Ukiwa kama kijana wa kike au kiume na uliwahi kufanya makosa huko nyuma ukajiingiza kwenye mahusiano ambayo yalikupa maumivu na yakaharibika, wakati mwingine ukiwaza kuingia kwenye mahusiano mengine unajiona utakutana na yale yale.

Wakati mwingine unataka kufanya maamuzi ya kuwa na mtu mwingine ambaye unataka kuanza safari ya kuingia kwenye ndoa, lakini unasita sita kwa kufikiri huenda yakawa yale yale yaliyokutokea huko nyuma.

Makosa yapo, tena unaweza kujeruhiwa haswa, ukiwa binti unaweza ukawa uliingia kwenye mahusiano na mwanaume ambaye hakuwa na subira akawa amekupa mtoto kabla ya ndoa na akakuachia mtoto hapo.

Zipo sababu nyingi, wengine walivyoona wamepata mtoto kabla ya kufunga ndoa walikimbia, wapo watoto hawawajui baba zao, sio kana kwamba wamekufa ila walikimbia kukwepa aibu, wakawaacha wenzao hapo.

Miaka imepita baada ya mtu kutokewa na tukio kama hilo, alilia sana na kujiapiza kila aina ya viapo ila baadaye Mungu aliwasaidia na wakaachilia yote yaliyowatokea. Sasa wanaona wanapaswa kuingia kwenye ndoa na mwanaume/mwanamke sahihi.

Wapo wengine waliachwa na wenzao wiki moja au siku mbili au tatu kabla ya harusi yao, kitendo hicho kiliwaumiza na kuwafanya kuwa katika hali sio nzuri, kwa kuwa Mungu ni mwema miaka ilivyoenda ameachilia neema juu yao na sasa wanataka kuingia kwenye ndoa.

Wengine walikutana na shida ya mahusiano wakiwa shuleni, walikatisha masomo yao kwa kukimbia mimba na waliokimbiwa waliachiwa jukumu la kulea, na waliowakimbia hawakurudi kuja kuendeleza maisha yale waliyoanza mapema.

Sasa wamekuwa watu wazima sasa, kama ni mtoto amekuwa mkubwa, huenda na shule ameshaanza, anahitaji sasa kuwa mke wa mtu, mtu wa namna hii anahitaji umakini ili asirudie kosa alilolifanya huko nyuma.

Kukosea kila mtu anaweza kukosea kwenye maeneo tofauti sio lazima kwenye mahusiano tu, ikiwa ulikosea kwenye mahusiano na ukapita kwenye maumivu makali kwa namna yeyote ile iliyokutokea iwe kwa kuachana au kuachwa. Unapaswa kufahamu hiyo ilikuwa shule yako ya kujifunza, unapaswa uwe umefaulu vizuri.

Zingatia mambo 5 yafuatayo;

1. Usiendeshwe na mihemko

Unapaswa kukomaa kiakili na kiroho, usijiingize haraka kwenye mahusiano na mtu ambaye hujamfahamu vizuri, kisa amekuambia anakupenda unaona ndio huyo huyo, na kisa umemwona ni mzuri na anakuheshimu unaamua kuingia naye kwenye uchumba.

Usiwe na haraka, omba Mungu, usiwe na hofu ykupita kiasi ila ukimshirikisha Mungu na ukawa huna mihemko ya kutaka awe mke au mume wako haraka haraka, Mungu atakusaidia na utakuwa salama.

2. Usijishushe thamani yako

Hii inaweza kuwakumba hasa mabinti au wanawake, kwakuwa alipata mtoto kabla ya ndoa na akawa ameachwa, anajiona kwa mtazamo wa tofauti kabisa hasa jamii zetu za kiafrika ndio zinamfanya ajidharau Zaidi.

Wewe ni mtu wa thamani sana mbele za Mungu, hata kama kuna watu wanakulinganisha kama nguo ya mtumba, wewe ni mtu sio nguo, na Yesu alikufia msalabani, kama ulitubu Yesu amekusamehe na unapaswa kupata mtu sahihi wa kuishi na wewe.

3. Usiseme yeyote atakayekuja mbele yangu nitamchukua au nitachukuliwa naye

Wewe sio mnyama asiye na maamuzi ya kufanya, hupaswi kujirahisha kwa mtu yeyote, nimetangulia kukuambia wewe ni wa thamani mbele za Mungu haijalishi sisi wengine tunakuonaje. Kazi yako ni kutulia na kutunza maisha yako mbele za Mungu.

Kwenda kujitupia kwa mwanamke au mwanaume yeyote kisa huko nyuma uliumizwa kwenye mahusiano, unaweza kujiingiza kwenye maumivu mengine makubwa Zaidi.

4. Jithamini na jipende sana

Ukijielewa wewe ni wa thamani mbele za Mungu utaacha kujidharau kwa namna yeyote ile, haijalishi mazingira yanakuonaje, ukijithamini maana yake utajipenda, ukifanya hivyo utailazimisha jamii ikuone kwa namna ya tofauti.

Watakuheshimu na kukuona ni mtu wa maana, mtu asiyependa upuuzi, yale ya nyuma yatabaki simulizi ila watajua wewe sio yule wa miaka kadhaa iliyopita.

5. Samehe na achilia yote yaliyokupata nyuma

Usidumu wala usiingie na uchungu kwenye mahusiano mapya, hii inaweza kukusababishia madhara makubwa sana, Mungu anaweza asiwepo kwenye uchaguzi wako, ukajikuta unarudia yale yale tena kwa namna nyingine.

Usitembee na uchungu wa kutosamehe yule aliyekutenda mabaya kwenye mahusiano yenu, awe alikufanya nini, achana na hayo mambo ya nyuma na usamehe.

Ukifanya haya na ukayazingatia sawa sawa hutaweza kurudia kosa lile lile, utakuwa na ndoa nzuri sana, ndoa ambayo itakuwa faraja katika maisha yako yote.

Karibu kwenye kundi la wasap la kusoma biblia na kutafakari, wasaliana nasi kwa wasap +255759808081, hii itakufanya ukue kiroho, ukikua kiroho hata maamuzi yako yanakuwa sawa.

Mungu akubariki sana

Samson Ernest

+255759808081