Kila mmoja ana mawazo yake anayowaza, kile kimeujaza moyo wa mtu ndicho kinamtengezea mtu yule mawazo ndani yake.

Yanaweza yakawa mawazo mazuri sana, mawazo ya kuujenga ufalme wa Mungu kupitia huduma yako, mawazo ya kujenga nyumba nzuri, mawazo ya kujenga familia bora, mawazo ya kuimarisha kazi yako, na mengine mengi.

Pia yapo mawazo mabaya, mawazo potofu, mawazo yanayomkosea Mungu, mawazo yanayowaza kutenda mabaya mbele za Mungu.

Mawazo mabaya siku zote huzalisha matokeo mabaya, maana katika ubaya hakuna kizuri kinaweza kuzaliwa. Mpaka pale mtu mwenyewe atakapoamua kubadili mawazo mabaya kwa kumwendea Mungu.

Tunapaswa kulinda sana mioyo yetu, isiwe na mrundikano wa mabaya, tunapojiepusha kurundika mabaya ndani ya mioyo yetu, na mioyo yetu inapokuwa safi.Tunakuwa tumejiepusha na mawazo mabaya ndani yetu.

Rejea: Ee Yerusalemu, jioshe moyo wako usiwe na uovu, upate kuokoka. Mawazo yako mabaya yatakaa ndani yako hata lini? YER. 4:14 SUV.

Ondoa mawazo mabaya ndani yako, mawazo mabaya ni ya mtu ambaye ameanza kwenda kinyume na Mungu wake. Wewe uliyeokoka hupaswi kuwa na mawazo mabaya.

Rejea: Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano. MT. 15:19 SUV.

Moyo wako unapaswa kuwa na Neno la Mungu, unapokuwa na Neno la Mungu la kutosha, badala ya kuanza kuwaza mabaya. Unakuwa mtu wa kutafakari mambo ambayo yanaleta utukufu kwa Mungu wako.

Ukiona umejaa mawazo mabaya siku zote, alafu unasema umeokoka, jirudi upya ujihoji, kuna mahali utaona hauendi sawa.

Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.