Haleluya, nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, wakati mwingine tena Mungu ametupa kibali cha kuifikia siku ya leo. Tuna kila sababu za kumtukuza yeye kwa matendo yake makuu kwetu maana zipo changamoto ngumu sana tunakutana nazo kiasi kwamba tunafika wakati tunajisikia kuchoka, lakini yeye hututia nguvu za kushinda na kuweza kusonga mbele.

Akili/ufahamu wako unatoka ndani ya moyo wako, kila wazo unaloliona kwako fahamu kwamba linatoka ndani ya moyo wako. Kiwe kizuri au kibaya kinatoka ndani ya moyo wako, moyo ndio mashine inayozalisha kila kitu kinachotokea katika matendo yako ya mwili wako.

Ujuzi wowote ulionao umetokana na moyo wako, moyo wako umebeba akili/ufahamu wako.

Rejea; Amewajaza watu hao akili za moyoni, ili watumike katika kazi kila aina, ya mwenye kuchora mawe, na kazi ya werevu, na ya mwenye kutia taraza, katika nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri, na ya mwenye kufuma nguo; ya hao wafanyao kazi yo yote, na ya wenye kuvumbua kazi za werevu. Kutoka 35:35 SUV.

Kila mmoja unayemwona anaonekana ana akili nyingi sana jua kwamba zinatoka ndani ya moyo wake, kila ovu/baya unaloliona linafanywa na mtu/watu elewa uharibifu ulianza ndani ya moyo wake.

Mtu kushindwa kuelewa Neno la Mungu inakuja pale ufahamu/akili zake zinapokuwa zimefungwa ndani ya moyo wake.

Rejea; Kwani mioyo yao imeificha ufahamu; Kwa hiyo hutawakuza. AYUBU. 17:4 SUV.

Hekima au busara za mtu zinatoka ndani ya moyo wake,

Rejea; Wafalme wote wa duniani wakamtafuta Sulemani uso wake, ili waisikie hekima yake, Mungu aliyomtia moyoni. 2 Nyakati 9:23 SUV.

Vilevile upumbavu wa mtu hutoka ndani ya moyo wake,

Rejea; Mpumbavu amesema moyoni, Hakuna Mungu; Wameharibu matendo yao na kuyafanya chukizo, Hakuna atendaye mema. Zaburi 14:1 SUV.

Watu kumkataa Bwana wetu Yesu Kristo na wengine kumkataa katika roho na kweli, na kufuata njia zao mbaya, hii ni kufungwa ndani ya mioyo yao wasiweze kulielewa hili.

Rejea; Katika kukosa na kumkana Bwana, na katika kugeuka tusimfuate Mungu wetu, tukinena jeuri na uasi, na kukusudia maneno ya uongo na kuyatoa moyoni. Isaya 59:13 SUV.

Nimejaribu kukupa maandiko mengi Matakatifu yanayoonyesha ufahamu/akili zinavyotoka ndani mioyo yetu.

Huenda hukujua chanzo cha akili/ufahamu wa mtu unatoka wapi, kupitia hayo maandiko utakuwa umeelewa vizuri akili/ufahamu wako upo ndani ya moyo wako.

Matokeo mengi mabaya unayoona leo ni kwa sababu ya moyo wa mtu hukuwa na akili/ufahamu mzuri wa kutenda jambo lililo sahihi kufanya.

Huu ni ugonjwa mbaya sana unaotesa kanisa la leo na taifa kwa ujumla, wengi mioyo yetu imefungwa katika dini/madhehebu yetu. Tumeshindwa kuenenda kama Mungu anavyotutaka kuenenda kwa sababu tu mioyo yetu imefungamana na dini.

Wengi wameenda kutafuta msaada kwa waganga wa kienyeji, mioyo yao ikafungwa huko huko pasipo wao kuelewa.

Unaposikia mtume/nabii/mchungaji wa uongo, na bado unaona watu wanamkimbilia na kumfuata. Elewa mioyo yao imefungwa wasipate ufahamu/akili za kutambua huyo sio mtenda kazi wa Mungu.

Wengi wetu tumeshindwa kumfahamu Mungu wetu vizuri kwa sababu mioyo yetu imefungwa na shetani tusiweze kujua mambo mengi ya Mungu. Ndio maana leo mtu anasema ameokoka lakini bado mlevi, mzinzi, mwizi na mengine mengi mabaya.

Wengi wamekufa na vipawa/vipaji vyao pasipo kuvifanyia kazi, kwa sababu ndani ya mioyo yao walifungwa fahamu/akili zao.

Jambo la msingi kwako kulizingatia hapa ni kuomba Mungu juu ya fahamu/akili zako, mwambie Mungu afungue moyo wako ili uweze kufikiri vyema.

Moyo wako ukifunguliwa yapo mengi sana utaweza kuyajua na kuyatendea kazi, umeona mtu anaenda ndivyo sivyo ombea ufahamu/akili zake zitokazo ndani ya moyo wake.

Ili usimtende Mungu dhambi unapaswa kumjua vizuri kwa kuliweka Neno lake moyoni mwako kwa wingi, moyoni ndipo panatoka mawazo mazuri au mabaya, ndipo panatoka akili/fahamu nzuri au mbaya.

Rejea; Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi. Zaburi 119:11 SUV.

Kuanzia sasa jifunze kuomba Mungu afungue moyo wako, huenda hapo ulipo unajiona unaelewa vizuri maandiko Matakatifu kumbe ufahamu wako umefungwa kama rafiki zake na Ayubu.

Walikuwa wanamweleza vitu ambavyo walijua Ayubu atakuwa ametenda dhambi mbele za Mungu, kumbe ufahamu wao ulikuwa umefungwa wasiweze kuelewa juu ya jaribu alilokuwa analipitia Ayubu.

Rejea; Kwani mioyo yao imeificha ufahamu; Kwa hiyo hutawakuza. AYUBU. 17:4 SUV

Hebu jiulize ufahamu/akili zako zipo salama, utajuaje fahamu/akili zako zipo sawa na wakati moyo wako umefungwa? Ni kwa kuamua kumkimbilia Mungu kumaanisha.

Madhara ni makubwa sana, ndio maana leo hii matokeo mengi mabovu katika maisha yetu ni kwa sababu mioyo yetu ilikuwa imefungwa. Inaweza kabisa ilifungwa na shetani mwenyewe na uwezekano upo imefungwa kwa ujinga wetu wa kutokuwa na mahusiano mazuri na Mungu wetu.

Mungu akusaidie uweze kuelewa hili jambo, moyo wako ukafunguliwe uweze kujua mengi ambayo hukujua hapo kabla ili Mungu aweze kutukuzwa kupitia wewe.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.