Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake”, Mt 13:24‭-‬25 SUV.

Tukiwa kama wazazi kuna malezi mema tunajitahidi kuyapanda kwa watoto wetu, tunavyopanda hayo malezi mema tusifikiri Shetani atakaa kimya, na yeye atahakikisha anapanda na mambo yake mabaya.

Tukiwa kama watumishi wa Mungu tunaowapandia washirika wetu mafundisho ya kuwasaidia katika maisha yao, tufahamu yupo mwovu atakuja nyuma kuharibu ile mbegu njema tuliyopanda kwao.

Mfano huu tuliousoma kwenye andiko hilo mwanzo, kuhusu ngano na magugu unasisitiza kwamba Shetani atapanda sambamba na wale wanaopanda neno la Mungu kwenye mioyo ya watu.

Shamba lililonenwa katika andiko hili linawakilisha ulimwengu na mbegu njema inawakilisha watu waaminifu wa ufalme.

Lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu”, Mt 13:38 SUV.

Vile ambavyo injili inahubiriwa ulimwenguni kote na kuzaa matunda ya waamini wa kweli, ndivyo na Shetani anavyopanda wafuasi wake kwa wingi miongoni mwa wana wa Mungu, ili kuukabili ukweli wa Mungu uliopandwa kwao.

Lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika”, Mt 13:25‭, ‬39 SUV.

Kazi kubwa wanayofanya wajumbe wa Shetani ndani ya ufalme wa mbinguni unaoonekana ni kudhoofisha mamlaka ya neno la Mungu (Mwa 3:4) na kuendeleza uovu na mafundisho ya uongo (Mdo 20:29-30)

Yesu alizungumzia sana kuhusu udanganyifu mkubwa uliopo kati ya watu wake uliosababishwa na hao wanaoitwa Wakristo, ambao ki uhalisia ni walimu wa uongo ila wamejificha kwenye vazi la ukristo.

Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi”, Mt 24:11 SUV.

Hali ya kuwepo kwa wingi wajumbe wa Shetani kati kati ya wana wa Mungu, itakwisha pale Mungu atakapoangamiza waovu wote mwisho wa dunia.

Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi, na kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watakapong’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio, na asikie”, Mt 13:40‭-‬43 SUV.

Mbinu kubwa anayotumia Shetani ni kuwaingiza watu wake kwa siri kwa wana wa Mungu, mnakuwa kundi moja lenye watu wenye kazi ya kuharibu kweli ya Mungu iliyopokelewa ndani ya mioyo yenu, unaweza usitambue haraka kama huna neno la Mungu.

Hili halitaepukika kamwe, huwezi kusema kwetu hawapo watu wa namna, unapaswa kufahamu hili, maana tunao kwenye makundi yetu ya kanisa, tukifikiri nia yetu ni moja ila sivyo hivyo tunavyowaza au kufikiri au kuamini.

Muhimu ni kukomaa kiroho na kuwa na neno la Mungu la kutosha mioyoni mwetu, hii itatusaidia kuwatambua wajumbe au maajenti wa Shetani waliojiingiza katikati yetu.

Nakukaribisha kwenye kundi la wasap la kusoma neno la Mungu kila siku na kupata muda wa kutafakari kile umesoma, ukipenda wasiliana nasi kwa wasap +255759808081, utaunganishwa.

Soma neno ukue kiroho
Mungu akubariki sana
Samson Ernest