“Basi, toeni matunda yapatanayo na toba; wala msianze kusema mioyoni mwenu, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba katika mawe haya Mungu aweza kumwinulia Ibrahimu watoto”, Lk 3:8 SUV.

Toba halisi kwa mtu inaambatana na tunda la haki, matendo yake yanapaswa kuwa mema kwa watu na mbele za Mungu.

“Akawaambia, Msitoze kitu zaidi kuliko mlivyoamriwa. Askari nao wakamwuliza, wakisema, Sisi nasi tufanye nini? Akawaambia, Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; tena mtoshewe na mshahara wenu” Lk 3:13‭-‬14 SUV.

Imani ya kweli inayookoa na kubadilisha maisha ya watu, lazima ionekane kupitia maisha ya kuacha dhambi na kuzaa matunda ya Kimungu.

“Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni”, Yn 15:16 SUV.

Wapo watu wanasema wanamwamini Kristo na ni wana wa Mungu, ila bado hawaishi maisha ya kumzalia Bwana matunda mazuri.

Watu wa namna hiyo ni kama ile miti isiyozaa itakayokatwa na kutupwa motoni

“Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni. Ambaye pepeto lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake; na kuikusanya ngano yake ghalani, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika”, Mt 3:10‭, ‬12 SUV.

Unapaswa kujiuliza ni kweli unamzalia Bwana matunda katika maisha yako ya wokovu? Unaenenda sawa sawa na neno la Mungu linavyokutaka? Unaishi maisha yenye ushuhuda mzuri katika maisha yako?

Ukiwa kinyume cha hapo na tayari umempokea Kristo moyoni mwako, unapaswa kubadili mwenendo wako na kuwa safi mbele za Mungu.

Ukiwa bado hujampa Yesu maisha yako, unapaswa kuacha matendo mabaya yasiyofaa mbele za Mungu na kutubu. Yesu ataingia moyoni mwako na utafanywa upya katika maisha yako.

Soma neno ukue kiroho
Mungu akubariki sana
Samson Ernest