“Ndipo akawafungulia Baraba; na baada ya kumpiga Yesu mijeledi, akamtoa ili asulibiwe”, Mt 27:26 SUV.

Vipo vipigo vingi vinavyoleta matokeo hasi au mabaya kwa watu, wapo watu walipigwa hadi kufa, wengine wameachiwa vilema kwenye miili yao hadi leo baada ya kipigo na mateso makali.

Wakati wa mtu kupigwa mijeledi enzi za kirumi mtuhumiwa alivuliwa nguo na kuwekwa kwenye nguzo au kuinamishwa kwenye nguzo fupi, na kufungwa mikono yake miwili.

Kifaa cha kutesa kilikuwa na mpini mfupi wa mti ambao mikanda kadhaa ya ngozi imeambanishwa nayo, ikiwa na vipande vya chuma au mifupa iliyofungwa kwenye mikanda hiyo.

Vichapo vingi vilifanyika hasa maeneo ya mgongoni vikihusisha watu wawili, mmoja akimchapa mtuhumiwa kutoka upande mwingine wa pili, wakimchapa kwa zamu.

Kitendo hiki kilisababisha mwili wa aliyechapwa kukatwa kiasi kwamba mishipa ya damu ya vena na ateri, na hata wakati mwingine viungo vya ndani vilitoka nje. Unaweza kuona jinsi gani ilikuwa ni mateso yaliyoambatana na maumivu makali.

Mara nyingi sana mtuhumiwa alikufa wakati wa kupigwa mijeledi hii niliyokwisha kukueleza vile ilivyokuwa au ilivyotengenezwa. Iliharibu sana mwili wa aliyechapwa.

Kupigwa mijeledi kulikuwa ni mateso ya kutisha sana, hata baadhi ya filamu zilizoigiza kuhusu mateso ya Yesu zimejaribu kuonyesha hili, inaweza isiwe halisia sana ila inatupa picha vile ilikuwa wakati Yesu anateswa.

Bila shaka kutokana na kipigo alichopigwa Yesu inatupa picha kwamba kushindwa kwa Yesu kubeba msalaba wake kulitokana na kipigo kibaya alichokipata.

“Na walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka shamba, wakamtwika msalaba, auchukue nyuma yake Yesu”, Lk 23:26 SUV.

Kipigo hichi na mateso aliyoyapata Yesu hayakuwa ya bure, yalikuwa na faida kubwa sana, tunapaswa kuelewa hili kama waamini.

“Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona”, Isa 53:5 SUV.

Habari njema ni kwamba kupigwa kwake Yesu, mimi na wewe tumepona, yale mateso yake, kile kipigo cha Yesu, yale maumivu aliyopitia Yesu, sisi tumepona.

Tofauti kabisa na vipigo vingine wanavyokutana navyo watu wengine, kipigo cha Yesu kilikuwa na manufaa kwetu tunaomwamini, tunao ujasiri wa kwenda kwake akatuponya na shida zinazotusumbua.

Mateso unayopitia fahamu ya kwamba Yesu alishayalipia kwa gharama kubwa sana, wakati mwingine tunateseka kwa sababu ya kutokujua kile Yesu alifanya kwetu, na wakati mwingine ni kutomwamini Yesu Kristo.

Ukitaka kumfurahia huyu Yesu ni kumfahamu kupitia vizuri neno lake, hatuogopi kusema habari zake, mateso yake, kifo chake na kufufuka kwake, tunao ujasiri huo kwa sababu kuna mambo makubwa sana yamefanyika kupitia Yesu.

Tunalo jina lipitalo majina yote hapa duniani, hili ndilo jina ambalo mapepo yakisikia yanakimbia, jina lenye uweza mkuu, magonjwa yanamwachia mtu kupitia jina la Yesu Kristo, wazinzi wanaacha uzinzi wao, walevi wanaacha ulevi wao, pale tu wanapoamua kumpokea mioyoni mwao.

Kama bado hujampokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako, unayo nafasi leo, na kama una ugonjwa unakusumbua mwamini Yesu atakuponya ugonjwa wako unaokusumbua.

Soma neno ukue kiroho
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081