiano kwa sababu ya mitazamo mibaya, hii mitazamo mibaya inaweza kuchangiwa kwa kutokusamehe, hata kama ipo sababu nyingine. Sababu mojawapo inaweza ikawa kutokusamehe aliyemuacha.

Uoga mwingine huwa umesababishwa na hili la kutosamehe, anaanza kuona akiingia kwenye mahusiano tena atakutana na shida aliyokutana nayo kipindi cha nyuma. Kwa hiyo anaona njia salama ni kutojiingiza kwenye mahusiano rasmi.

Pamoja na wengine wamejenga uoga wanakuwa na mahusiano yanayomchukiza Mungu, anakuwa anaona bora kufanya uasherati na wanaume/wanawake kuliko kuingia kwenye mahusiano ya ndoa.

Ili kijana kuweza kushinda hii hali ni vyema kusamehe na kuachana na dhana potofu juu ya mahusiano, kufanya hivyo ile hofu iliyokuwepo ndani yake inakosa nguvu.

5. Kila Atakayekupenda Utaona Anaigiza

Hili linawakumba wengi na wengine wapo kwenye ndoa na waume zao au wake zao wanaonyesha kuwapenda ila wanawaona wanaigiza tu hakuna upendo wowote wanaouonyesha kwao. Mitazamo kama hii inakaa ndani ya mtu kwa muda mrefu na inakuwa tabia yake, hata anapoona watu wanapendana anaona wanaigiza.

Kilichomfanya kijana huyu aone hivyo ni kutosamehe, anakumbuka vile walipendana na msichana au mvulana Fulani alafu akaachwa au wakaachana, anaona wote wako hivyo. Shida hii inatokana na mambo mabaya aliyofanyiwa na mchumba/rafiki yake aliyepanga kuishi naye kwenye maisha ndoa.

Dawa ya hii ni kusamehe, kusamehe kunaondoa dhana potofu ndani ya mtu, ile kuona anayekupenda anaigiza itaondoka yenyewe, hapo ndipo utaanza kujua anayeigiza na mwenye upendo wa kweli ni yupi.

Tusamehe, na jua ilikuwa safari, na kubali kuwa lilikuwa darasa lako, hayo uliyofanyiwa ilikuwa somo kwako. Katika hilo somo utakuwa umeelewa mambo yapi hupaswi kufanya kwenye uchumba, na mengine utawasaidia walio nyuma yako.

Mwisho, hayo ndio madhara yanayoweza kukupata usiposamehe yule uliyempenda sana na akakuacha. Hakikisha unasamehe, hiyo ni tabia ya Kimungu kwa watoto wa Mungu.

Kama una changamoto yeyote au unahitaji kujifunza jambo Fulani kuhusu mahusiano, unaweza kutuandikia kwenye email; samsonaron0@gmail.com, au wasap +255759808081. Changamoto yako inaweza kuwa somo kwa wengine na ukawavusha mahali pale itakapokuwa Makala ya kujifunza.

Mungu akubariki sana.

Samson Ernest

+255759808081