Kwanza unapaswa kufahamu Mungu wetu ni mwaminifu sana, kwanini nasema ni mwaminifu? Lile ambalo umemwomba atakupa.
Ukiomba na ukiamini uwe na uhakika Mungu anaweza kukujibu maombi yako, bila kujalisha hilo jambo lina ukubwa gani.
Katika kujibiwa huwa kunaleta faraja, huwa kunaleta furaha, huwa mtu anakuwa na ushuhuda mkubwa sana wa kuwashirikisha wengine.
Pamoja na kujibiwa mtu hitaji la moyo wake, wengi huwa tunafikiri imetosha. Tunabaki kufurahia majibu na wakati mwingine kujisahau na kurudi katika maisha ya kawaida.
Kawaida vipi? Wapo watu baada ya kupata haja ya mioyo yao, hata ile bidii mbele za Mungu huwa inashuka chini kwa kiwango kikubwa sana.
Ile kujali mambo ya Mungu inakuwa sio sana kama wakati ni muhitaji, anabaki wa kawaida sana hadi kufikia kiwango cha kuanza kufanya mambo yasiyompendeza Mungu.
Kama nilivyotangulia kusema hapo awali, Mungu wetu anaweza kusikia maombi yetu na akatupa haja ya mioyo yetu. Kama tunavyoona kwa Suleiman kwenye mstari huu;
Rejea: BWANA akamwambia, Nimeyasikia maombi yako na dua zako, ulizotoa mbele zangu. Nimeitakasa nyumba hii uliyoijenga ili niweke jina langu humo milele; tena macho yangu na moyo wangu utakuwapo hapo siku zote.1 FAL. 9:3 SUV.
Katika kujibiwa kwetu huwa kuna faida zaidi tutakayopata kama tutaendelea kuenenda katika njia za Bwana.
Hili tunaweza tusiwe tunalijua sana ila tunapaswa kufahamu kuwa lipo, ndio maana unaweza kumwona mtu ametoa ushuhuda wa kutendewa jambo fulani na Mungu.
Baadaye kadri siku zinavyozidi kwenda unakuja kumwona anastawi zaidi kwenye maeneo mbalimbali kwenye maisha yake. Usipojua siri ni nini unaweza ukaanza kufikiri kuna watu wana bahati zao.
Ukweli ni huu, tunapomwomba Mungu akatujibu kile tulimwomba, anatupa zaidi kile ambacho hatukumwomba, anatufanya imara zaidi kwenye maeneo mbalimbali tunayomtumikia katika maisha yetu.
Mungu anatuthibitishia hili kupitia maandiko matakatifu, anamwahidi jambo mfalme Suleiman baada ya kumjibu maombi yake.
Rejea: Na wewe, ukienda mbele zangu kama alivyokwenda Daudi, baba yako, kwa ukamilifu wa moyo, na kwa adili, kufanya hayo yote niliyokuamuru, na kuzishika sheria zangu na hukumu zangu, ndipo nitakapokifanya imara kiti cha ufalme wako juu ya Israeli milele; kama nilivyomwahidia Daudi, baba yako, nikisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Israeli. 1 FAL. 9:4-5 SUV.
Hii pia inatufundisha kwamba zipo ahadi za Mungu ambazo zinahitaji kuenenda katika njia zake ndipo atupe/atutendee yale ametuahidia.
Tupaswa kuenenda katika njia za Bwana ili tuweze kupokea ahadi za Mungu alizotuahidia kupitia neno lake. Kutenda mapenzi ya Mungu, na utakatifu wako utakusababishia Mungu akupe kile amekuahidia kupitia neno lake.
Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
www.chapeotz.com
+255759808081