
Ukimtendea mtu wema kwa kumsaidia jambo fulani, na huyo mtu akafanikiwa katika maisha yake. Ikitokea huyo mtu akaja kuonyesha kutotambua msaada wako uliompa, au wema wako, inaweza kukuumiza moyo wako.
Vilevile kumtendea mtu yaliyo mema wakati anauhitaji, ukawa pamoja naye, ukamsaidia lile alikuwa na shida nalo. Yule mtu akaja kuonyesha kutambua kile ulimfanyia, huwa inatia moyo sana.
Kumsaidia mtu kwa kutegemea jambo fulani kwake, labda aje akusaidie na wewe ukiwa na shida. Ama ukategemea uje umtumie kwenye eneo fulani la kukuzalia wewe matunda, ikatokea akaenda kinyume na wewe.
Ule moyo wako wa kuwasaidia wengine, au kujitoa kwa ajili ya wengine, ule moyo unaweza ukakutoka, kwa sababu ulifanya hivyo kwa kutegemea kitu kutoka kwa uliyemsaidia.
Moyo wa kutoa au kujitoa kwa ajili ya wengine, huwa huondolewi na mabaya ya watu waliokutendea vibaya. Baada ya wewe kuwatendea mema, ikiwa neno la Mungu lipo la kutosha moyoni mwako litakufanya usikate tamaa.
Kama kichwa cha somo kinavyosema hapo juu, yapo matunda ya kutendea wengine mema. Hayo matunda unaweza ukavuna wewe na ukala, ama anakuja kula mtoto/watoto wako.
Tena wakati huo ukiwa haupo duniani, watoto wako ndio watavuna matunda ya baba/mama yao. Yale aliwatendea watu, au yale alimtendea mtu, inakuja kuwa msaada kwa mtoto wako.
Tunaona kwa Yonathani, Yonathani alimtendea mema mengi Daudi, wakati baba yake Sauli anamuwinda amuue, Yonathani alikuwa bega kwa bega na Daudi. Sio hilo tu Yonathani alimpa taarifa muhimu za kumsaidia Daudi asiuawe.
Biblia inaweka wazi kuwa Yonathani alimpenda sana Daudi kama roho yake, akadiriki kutoa vitu vyake kumpa.
Rejea: Nao Yonathani na Daudi wakaahidiana, kwa kuwa alimpenda kama roho yake mwenyewe. Ndipo Yonathani akalivua joho alilokuwa amelivaa, akampa Daudi, na mavazi yake, hata na upanga wake pia, na upinde wake, na mshipi wake. 1 SAM. 18:3-4 SUV.
Hii ilikuwa ishara kubwa sana ya kuonyesha upendo kwa Daudi, Yonathani alimaanisha kweli kuhusu urafiki wao.
Uhusiano huu wa Daudi na Yonathani ni habari ndefu, unaweza ukasoma kitabu cha 1 Samwel. Utapata habari kamili na kuona kwa uzuri zaidi hichi ninachokueleza hapa.
Hapa nakuonyesha mistari michache vile Yonathani matokeo ya wema wake yalivyotokea, matunda ya wema wake kwa Daudi, mtoto wake Yonathani alikuja kuyala.
Rejea: Kisha Daudi akasema, Je! Amesalia mtu mmoja katika nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema kwa ajili ya Yonathani? 2 SAM. 9:1 SUV.
Hilo ni swali mfalme Daudi anauliza, aliitiwa mtu wa kuweza kujibu hilo swali, hakujibu mtu yeyote asiye na uhakika na jibu lake. Haya ndio majibu ya swali lake;
Rejea: Palikuwa na mtumishi mmoja wa nyumba ya Sauli, jina lake Siba, basi wakamwita aende kwa Daudi; na mfalme akamwuliza, Wewe ndiwe Siba? Naye akasema Mimi, mtumwa wako ndiye. Mfalme akasema, Je! Hakuna hata sasa mtu ye yote wa nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema ya Mungu? Siba akamwambia mfalme, Yonathani anaye mwana hata sasa, aliye na kilema cha mguu. 2 SAM. 9:2-3 SUV.
Kumbuka kipindi Daudi yupo na Yonathani alikuwa bado hajawa mfalme, ijapokuwa alikuwa amepakwa mafuta ya kuwa mfalme wa Israel baada ya Mungu kumkataa Sauli.
Sasa wakati Daudi anauliza haya, Yonathani alishauwawa kwenye vita, kama tunavyosoma kwenye maandiko.
Rejea: Wafilisti wakamfuatia sana Sauli na wanawe, Wafilisti wakawaua Yonathani, na Abinadabu, na Malkishua, wana wa Sauli. 1 SAM. 31:2 SUV.
Wema wa Yonathani hakusaulika kwa Daudi, alitaka kulipa huo wema kwenye familia ya Sauli. Akampata mtoto wa Yonathani ambaye alikuwa kilema, akampa heshima kubwa.
Heshima ambayo ilimfanya mtoto yule akaogopa sana na kusema yale ya moyoni mwake kama inavyoonekana kwenye mstari huu.
Rejea: Akasujudu, akasema, Mimi mtumwa wako ni nini, hata ukamwangalia mbwa mfu kama mimi? 2 SAM. 9:8 SUV.
Labda unaweza kujiuliza ni heshima ipi alipewa huyu mtoto wa Yonathani hadi anaongea haya maneno, hebu tusome huu mstari hapa chini.
Rejea: Daudi akamwambia, Usiogope, maana bila shaka nitakutendea mema; kwa ajili ya Yonathani, baba yako, nami nitakurudishia mashamba yote ya Sauli, baba yako; nawe utakula chakula mezani pangu daima. 2 SAM. 9:7 SUV.
Mefiboshethi alipata heshima kubwa sana, heshima ambayo ilitokana na wema wa baba yake Yonathani aliomtendea Daudi.
Haya ni matunda ya kutendea wengine mema, bila kujalisha wengine huwa wanarudisha mabaya. Mungu hawezi kulipa baya kwa mtu wake ambaye anawatendea wengine mema.
Kama Yonathani angekuwa hai na kuona vile mtoto wake amepewa heshima kubwa na rafiki yake Daudi, angefurahi sana.
Hili liwe somo kwetu, tunapaswa kuwatendea wengine mema, hasa pale Roho Mtakatifu anapotusukuma kufanya jambo juu ya wengine.
Hatupaswi kuwa na mioyo migumu, tunaweza tusivune matunda ya wema wetu sisi kama sisi, lakini wakaja kuvuna watoto wetu.
MUHIMU; kama bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma neno la Mungu kila siku na kushirikishana tafakari. Tuma ujumbe wako kwa wasap namba hii +255 759 80 80 81, andika neno CHAPEO YA WOKOVU wakati unawasaliana nasi.
Mungu atusaidie sana tuweze kutenda wema.
Samson Ernest
www.chapeotz.com
+255 759 80 80 81.