Nakusalimu katika jina la Bwana wetu YESU Kristo aliye hai, habari za muda huu ndugu yangu katika Kristo.

Napenda kukushirikisha mambo machache, naamini kupitia huu ujumbe utaenda kupata kitu kizuri cha kufanyia kazi katika maisha yako ya kiroho.

Najua kila mmoja wetu aliyeokoka huomba, haijalishi anaombaje ila nafahamu kila mmoja wetu huwa ana utaratibu wa kumwomba Mungu.

Kuomba kwetu huku huenda kumeshindwa kuzaa matunda huenda kwa sababu ambazo zipo ndani ya uwezo wetu, na tumeshindwa kuepukana nazo. Ili Mungu aweze kutujibu maombi yetu tuliyoomba kwake.

Tunajua Mungu hapendi dhambi, na tunaelewa tunapoenda mbele za Mungu tunapaswa kutubu na kujitakasa kwa damu ya Yesu Kristo. Tunapoenda mbele za MUNGU kwa unyenyekevu kuomba, hatupaswi kurudia dhambi baada ya kuomba.

Sasa unakuta mtu anaomba Mungu amsaidie hitaji fulani, lakini hayupo tayari kuachana na dhambi zake anazofanya. Huko ni kujidanganya ndugu yangu, ikiwa hatuacha maovu yetu, tusitegemee Mungu atutendee vile tunataka sisi, ila hatutaki kufuata maagizo yake.

Sikuambii uanze kuongopa kwenda mbele za Mungu kwa sababu umetenda dhambi, nenda mbele za Mungu kutubu na akusafishe kwa damu ya Yesu. Kwa kumaanisha kuachana na maovu yanayokutenga na uso wa Mungu.

Mfano kaka/dada anaomba Mungu ampe mume/mke mwema atakayemfaa, wakati huohuo afanya uasherati na wanaume/wanawake ovyo. Mtu wa namna hii unafikiri Mungu atawezaje kumsaidia hitaji la moyo wake, ambalo anamwomba kila siku.

Unakutana na mtu anamwomba Mungu amponye na ugonjwa fulani ulioshindikana hospital, wakati huohuo anahaingaika na waganga wa kienyeji kutafuta tiba ya ugonjwa wake. Mungu yupi atamjibu ndugu huyu, anayechanganya Mungu wa kweli na miungu mingine, ambayo ni chukizo mbele za Mungu.

Tukielewa hili inaweza kutusaidia, usitake Mungu akufanyie jambo fulani wakati hutaki kuachana na ya dunia. Utakapokubali kurudi kwa Yesu Kristo miguu yote miwili, na si mguu mmoja nje na mguu mmoja ndani, utafanikiwa katika mambo yako.

Mungu wetu anajibu kabisa, hili tunaliona kupitia maandiko yake Matakatifu kutoka biblia;

REJEA: BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu. ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. 2 NYA. 7:12‭, ‬14 SUV.

Ukiomba toba Mungu atakusamehe, ukimwomba Mungu juu ya eneo lolote juu ya maisha yako, atakujibu sawasawa na hitaji la moyo wako. Ilimradi umeomba kwa mapenzi yake.

Hebu tujiulize tumezuia maombi mangapi kwa kushindwa kusamehe wengine waliotukosea, alafu tunataka sisi tusamehewe na Mungu? Unakuta jambo ambalo limezuia majibu ya mahitaji yetu ni kutosamehe wengine.

Unakuta mtu anapima makosa ya kusamehe na makosa asiyoweza kusamehewa, wakati huo huo anataka Mungu amsamehe maovu yake ambayo mengine ni aibu hata kutamkwa mbele za watu.

Hebu fikiria dada/mama ametoa mimba zaidi ya moja, Mungu amemwacha labda atatubu kwa kosa alilofanya. Kweli inatokea siku anaamua kutubu na Mungu anamsamehe, ila yeye anatokea mtu anamkosea anashindwa kumsamehe mtu huyo. Unaweza kuona ni jinsi gani tunazuia majibu yetu kutoka kwa Mungu.

Usiwe na shaka kuhusu Mungu kujibu hitaji lako, cha msingi uwe mwangalifu na maisha yako ya wokovu yasiwe na dosari sehemu. Kuwa na dosari yatakusababishia usijibiwe maombi yako kama tulivyosoma NENO hapo juu.

Ili maisha yako ya wokovu yazidi kuwa imara, endelea kuimarisha uhusiano wako na Mungu wako, usikosee njia ukategemea Mungu ataendelea kuwa na wewe.

Ili Mungu aendelee kujibu maombi yetu, tuhakikishe maisha yetu ni safi mbele zake, tusijichanganye na maovu hatutajibiwa mahitaji yetu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com