
Kama tunaweza kutaja maeneo magumu katika maisha ya mwanadamu, mojawapo linaweza kuwa eneo la kutoa maamzi ya haki.
Kwanini kunakuwa na ugumu katika hili? Unaweza kukutana na kesi ya mtu wako wa karibu sana na mtu mwingine ambaye sio wa karibu yako sana. Yaani hamna ule ukaribu naye sana.
Anaweza akawa ni mzazi/mlezi wako, anaweza akawa ni mtoto wako, anaweza akawa ni rafiki yako, anaweza akawa ni mume/mke wako.
Ikija kesi mezani ambayo wewe kama kiongozi au mtumishi wa Mungu unapaswa kuiamua, na ili uiamue vizuri hiyo kesi unapaswa kutenda haki kwa kila mmoja wao.
Ukitaka kuamua vizuri, na ukitaka kuwa na sifa za mtu wa haki, hupaswi kufanya yafutayo;
1. Usipotoshe.
Hili ni la muhimu sana kuzingatia unapokuwa kwenye nafasi ya mwamzi wa kesi yeyote ile, hupaswi kuwa ni mmoja wa wawapotoshaji ili umtetee asiyestahili na kumwingiza hatiani asiyehusika huku ukijua hilo.
2. Usipendelee.
Zipo kesi ngumu hasa zile ambazo zinahusiana na watu unaowafahamu kwa ukaribu sana, anaweza akawa moja ya watu walioshitakiana mmojawapo ni rafiki yako wa karibu.
Usipokuwa makini utamwingiza hatiani asiyehusika na anayehusika utamwacha anaendelea vizuri. Kufanya hivyo utakuwa umemuumiza asiyehusika na utakuwa hujatenda haki.
3. Usipokee Rushwa.
Miongoni mwa vitu ambavyo vinatia upofu kwa watu ni rushwa, rushwa ni hatari sana kwa watu ambao wana misimamo ya kutenda haki.
Ukijidanganya uipokee na kufikiri utafanya unavyoona wewe mwenyewe, uwe na uhakika utafanya kama ilivyokusudiwa ufanye.
Unaweza kutoa maamzi ya kijinga sana yakamuumiza asiye na hatia kutokana na kupokea rushwa.
Haya yote ninayokueleza hapa sio maneno yangu, ndivyo neno la Mungu linavyotuelekeza tusifanye hayo tunapotaka kuwa watoa maamzi wazuri au watenda haki wazuri.
Rejea: Usipotoe maamuzi; wala usipendelee uso wa mtu; wala usitwae rushwa; kwa kuwa rushwa hupofusha macho ya wenye akili, na kugeuza daawa ya wenye haki. KUM. 16:19 SUV.
Umeona huo mstari, unatuweka wazi kabisa, ukitaka kuwa mpatananishi mzuri, ukitaka kuwa mwamzi mzuri wa watu, hakikisha hufanyi hayo mambo matatu hapo juu.
Kutokufanya hivyo utakuwa kiongozi mzuri sana asiyekandamiza mtu yeyote, mwanzo watu hawatakupenda sana ila itafika mahali watakuelewa na kukupenda.
Na hata wakitokea wapo hawakupendi ujue ni jambo la kawaida, lakini uwe mtu ambaye haangalii watu usoni. Ukiwa hivyo watu wataheshimu sana maamzi yako, maana wanajua huwa huangalii ukaribu wako na mtu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com