Tunapojifunza Biblia tunaona jinsi Yesu mwenyewe wakati ametoka kwenye maombi ya siku arobaini, tunaona jinsi Shetani alikuja na kumjaribu.
Pamoja na yale maombi ya siku arobaini hayakuweza kuzuia majaribu yasimkute Yesu, lakini ni kwa sababu kazi ya majaribu ni kumuimarisha mtu, ndio maana huwezi kuyazuia yasije kwako.
Kuna shuhuda nyingi tu watumishi wa Mungu wanashuhudia jinsi wanavyopita kwenye majaribu makubwa, na Mungu amewawezesha kushinda.
Yamkini upo umesimama vizuri na Mungu, lakini unashangaa majaribu kwako hayaishi, tena ndiyo yanazidi kuja mazito na makubwa, usiogope maana unafanywa kuwa imara na kujengewe misuli ya imani ndani yako.
Tunajifunza maandiko pia tunamuona Eliya, tunaweza kuona jinsi Mungu alivyomtumia kwa matendo makuu mpaka Israeli wakajua kwa hakika Mungu wa Eliya ndiye Mungu aliye hai.
Basi, Ahabu akamwambia Yezebeli habari ya mambo yote aliyoyafanya Eliya, na jinsi alivyowaua manabii wote kwa upanga.
1FAL 19:1
Eliya alikuwa na nabii ambaye aliomba mbingu zikafungwa mvua haikunyesha katika nchi, lakini pia katikati ya mabaali na manabii wake, alimdhihirisha Mungu aliye hai, aliomba moto ukashuka na ukuiteketeza ile sadaka.
Lakini baada ya hapo tunaona majaribu yakiinuka juu yake, hayakuogopa ni kwa namna gani Mungu amemtumia kwa matendo makuu.
2 Ndipo Yezebeli akampelekea Eliya mjumbe, kusema, Miungu wanifanyie hivyo na kuzidi, nisipokufanya roho yako kesho, panapo wakati huu, kama roho ya mmojawapo wa hao.
3 Naye alipoona hayo, aliondoka, akaenda aihifadhi roho yake, akafika Beer-sheba, mji wa Yuda, akamwacha mtumishi wake huko.
1FAL 19:2-3
Yezebeli akainuka ili kutishia maisha yake, tunaona kilichotokea Eliya alikimbia aihifadhi roho yake, kwa nini kwa sababu majaribu kazi yake ni kukuimarisha.
Wakati wa majaribu ni wakati ambao unabaki peke yako, hata Yesu wakati wa kujaribiwa alikuwa peke yake, hata wakati wakati wa kuteswa kwake, alibaki peke yake.
Tunamuona hata Eliya ilifika wakati akamuacha mtumishi wake na akabaki peke yake, hivyo tunaweza kuona ni jinsi gani wakati huo kama mtumishi wa Mungu unapaswa kutambua kwamba unapita mahali pakukuimarishwa.
Usichoke na kukata tamaa, tambua kwamba Mungu anapokutazama anatamani kuona ulishinda, anatamani kukuona unasonga mbele.
Mungu akikutazama anatamani akuona ukiinuka na kujitia nguvu huku ukiendelea na safari, usikate tamaa wala usiendelee kukaa hapo, inuka.
Inuka maana safari bado ni ndefu, inuka ukalitimize kusudi la Mungu, haupo peke yako unaye Roho Mtakatifu ndani yako, hivyo tambua kwamba wewe ni mshindi.
Mungu akubariki sana.
By Rebecca Ernest