Ndani ya biblia neno “kuwa na kiasi” limetajwa mara kadhaa (1 THE 5:6, TIT 2:6, 1 PET 1:13). Hii inaonyesha wazi tunapaswa kutofanya jambo pasipo kuwa na kiasi hadi likakuletea madhara, yanaweza yakawa madhara ya kimwili au kiroho. Hata Roho Mtakatifu hutufundisha kuwa na kiasi na yeye mwenyewe ni wa kiasi, katika kazi zako unapaswa kuwa na kiasi, vile vile katika huduma unapaswa kuwa na kiasi.
Nikiwa na maana unapaswa kuangalia mambo ya familia yako, kuwa bize muda wote na maombi au kuhubiri injili alafu ukaacha kujali watoto wako, mke wako au mume wako, nakwambia utakuta mambo yameharibika. Maana utakuwa umeacha mlango wazi wa adui kufanya anachotaka, utajikuta unaacha ulichokuwa unafanya na kuanza kutumia muda mwingi kufanya kesi ambazo ungeziepuka kama ungekuwa na balasi kwenye utendaji wako.
Hata katika mahusiano yetu na watu wa jinsia nyingine, kama wewe ni mwanaume alafu ukawa na ukaribu na mabinti au wake za watu kupita kiasi, uwe na uhakika unajitafutia kashfa mbaya. Inawezakana kabisa huna mahusiano nao ya kimapenzi, ila kutokana na ukaribu wako ukapewa kashfa ya kutembea nao kimapenzi.
Vile vile kwa mwanamke unaweza ukawa huna mahusiano ya kimapenzi na mwanaume yeyote wa nje ya ndoa yako kama umeolewa, na kama hujaolewa inawezekana huna mahusiano ya kimapenzi na mwanaume yeyote. Ila kutokana na ukaribu mkubwa ulionao na wanaume hadi wengine mmepeana majina ya utani uliopita kiasi ujue unajitengenezea kashfa mbaya kwa ndugu au jamii.
Kama nilivyotangulia kusema hapo mwanzo, kuwa na kiasi ni jambo la msingi sana, upendo wa ndugu au marafiki unapaswa kuwa na kiasi, kama utakosa kiasi unajitafutia matatizo na utaona watu wana maneno ya uchonganishi au wana wivu na wewe.
Mbaya Zaidi unaweza ukawa na mahusiano mazuri na mwanamke/mwanaume wa nje ila mke/mume wako hakumbuki mara ya mwisho kuonyesha huo upendo unaouonyesha huko nje ilikuwa lini. Inawezekana hata mawasiliano yako kwenye simu na wanaume/wanawake wengine wa nje ni mazuri sana kupita yale ya mume/mke wako.
Mambo kama haya unayasababisha mwenyewe na baadaye utaanza kumsingizia shetani, maana huyohuyo mume/mke wako ataanza kukufikiria vibaya kutokana na hali anayokuona nayo. Usipokuwa na uelewa utaona ana mawazo potofu, elewa sio kana kwamba ana mawazo potofu ila wewe ndio unasababisha hayo yatokee.
Kwa kuwa mna ukaribu sana na wanaume/wanawake wengine, mnaweza mkawa mnaenda mahali kupata chakula wakati mwingine mnajitenga na kuwa na sehemu yenu maalumu, alafu wewe huyo huyo hukumbuki ulifanya hivyo kwa mke/mume wako lini. Unafikiri jamii inayokuzunguka itakufikiriaje ukilinganisha na dunia ya sasa ilivyochafuka.
Unafikiri mchumba wako atakufikiria vipi kutokana na ukaribu uliopitiliza na wadada/wakaka wengine alafu kwake haoni huo ukaribu na upendo unaouonyesha kwa wengine. Huoni unaweza kupeperusha ndege wako mzuri kwa sababu ya matendo yako yasiyofaa mbele ya macho ya watu?
Sisi ni barua inayosomwa na kila mtu, hasa sisi tuliokoka tunafuatiliwa mno na watu, kuanzia mtaani kwako, kazini kwako, shuleni kwako, na popote unapokuwepo watu wanakufuatilia yale unayofanya na unayozungumza. Hata kwenye mitandao ya kijamii kila unachokifanya kuna watu wanakufuatilia njia zako.
Ninyi ndinyi barua yetu, iliyoandikwa mioyoni mwetu, inajulikana na kusomwa na watu wote; 2 Kor 3:2 SUV.
Unaweza kuona vile ulivyo kioo, hadi wale wanashirika wenzako wanalo jukumu la kukuangalia, wakiona jambo lisilokuwa zuri kwako watasema, utasema kwanini wanafuatilia maisha yangu, ukianza kusema hivyo ujue umejisahau kuwa wewe ni barua inayosomwa na kila mtu.
Ikiwa ni barua inayosomwa na kila mtu, tunapaswa kuhahakisha barua yetu inasomeka vizuri kila siku, kila mtu anapotaka kuisoma pasiwepo na maandishi yaliyofutika na yanaonekana yana ujumbe muhimu. Hakikisha ushuhuda wako unautunza kwa gharama yeyote, usijifanye wewe ni mtu wa watu alafu ukaharibu ushuhuda wako.
Ninapoenda kuhitimisha somo hili ninakuasa uwe makini, kuwa na kiasi, acha mazoea ya kupita kiasi na watu wa jinsia tofauti na yako, ikiwezekana na wa jinsia yako uwe na kiasi nao, unaweza kupewa kashfa mbaya. Hasa wale marafiki ambao wanajulikana wana tabia chafu za ushoga au usagaji, uwe makini nao, hatupaswi kuwatenga ila tunapaswa kutumia akili alizotupa Mungu kuishi nao bila kutuchafua.
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081