Miongoni mwa vitu vya kulinda siku zote katika maisha yetu ya kila siku ni kiburi, wengi sana wamerudi chini ghafla kihuduma, kwa sababu ya kujaa kiburi baada ya kufanikiwa kihuduma.

Wengi sana wameshindwa kuendelea kudumu na mafanikio yao makubwa waliyofikia baada ya kuinuka kiburi ndani yao.

Waswahili wanasema, ukitaka kujua tabia ya mtu vizuri, mtu huyo apate pesa za kutosha, yaani kula kwake chakula anachokitaka iwe sio shida, kutembelea gari analolitaka kwa pesa zake iwe sio shida, kuishi nyumba za kupanga awe ameshasahau kabisa. Maana yeye mwenyewe tayari anapangisha nyumba, tena sio moja ni nyingi.

Mtu akishafikia kiwango hichi ndio unaweza kujua alivyo, maana kuna watu ni wakarimu sana, kwa sababu hawana kitu mfukoni. Unaweza kudhania ni wakarimu kumbe ni unyonge wa umaskini/fukra ndani yao.

Ukitaka kujua alivyo mtu, apate cheo kikubwa , awe na amri, na mamlaka ya kufanya chochote anachofikiri kwake ni sahihi. Hapo ndipo utamwelewa vizuri huyo mtu ana tabia gani, maana anao uhuru wa kutosha.

Mtu mwingine unaweza kumwona ni kiongozi mzuri, kwa sababu yupo chini, siku akipata nafasi ya juu kabisa. Awe na mamlaka makubwa, ambapo hakuna zaidi yake juu, utaona uhalisia wa tabia yake.

Wapo leo watu wanamtafuta Mungu kwa bidii sana, kwa sababu wana uhitaji fulani mbele za Mungu. Siku akifanikiwa hilo jambo, na Mungu anamsahau kabisa na ile bidii yake mbele za Mungu inatoweka kabisa.

Mtu alikuwa anampenda sana Mungu akiwa ana shida ya mtoto, bidii yake ya ibada ilikuwa kubwa sana. Baada ya kupata mtoto, ile bidii ilitoweka kabisa.

Huo ni upande wa bidii, tukirudi katika upande wa aliyekuwa chini baada ya kuinuliwa juu na Mungu. Alianza kujiinua mwenyewe badala ya kumwinua Mungu aliye juu.

Kuna watu ni wanyenyekevu mbele za Mungu ila ukweli ni kwamba, bado wapo kwenye hatua fulani ambayo bado hawajajulikana kihuduma. Siku amejulikana hata na mtoto wa shule ya awali, utamwona akianza kuinua mabega juu.

Hili ndilo lililowakumba Moabu, waliinuka kiburi kingi na jeuri ya kutosha, na majivuno ya mengi. Ikamfanya Mungu kukasirika kwa ajili ya hayo.

Rejea: Tumesikia habari za kiburi cha Moabu; Ya kuwa ana kiburi kingi; Jeuri yake, na kiburi chake, na majivuno yake, Na jinsi alivyotakabari moyoni mwake. Najua ghadhabu yake, asema BWANA, ya kuwa si kitu; majisifu yake hayakutenda neno lo lote. YER. 48:29‭-‬30 SUV.

Mungu anapokubariki endelea kunyenyekea chini ya mkono wake, usije ukajiinua na kuanza kujitwalia utukufu wake. Hautofika mbali ndugu, utakwama haraka sana, na kushushwa chini.

Kiburi hakifai katika mafanikio uliyopata, Mungu amekupa ili umtumikie yeye, unapojiinua kwa kitu alichokupa Mungu. Unakuwa unajitafutia laana mbele za Mungu.

Rejea: Na Moabu ataangamizwa, asiwe taifa tena, kwa sababu alijitukuza juu ya BWANA. Hofu, na shimo, na mtego, zaja juu yako, Ee mwenyeji wa Moabu, asema BWANA. YER. 48:42‭-‬43 SUV.

Vizuri kujua hili, kadri unavyozidi kufanikiwa kihuduma, hakikisha unaongeza kiwango chako cha kuwa karibu zaidi na Mungu wako. Kuwa mtu wa kusoma Neno lake, na kuwa mtu wa maombi sana, tena ya kufunga.

Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
WhatsApp: +255759808081