Usishangae kwa uyaonayo kwa watu wanaoona wapo sahihi kwa njia waziendeazo, usitaajabu kuona watu wanamwamini mtumishi wa uongo. Hata kama wanaambiwa hapo walipo sio sehemu salama ya kuwaogoza wafike kwa Baba mbinguni, hawatakuelewa na ikiwezekana watakuona hujui chochote.

Neno la Mungu lilishasema, wapo watu wana masikio lakini hawasikii kitu, wapo watu wana macho ya kuona ila hawaoni chochote.

Macho yao ya ndani yametiwa giza wasipate kujua nuru, masikio yao yametiwa pamba wasipate kuelewa wanachosikia. Wawe wanaambiwa chochote kilicho kinyume na Kristo wataona sawa tu.

Wakati wewe unahaingaika kumvuta gizani, yeye anajitahidi kujinasua kwako ili aendelee kubaki gizani ambapo wewe kiu yako atoke huko aje nuruni.

Huenda umefikiri haya ninayoyasema ni mtazamo wangu tu wa kibidanamu, usijali nitakupa andiko.

REJEA; Mwanadamu, wewe unakaa kati ya nyumba iliyoasi, watu ambao wana macho ya kuona, ila hawaoni, wana masikio ya kusikia, ila hawasikii; kwa maana ni nyumba iliyoasi. Ezekieli 12 : 2.

Uwezekano upo hata hayo maandiko unaweza ukafikiria sio halisi, unaweza kushika biblia yako ukasoma Ezekieli 12:2.

Sio kila nyumba ya ibada inamwabudu Yesu Kristo, zipo nyumba za ibada zimepitia mgongo wa kulitaja jina la Yesu ila wanamwabudu mungu/yesu wao.

Mafundisho ya kweli ya Mungu wengi hawayapendi, wengi wanakimbilia sehemu zinazotaja mafanikio ya mwili kuliko kumhubiri Kristo. Wengi wapo tayari kumwabudu mtu kuliko Mungu.

Sisemi kufanikiwa ni kubaya, sisemi kuwaheshimu manabii/wachungaji/mitume/maaskofu ni vibaya. Heshima ya mtumishi wa Mungu itabaki pale pale ila haiwezi kugeuza mtumishi yule kuchukua utukufu wa Mungu.

Huenda hata hapo umeanza kufikiri sipo sawa kusema hayo, hebu nikupitishe kwenye andiko hili tena huenda ufahamu wako ukajua ulipo.

REJEA; Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti;
nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo. 2 Timotheo 4 :3_4.

Hakuna njia ya mkato  kwa Mungu katika kufanikiwa kiroho na kimwili, neno la Mungu halina kigeugeu mwanzo na mwisho.

Neno limesema usinzini litabaki vile vile, neno la Mungu limesema usifanye uasherati lipo vile vile, neno limesema usiseme uongo lipo pale pale, neno la Mungu limeseme usilewe kwa mvinyo lipo vile vile, neno la Mungu limesema limesema…

Pamoja na hayo yote watu wamejiepusha na kweli ya Mungu, wamekimbilia hadithi za uongo na miujiza feki.

Niseme kwamba nyakati hizi ni zile zilizonenwa kuwa watu watakuja kuikataa kweli ya Mungu na kukimbilia mafundisho potofu.

Kusoma wanasoma ila hawaelewi wanachosoma, masikio ya kusikia wanayo ila hawasikii wanachoambiwa, macho wanayo na  hayana ulemavu ila hawaoni, akili wanazo ila hawaelewi kama wasio na akili.

Mungu hujawahi kushindwa jambo saidia kanisa lako, siku moja tuketi pamoja na wewe.

Samson Ernest.
+255759808081.