Haleluya,

Huenda umeona nimekuuliza swali gani hili, lakini pamoja na kuona hivyo, nikuombe tuwe pamoja hapa.

Huenda hujawahi kujiuliza hili swali, na wala hujawahi kufikiria kabisa kuhusu hili jambo la kuhusu miaka yako ya kuishi hapa duniani.

Haijalishi utaogopa wala haijalishi kujisahaulisha kwako inaweza kukufanya usife siku moja, kufa kupo pale pale sema itategemeana utakufa katika hali gani. Ukiwa mwenye dhambi au ukiwa unaishi maisha matakatifu.

Kifo kipo kwa mwanadamu, wachache sana utawapata kama akina Henoko na Elia, hawa hawakuonja mauti kama wanavyokufa wengi leo. Baada ya hao, tangu mtoto mpaka nafikia utu uzima, sijawahi kusikia mtumishi fulani wa Mungu amenyakuliwa na Mungu.

Kwa maana hiyo wengi wetu tutarudi mavumbini, kama yasemayo maandiko matakatifu. Ikitokea bahati ukakutwa na siku ya mwisho, ambayo ni siku ya unyakuo ukakutwa hai, napo mshukuru Mungu kwa kutoonja mauti.

Rejea: Wamrudisha mtu mavumbini, usemapo, Rudini, enyi wanadamu. ZAB. 90:3 SUV

Tunajua wote ipo siku tutaitwa marehemu, uhakika huo upo na tunaweza kukubaliana kwa pamoja kuhusu hili la kifo.

Umri tuliopewa wa kuishi hapa duniani, ni miaka michache sana kama tutakuwa na kazi ya kuifanyia hiyo miaka. Pia tunaweza kuiona ni mingi sana kama hatutajua ukomo wetu wa kuwa hai.

Unaweza kuishi unavyoweza kuishi kwa kutumia uhuru ulionao sasa, pia unaweza kuishi maisha yeyote ya anasa kwa kadri utakavyoweza. Ukiwa na uhakika una nguvu na umri bado unaruhusu kufanya hayo, ukashangaa siku moja Mungu akakuambia hapo ulipofikia imetosha.

Rejea: Umezipunguza siku za ujana wake; Umemvika aibu. ZAB. 89:45 SUV

Wakati unajivuna una miaka mingi ya kula ujana, Mungu anatazama uovu wako anasema miaka 25 au 30 au 35 uliyoishi inatosha kabisa. Nakunyang’anya uhai wangu, subiri siku ya hukumu yangu. Maana uliambiwa acha dhambi hukutaka kusikia, watumishi wa Mungu walikuletea injili takatifu ukaikataa mwenyewe.

Upo duniani kwa kipindi kifupi mno ndugu yangu, kama una miaka 30 leo maana yake umebakisha miaka 40 au 50, kama una miaka 40 leo maana yake umebakisha miaka 30 au 40. Na kama una miaka 60 maana yake umebakisha miaka 10 au 20. Huo umri ni wa mtu mwenye nguvu za kuweza kufanya shughuli zake.

Wapo wanaopata neema ya kufika miaka 120, lakini wanakuwa wazee sana wasiojiweza kwa lolote. Wapo wanapata neema ya kufika miaka 100 na wapo wanaopata neema ya kufika miaka 90.

Ila maandiko matakatifu yanatupa ukomo wa miaka fulani tukiwa na nguvu za kufanya shughuli mbalimbali bila tatizo lolote. Ambapo ukivuka hapo, unakuwa huna tena uwezo wa kuzunguka huku na kule kama mwenye nguvu.

Rejea: Siku za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara. ZAB. 90:10 SUV.

Hebu kaa utafakari, utautumiaje umri ulionao sasa kumzalia Mungu matunda au bado unaona una miaka ya kutosha. Kwa mjibu wa maandiko matakatifu, una muda mfupi mno wa kuweka alama njema kabla umauti haujakufika.

Mauti haitaangalia ulikuwa mchungaji, nabii, mtume, mwalimu na mwinjilisti, uzee ukishakufika kinachofuata ni umauti. Hakikisha unautumikia ujana wako vizuri, hakikisha miaka yako ya uzee unaimaliza vizuri.

Unapofanya kazi zako, jua una muda mfupi wa kuwepo kazini, unapofanya huduma ya Mungu jua una muda mfupi sana wa kufanya hiyo huduma. Siku yaja hutokuwa na nguvu tena ya kutumika shambani mwa Bwana.

Umekosana na watu, tafuta amani nao, hakuna mwenye leseni ya kuishi milele. Achalia moyoni mwako waliokukosea, hujui kesho yako ipo vipi, ukipuuza utaikosa mbingu hivi hivi kizembe.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu
www.chapeotz.com
+255759808081.