Haleluya,

Wakati wa sodoma na Gomora, Mungu hakuangamiza hiyo miji mpaka alipohakikisha amewaondoa wenye haki wake kwanza wanaolitukuza jina lake.

Mahali alipo mtu anayemwabudu Mungu katika roho na kweli, kuwepo kwake inamfanya Mungu atukuzwe mahali pale. Hata kama inaonekana mahali pale watu wanatenda dhambi sana, kwa uwepo wa mwenye haki wa Mungu, inamfanya Mungu aone kutukuzwa mahali pale.

Eneo ambalo halina wakristo wanaomcha Mungu katika roho na kweli angalia ukuaji wake wa maendeleo. Utaona upo chini sana, na kama upo juu asilimia kubwa utaona wana mali zisizo halali, na zisizo na misingi ya kiMungu ndani yake.

Uliyeokoka unaweza kuwepo mahali ambapo wanamtenda Mungu dhambi sana, ila kwa uwepo wako ukafanya watu wengi sana wakamjua Mungu.

Uwepo wako mahali unaweza kusababisha eneo hilo likawa na hali ya hewa nzuri ya kiroho, unaweza kufika mahali walikuwa wanasumbuliwa sana na nguvu za giza. Ila kuwepo kwako siku hiyo, watu wa eneo lile wanaweza kulala kwa raha sana siku hiyo.

Mwana wa Mungu atambulika mahali popote pale akiingia, nguvu za giza zinajua kabisa hapa leo tumeingiliwa. Na haziwezi kukaa mahali pale, zitaondoka tu.

Kadri wenye haki wanavyozidi kuongezeka mahali, uwe na uhakika mahali pale patakuwa na baraka za Mungu za kutosha. Kama ni mafanikio ya kimwili utaona watu wa Mungu watazidi kufanikiwa.

Utaona mazao yakilimwa na kustawi vizuri sana, na utashangaa mahali pengine mazao yakiwa yamekauka. Mvua ni ile ile na sehemu ni ile ile, pamoja na hayo ujue uhusiano mbaya/mzuri na Mungu ndio unaleta hayo yote.

Rejea: Mji hutukuzwa kwa mbaraka wa mwenye haki; Bali mji hupinduliwa kwa kinywa cha mwovu. MIT. 11:11 SUV

Amini uwepo wako mahali popote pale hata kama hakuna mkristo hata mmoja, ukawepo wewe mmoja tu, uwe na uhakika mahali pale Mungu aliye hai atatukuzwa tu.

Hata uwepo wako kwenye mitandao ya kijamii, unamfanya Mungu atukuzwe kupitia mafundisho yako mbalimbali unayotoa.

Kupitia shuhuda zako mbalimbali, unamfanya Yesu Kristo atukuzwe hata na wale wanaolikataa jina lake kuu.

Mungu akusaidie kutambua mahali popote unapokuwepo, una nafasi kubwa ya kubadilisha mazingira yale kiroho.

Mungu akubariki kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu
chapeo@chapeotz.com
www.chapeotz.com
+255759808081.