Mtazamo wako juu ya Bwana unaweza kukufanya ukawa jasiri mbele za Mungu, na shida zingine unazokutana au unazopitia. Ukaziona si kitu sana kwako, maana unajua uliyenaye ndani yako ni zaidi ya hayo uliyokutana nayo.

Pia mtazamo wako juu ya Bwana, unaweza kukufanya ukaendelea kunyanyaswa na shida yako. Sio kana kwamba Mungu hawezi kukusaidia kuvuka hilo jambo, unashindwa kuvuka kwa sababu mtazamo wako juu ya Bwana ni tofauti kabisa.

Kuna majaribu yamewabana watu vibaya kutokana na vile wanavyomtazama Mungu wao. Wana hofu nyingi sana, wanaona kama vile wanayopitia Mungu hawezi kuwasaidia. Na kama wanajua Mungu anaweza, ule uhakika kama anaweza kuwasaidia, kwao ni mdogo sana.

Hujawahi kuona unamwambia mtu, Mungu atakuponya na ugonjwa huo, Mungu atamponya mzazi wako, Mungu atamponya mtoto wako, Mungu atamponya mke/mume wako. Lakini pamoja na kuitikia kuwa Mungu atamponya, unamwona usoni anaonyesha ana mashaka mengi sana.

Yapo mambo mengi tunaona Mungu amechelewa kutujibu ila ukiangalia ukweli wake. Utaona sio kwamba Mungu amechelewa kutujibu maombi yetu, mitazamo yetu ndio inatufanya tuone bado. Kumbe Mungu alishajibu siku nyingi, au ameshindwa kutujibu kutokana na mitazamo yetu hasi.

Mungu ni mweza wa yote, hakuna lililogumu kwake, tunaposema hakuna, uwe na uhakika kweli hakuna lililogumu kwake. Usiseme tu mdomoni alafu moyoni unakataa kabisa hili.

Uweza wa Mungu unaweza kusambaratisha milima, milima inatii uweza wa Mungu. Milima inaogopa uweza wa Mungu, kama milima inaweza kuogopa nguvu ya Mungu. Hilo tatizo lako ambalo linakusumbua sana, unafikiri ukilipeleka mbele za Mungu litashindikana?

Unaweza kusema haiwezekani milima ikamwogopa Mungu, itashindikanaje wakati Mungu mwenyewe ndio ameiumba? Kama hilo ni gumu kuamini, na Neno la Mungu nalo utashindwa kuliamini?

Rejea: Milima ilikuona, ikaogopa; Gharika ya maji ikapita; Vilindi vikatoa sauti yake, Vikainua juu mikono yake. HAB. 3:10 SUV.

Haleluya, sijui kama umeanza kunipata vizuri kuhusu haya ninayokueleza hapa, kama huwezi kuamini hata Neno la Mungu. Utakuwa unajitafutia matatizo mwenyewe, mtu yeyote aliyeokoka anapaswa kuliamini Neno la Mungu.

Umeona hapo katika huo mstari, milima ilipomwona Mungu, iliogopa, ikaruhusu maji yakapita. Kama hili linawezekana kwa Mungu, je! Shinda yako itashindikanaje kwake? Lazima iwezekane.

Tena sio milima tu, jua na mwezi vinasimama kupisha miale ya Mungu, ni vitu vinavyoonekana kibinadamu haviwezekani ila kwa Mungu vinawezekana kabisa.

Rejea: Jua na mwezi vikasimama makaoni mwao; Mbele ya nuru ya mishale yako ilipotapakaa, Mbele ya mwangaza wa mkuki wako umeremetao. HAB. 3:11 SUV.

Hebu badili namna ya kufikiri juu ya Bwana, huenda umezuia baraka zako nyingi sana kutokana na kumwona Mungu kwa namna ya kushindwa kukusaidia shida yako.

Mungu wetu ni mweza wa yote, acha maneno ya wanadamu, acha kuumizwa na majibu ya madaktari. Jibu lako lipo kwa Mungu mwenyewe, nenda mbele zake kwa ujasiri mkubwa atakusaidia.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com